Halmashauri ya Kisarawe inatarajia kuanza ujenzi wa shule ya bweni ya wasichana baada ya harambee tokomeza zero iliyofanyika Machi 30,2019.
Akiongea na Waandishi wa Habari leo,Mkuu wa wiliya ya Kisarawe Jokate Mwegelo amesema baada ya mafanikio yaliyopatikana kwenye harambee tokomeza zero taratibu za ujenzi zimeanza.
“Tumefanikiwa kupata shilingi 915,174,000 kati ya shilingi 1.38 bilioni ambazo zilikuwa ndio lengo letu katika harambee iliyofanyika kwetu ni mafanikio makubwa yanayowezesha kuanza ujenzi” amesema Jokate.
Amesema fedha hizo zinajumuisha ahadi,vifaa vilivyotolewa pamoja na fedha taslimu shilingi 80,641,000 .
“Ziko ahadi nyingi zilizotolewa ikiwemo madarasa sita ambayo ni sawa na shilingi 120 milioni,mabweni 2 sawa na 160 milioni,maabara,mifuko 1890 ya simenti,mbao pamoja na mabati”amesema
Jokate amesema tayari eneo kwaajili ya ujenzi wa shule hiyo lililotolewa na wananchi limeshasafishwa na wahandisi waliojitolea wameanza kupitia michoro ya majengo hayo kwaajili ya kuanza ujenzi.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Musa Gama amesema shule hiyo itakayokuwa na kidato cha kwanza hadi cha sita itakuwa ya mfano na itasaidia kuongeza kwa kiwango kikubwa kiwango cha kufaulu.
”Jambo tunaloenda kulifanya ni shirikishi ndio maana tunaungwa mkono na wadau mbalimbali ikiwemo wananchi waliojitolea ardhi kwaajili ya ujenzi wa shule hii ili kuongeza kiwango cha ufaulu”amesema Gama.
Post A Comment: