Na WAMJW - NJOMBE
Serikali
ya awamu ya tano imefanikiwa kuvuka kiwango cha upatikanaji wa dawa
muhimu kwa binadamu kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika
ngazi ya Hospitali ya Wilaya kwa kuwa na idadi kubwa ya dawa muhimu
zinazopatikana kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alipotembelea Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa
wa Njombe kujioinea hali ya utoaji wa huduma.
Waziri
Ummy Mwalimu aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Zainab
Chaula pamoja na watendaji walio chini ya Wizara yake, amesema kuwa
Serikali ya awamu ya tano imeendelea kuboresha upatikanaji wa dawa kwa
wananchi huku ikipitiliza kiwango kilichowekwa na WHO kwa kuwa na dawa
muhimu 312 huku kigezo kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani kikiwa ni
dawa 30.
“Tuna
mfumo wa ukusanyaji wa taarifa kuanzia ngazi ya zahanati, kituo cha
afya mpaka hospitali unaotuwezesha Serikali kutambua mahitaji na
matumizi ya dawa katika vituo vya kutolea huduma” amesema Waziri Ummy
wakati akifafanua namna ya Serikali ilivyojipanga kupata takwimu sahihi
za dawa.
Waziri
Ummy amesema kuwa zipo propaganda zinazoendeshwa na watu wenye
ushawishi ambao wamekuwa wakiwahadaa wananchi kwa kusema kuwa dawa
hakuna ili hali dawa zipo na zinapatikana katika vituo vya kutolea
huduma.
“Ni
lazima tumtendee haki Rais wetu DKt. John Pombe Magufuli, amefanya
makubwa kwenye Sekta ya Afya kwa kuboresha upatikanaji wa Dawa,
tunaposema tumeongeza upatikanaji wa dawa maana yake dawa zinapatikana
kwa urahisi hata kwenye vituo binafsi” amesema Waziri Ummy,
Waziri
Ummy amezitaja dawa zenye kipaumbele kikubwa zikiwemo Dawa za kudhibiti
maambukizi ya bakteria (Antibiotics), Dawa za kudhibiti Malaria, Dawa
za magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Dawa za uzazi salama pamoja na Dawa za
maumivu.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa
Ofisi yake kupitia Waziri wa Afya wako mbioni kuwasilisha muswada wa
Bima ya Afya ambao utawawezesha wananchi wote sasa kuwa na bima ya afya.
Aidha,
Dkt. Chaula amewataka watumishi katika Hospitali hiyo kuwahamasisha
zaidi wagonjwa kujiunga na huduma za bima ya afya ili kuwa na uhakika wa
matibabu pindi wanapougua.
“Niwaombe
watendaji wote hapa kuwasisiza wagonjwa wanaofika hapa kupata matibabu
kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya” Alisema Dkt. Chaula.
Naye
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Winfred Kyambile amesema kuwa
hali ya upatikanaji wa huduma imeimarika kutokana na mapato kuongezeka
hivyo kuiwezesha Hospitali kutoa huduma bora kwa wananchi.
Dkt.
Kyambile amesema kuwa kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa imesaidia
kuongezeka kwa mapato hospitalini hapo, amesema kuwa hapo awali mapato
ya hospitali hiyo kwa mwezi yalikuwa Shilingi Milioni 12 huku sasa
mapato hufikia Shilingi milioni 90 mpaka 100, fedha ambazo amesema
wanazitumia kuboresha huduma za afya katika hospitali hiyo.
Post A Comment: