Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, amesema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ina jukumu la kukusanya Sh. trilioni 18, hivyo ni wajibu wa kila mfanyabiashara mkubwa na mdogo kuhakikisha analipa kodi stahiki kwa wakati ili kuweza kukusanya kiasi hicho.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega kwa niaba ya Gambo, katika semina ya siku moja kati ya TRA na wafanyabiashara wakubwa wa Mikoa ya Kanda ya Kaskazini, iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Alisema makusanyo hayo ni sawa na asilimia 64.3 ya makadirio ya mapato yote ambayo ni Sh. trilioni 32, vyanzo vingine ni mikopo ambayo ni Sh. trilioni 8.9, misaada na mapato ya ndani ambayo siyo kodi pamoja na mapato ya halmashauri zote nchini ni shilingi trilioni 2.16.
Alisema anaamini kumeshafanyika marekebisho ya sheria za kodi na kupitishwa na bunge, hivyo ni wajibu wa kila mfanyabiashara mkubwa, mdogo na wengine wote kuhakikisha wanafahamu namna bora ya kukuza kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari.
Gambo alisema serikali imejikita katika miradi endelevu yenye malengo ya kutatua matatizo au kero za Watanzania wa kawaida na wa hali ya maisha ya chini, ili wapate matumaini mapya katika maisha.
Post A Comment: