Kiasi Cha Shilingi bilioni 1.2 kimetumika kununulia vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya vyuo vya ualimu vya umma 18, kwa lengo la kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji katika vyuo hivyo ili kuzalisha walimu bora na wanaoendana na ulimwengu wa Teknolojia.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu Profesa James Mdoe kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati wa halfa ya utoaji vifaa mbalimbali vya TEHAMA zikiwemo Kompyuta 300, UPS 300 na Projector 100 kwa ajili vyuo hivyo vya Ualimu.
Katika hotuba yake, Profesa Mdoe amesema serikali ya Tanzania inawashukuru washiriki wa maendeleo ambao ni serikali ya CANADA kwa kufadhili mradi wa kuendeleza na kuboresha Elimu ya Ualimu (TESP ) kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Profesa Mdoe pia amewaasa Wakuu wa Vyuo kutumia vifaa hivyo kwa malengo yaliyo kusudiwa na ametoa onyo kwa Wakuu wa vyuo wote wanauhujumu jitihada za serikali za kuboresha miundombinu ya vyuo vya Ualimu kuacha mara moja tabia hiyo na kuwataka watumishi wote kutanguliza maslahi ya Taifa ikiwa ni pamoja na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
“ Nipende kuwasihi watumishi wote wa Wizara ya Elimu na hasa Idara ya manunuzi kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni wakati wa kutekeleza majukumu"
Vyuo vya Ualimu vya Umma ambavyo vimepata vifaa hivyo ni pamoja na Dawaka, Ilonga, Mandaka, Mhonda, Murutunguru, Mamire, Ndala,Singachini, Shinyanga na Vikundi.
Vyuo vingine ni Patandi, Tarime, Mpuguso, Simbawanga, Mpwapwa, Tukuyu , Morogoro na Korogwe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ualimu nchini Augustino Sahili ameiomba serikali kuharakisha kukamilisha mpango wa kuunganisha vyuo vyote vya Ualimu vya umma na Mkongo wa Taifa.
Imetolewa na:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
9/3/2019
Post A Comment: