Afisa Uhamiaji Mkoa Mara na Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Fredrick Kiondo akiongea katika hadhara ambayo ni sehemu ya Warsha ya “Ushirikishwaji Wananchi katika Ulinzi na Usimamizi wa Mipaka” iyosimamiwa na Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM) iliyofanyika katika uwanja wa Tarafa Kijiji cha Sirari, Wilayani Tarime.
Mwezeshaji katika mkutano huo, Mrakibu Allya Mtanda akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika katika Kijiji cha Sirari, Wilayani Tarime.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano wa “Ushirikishwaji Wananchi katika Ulinzi na Usimamizi wa Mipaka” iyosimamiwa na Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM).
Wananchi wakigawiwa vipeperushi wakati wa mkutano wa “Ushirikishwaji Wananchi katika Ulinzi na Usimamizi wa Mipaka” iyosimamiwa na Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM).
WAKAZI na viongozi wa Kata za Sirari, Gwitiryo, Pemba na Mbogi pamoja na wakazi wa Kata ya Isebania (Kenya) wameahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo mpakani ili kupambana na wimbi la wahamiaji haramu wanaoingia katika nchini Tanzania na Kenya.
Hayo wameyasema wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Tarafa ya Kijiji cha Sirari, Wilayani Tarime. Mkutano huo ambao ni sehemu ya Warsha ya “Ushirikishwaji Wananchi katika Ulinzi na Usimamizi wa Mipaka” unasimamiwa na Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM) ni muendelezo wa kuwajengea uelewa wananchi waishio maeneo ya mipakani ili kushiriki katika suala zima la Ulinzi na Usimamizi wa mpaka katika maeneo yao.
Akifungua mkutano huo, Mgeni rasmi Kemore Kemore ambaye ni Katibu Tarafa wa Inchugu ameishukuru Idara ya Uhamiaji na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji kwa kuamua kukutana na wananchi wa pande zote mbili kupawatia elimu juu ya Uhamiaji Haramu, Usafirishaji Haramu, Usafirishaji wa Magendo wa Binadamu, na athari zake kwa Usalama wa Nchi.
“Nashukuru sana kwa Uhamiaji na IOM kuja hapa na kufanya mkutano na wananchi. Wananchi wakielimika basi hata hizi changamoto za mpakani zitapungua au kwisha kabisa, na niwaombe viongozi wenzangu na wananchi wote mliohudhuria hapa, yote mtakayofundishwa basi nanyi muwe walimu kwa wengine ambao hawakufika hapa’’ Ameeleza Kemore.
Mkutano huo ulishirikisha wananchi wa kawaida, madereva bodaboda na mabasi, wafanyabiashara, mamalishe, wajasiriamali, vijana, Viongozi wa vitongoji, vijiji, na Kata pamoja na wawakilishi wa taasisi na idara za serikalini zilizopo mpakani kwa pande zote mbili (Kenya na Tanzania).
Mzee Chacha Magatti, mkazi wa Kijiji cha Sirari alisema kuwa baada ya kupata elimu juu ya madhara ya wahamiaji haramu kwa usalama na uchumi wa nchi sasa yuko tayari kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wa nchi.
“Kwa kweli inabidi wananchi wa maeneo ya mipakani tuwe wazalendo kwa nchi zetu. Unakuta watu hawatambuliki wametokea wapi, wanapita vijijini kwetu, wanapitishwa na bodaboda na mafuso kwenda Tarime. Ukichunguza unaweza kusema watu hao ni wasomali au waethiopia. Sasa kwa jinsi tulivyoelimishwa katika mkutano huu, nimeona kuanzia sasa si vyema kukaa kimya. Nikiwaona lazima nitoe taarifa kwa wahusika ili wajiridhishe kama hawa watu wameingia kihalali.” Alisema Mzee Magatti.
kwa upande wake Diwani wa Kata ya Sirari Nyangoko amesisitiza kuwa kuna haja ya kuwa na mikutano kama hii angalau mara mbili kwa mwaka ili kujenga uelewa kwa wananchi na kuwakumbusha wajibu wao kwa nchi yao kwani ulinzi wa nchi unaanzia ngazi ya familia, kitongoji, Kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla.
Akichangia mada ya Magendo ya binadamu na bidhaa, Afisa kutoka TRA alisema kwamba pamoja na juhudi zinazofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kudhibiti uingizaji na usafirishaji nje bidhaa zinazotakiwa kulipiwa kodi, bado kuna baadhi ya watu wanashiriki katika magendo lakini juhudi zinaendelea kuwadhibiti.
Pia mtoa mada kutoka Polisi, Mkaguzi Msaidizi Juma alisema suala la uhalifu mpakani japo kwa sasa limepungua lakini bado ni changamoto ambayo polisi wanaendelea kupambana nayo. Wahalifu wakifanya matukio Tanzania wanakimbilia upande wa pili (Kenya).
Aidha maafisa Uhamiaji na wale wa Mamlaka ya Mapato kutoka Kenya wamewaasa wananchi kufuata sheria wakati wa kuvuka mpaka ili kuepuka kuingia matatani kwani mtu anaevuka mpaka ni lazima apite kituo cha uhamiaji na kama ana mizigo lazima apite KRA kwa ukaguzi.
Diwani wa Kata ya Gutiryo Mheshimiwa Adam Nyawambura aliungana na viongozi wengine katika kuishukuru Idara ya Uhamiaji kwa kuandaa warsha na mikutano na wananchi kwa kuwajengea uelewa wa mambo ambayo kwa mpakani yanaonekana kero kwa wananchi lakini yanatakiwa kufuatwa kwa mujibu wa sheria.
“Ni jambo jema kuja kwa wananchi na kuwaelimisha mambo yanayotakiwa kufuatwa kwa mujibu wa sheria za nchi, kuna mambo mengi wananchi wanadhani wanaonewa. Kumbe wanakuwa hajui sheria inasemaje, mfano mtu anaona shule ipo mita mia hapo Kenya anampeleka mtoto wake shule bila kufuata taratibu kwa kuwa hajui anatakiwa afanye nini, kumbe leo wananchi hasa wazazi wenye Watoto wao hapo Isebania watafuata utaratibu wa kupata vibali vya masomo kwa Watoto wao. Bila mkutano huu hii elimu tusingekuwa nayo.” Ameeleza Nyawambura.
Post A Comment: