Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kamati ya uhamasishaji iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda iendelee kutumika kufanya uhamasishaji kwa klabu zote zinazowakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.
Ameyasema hayo leo Jumatatu Machi 25, Ikulu jijini Dar es Salaam katika mkutano uliowakutanisha wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ pamoja na bondia Hassan Mwakinyo.
“Iwe ni timu ya taifa au klabu yoyote ile inayocheza katika mashindano hata kama ni wiki ijayo wewe endelea kwa sababu tunakuamini pamoja na watu wako na tunaamini kamati hii itatufikisha mbali,” amesema.
Pia Majaliwa amesema kampeni ya Watanzania watambue utanzania umeweza kudhihirika jana katika Uwanja wa Taifa kutokana na kila mtu alivyojitoa katika kuitangaza mechi ile.
“Mtu mmoja mmoja wasanii walivyokuwa wamevaa nguo zinazoonyesha Utanzania wao wa kuhamasisha watu kwenda uwanjani hakika waliobaki nyumbani walikuwa ni wachache kuliko waliokwenda uwanjani, ni jambo ambalo linapaswa kupongezwa,” amesema Majaliwa.
Majaliwa amesema katika mchezo wa jana, licha ya Uwanja wa Taifa kuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 60,000 lakini walioingia jana walikuwa 63,000.
Pia, Majaliwa amesema ana matumaini makubwa na bondia Hassan Mwakinyo hasa katika kuinua na kuitangaza nchi kupitia mchezo wa ngumi kutokana na kufanya vizuri katika mashindano.
Amesema bondia huyo ana historia nzuri katika mchezo wa ngumi lakini awali kilio chake kikubwa kilikuwa ni kukosa wadhamini kabla ya wizara ya michezo kumtafutia Sportpesa.
“Huko kwenye ubondia kulikuwa na makando kando lakini sasa kumeanza kutulia, tunaenda vizuri na ndiyo maana bwana Hassan (Mwakinyo) anaendelea vizuri katika michezo yake,” amesema.
Mbali na hilo pia Majaliwa alimuomba bondia huyo kuwashauri waangalizi wake kuleta mchezo mmoja nchini ili Watanzania wapate nafasi ya kumuona ana kwa ana akishughulika.
Post A Comment: