Muonekano wa Jengo la Wizara ya Madini linalojengwa katika Mji wa Serikali eneo la Ihumwa.
Waziri wa Madini Doto Biteko, (mwenye koti) Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (wa tatu kushoto) na Prof. Simon Msanjila (mwenye tisheti nyekundu) wakikagua maeneo maeneo mbalimbali ya jengo la Wizara
Waziri wa Madini Doto Biteko ( wa kwanza kushoto), Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (wa pili kushoto ) na Katibu Mkuu wa Madini Prof. Simon Msanjila, wakijadiliana jambo wakati wakikagua maeneo mbalimbali ya jengo la Wizara, eneo la Ihumwa.
Waziri wa Madini Doto Biteko katikati na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakiangalia kitu wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wizara, Ihumwa.
…………………….
*Viongozi Waandamizi Madini watembelea jengo la Wizara, Ihumwa
*Waziri Biteko asema wizara iko tayari kuwahudumia watanzania kutokea Ihumwa
*Mkandarasi aahidi kukamilisha ujenzi ndani ya siku Tano
Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Madini, wakiongozwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko wametembelea Jengo la Wizara ya Madini lililopo mji wa Serikali eneo la Ihumwa, Jijini Dodoma kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi huo.
Akizungumza baada ya kukagua jengo hilo, Waziri wa Madini Doto Biteko amewahakikishia watanzania wote pamoja na wadau wa madini kuwa, wizara iko tayari kuwahudumia kutokea eneo hilo la Ihumwa pindi itakapohamia na kuwataka watumishi kujiandaa kuhamia eneo hilo mara baada ya mkandarasi kukabidhi jengo kwa wizara. Vilevile, Waziri Biteko amezitaka taasisi nyingine zenye uhitaji wa kutumia madini ya mawe yanayopatikana nchini ikiwa ni pamoja na mable, kuwa wizara iko tayari kuwasaidia kwa kuwaunganisha na wajeta wake.
Pia, amemshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kutokana na msukumo alioutoa kuhakikisha ujenzi wa majengo ya serikali unakamilika kwa wakati. Aidha, amempongeza Mkandarasi kampuni ya Mzinga Holding Co. Ltd kutokana na kuongeza kasi ya ujenzi ikiwemo kuzingatia ubora nakuongeza kwamba, wizara imeridhika na ujenzi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, ameeleza kuwa, wizara imepanga kulifanya eneo la ofisi hiyo kuwa kijani kwa kuhakikisha inapanda miti ya aina mbalimbali na kuhakikisha kwamba eneo hilo linawekewa mazingira mazuri ya kuvutia.
Naye, Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila Amesema Mkandarasi Kampuni ya Mzinga Holding Co. Ltd imeahidi kuikabidhi Wizara jengo hilo ndani ya kipindi cha siku Tano zijazo “awali ujenzi ulianza kwa kusuasua lakini sasa uko katika hatua nzuri na mkandarasi amezingatia ubora,” amesema Prof. Msanjila.
Akizungumzia mahitaji ya ofisi na idadi ya watumishi, amemsema kwa idadi ya watumishi wa wizara Makao Makuu ofisi zilizopo katika jego hilo zinatosheleza mahitaji na kuongeza kuwa, kwa kuanza Idara zote na Vitengo vya Wizara vinatarajia kuhamia katika eneo hilo isipokuwa Idara ya fedha kutokana na masuala ya mfumo wa kifedha. Pia, ameeleza kuwa, wizara imetumia malighafi inayopatikana nchini yakiwemo madini ya mable ambayo yamepatikana kutoka kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini.
Kwa upande wake, Mkandarasi wa kampuni hiyo Hamisi Msangi ameihakikishia wizara kuwa , ndani ya siku tano zijazo, jengo hilo litakabidhiwa rasmi kwa wizara hiyo.
Post A Comment: