Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo ya Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Sikitu Saimoni akiongea na watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya wa mikoa ya Dodoma na Singida wakati wa mafunzo ya virutubishi mchanganyiko yanayoendeshwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa kushirikiana na TFNC jijini Dodoma


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Mafunzo  ya Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Sikitu Saimon amesema kwamba Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kupitia mradi wa Boresha Lishe umepanga kugawa virutubishi mchanganyiko katika mikoa ya Dodoma na Singida kwa ajili ya kupambana na utapiamlo kwa watoto chini ya miaka 2.

Sikitu amebainisha hayo wakati wa mafunzo ya matumizi ya virutubishi mchanganyiko kwa watoa huduma za afya wa mikoa ya Dodoma na Singida yanayofanyika kwa siku 3 kuanzia tarehe 01/04/2019 hadi tarehe 03/04/2019 katika ukumbi wa Ujenzi jijini Dodoma. Mafunzo hayo yametolewa kwa washiri kutoka vituo 40 vya wilaya za Bahi, Chamwino, Ikungi na Singida Vijijini.

Sikitu amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma ili waweze kuwasimamia na kuwaelekeza walengwa juu ya njia sahihi ya matumizi ya virutubishi hivyo kwa ajili ya kupambana na utapiamlo.

 “Tanzania sasa tunakabiliwa na aina mbili za utapiamlo; utapiamlo wa virutubishi vilivyozidi na utapiamlo wa upungufu wa virutubishi. Aina ya kwanza ya utapiamlo inawakabili sana watu wazima lakini hii aina ya pili inawakabili sana watoto wadogo chini ya miaka mitano. Athari ya utapiamlo kwa mtoto, humuathiri ukuaji wake kimwili na kiakili, na matokeo yake hata shuleni tunapata wanafunzi wasiofundishika au wasioelewa. Hivyo wakati sahihi wa kupapambana na utapiamlo kwa mtoto ni katika siku 1000 za mwanzo ya maisha yake kwa kuhakikisha mama anapokuwa mjamzito anapewa lishe bora, na mtoto anapozaliwa kwa miezi sita ya mwanzo anyonyeshwe maziwa ya mama pekee, na anapotimiza umri wa miezi sita hadi miaka miwili ni kuhakikisha anapewa chakula kilichoongezewa virutubishi mchanganyiko” amesema Sikitu Saimon.

Afisa Lishe kutoka WFP, Neema Shosho, amesema kwamba mradi wa Boresha Lishe unatekelezwa katika Wilaya nne za mikoa ya Dodoma na Singida ambazo ni Bahi na Chamwino kwa mkoa wa Dodoma, Ikungi na Singida Vijijini kwa mkoa wa Singida. Pia amesema kwamba mradi huu unatekelezwa kwa muda wa miaka 5 kuanzia mwaka 2017 na utakamilika mwaka 2022 ambapo awali mradi ulikua unagawa unga wa kutibu utapiamlo wa kadiri na unga lishe kwa wajawazito, wanawake wanaonyonyesha, na watoto wadogo wenye umri chini ya miaka miwili, zoezi lililokuwa linafanyika kila mwezi kwa mwaka mzima.

“Baada ya kufanyika tathimini na kubaini kuwa chakula kinachozalishwa na kaya katika maeneo ya mradi kinakuwa hakina virutubishi vya kutosha. Hivyo tukaona njia bora ni kuwapatia virutubishi mchanganyiko ambavyo vitaongezwa kwenye chakula. Kwa hiyo sasa tunabadilisha utaratibu, hatutakuwa tunagawa tena unga kama awali kwa kipindi chote cha mwaka mzima bali tutakukwa tunagawa katika kipindi cha mahitaji hasa wakati wa  kiangazi kuanzia  mwezi Oktoba hadi mwezi Machi” Amesema Neema Shosho.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: