Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, akizungumza kwenye uzinduzi wa Dar es Salaamya Kijani. Hlafa hiyo ilifanyika Chuo Kikuu Kishirikishi cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), na kuhudhuhuriwa na vijana wote wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa UVCCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala (kushoto), akiwa na mgeni rasmi katika uzinduzi wa Dar es Salaam ya Kijani, Katibu Mkuu wa UVCCM Mwal. Raymond Mwangwala (kulia).
Baadhi ya Vijana wa CCM wakiwa kwenye uzinduzi wa Dar es Salaam ya Kijani
Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Dar
es Salaam, umezindua kampeni ya ‘Dar es Salaam ya Kijani’ ikiwa na lengo la
kurudisha mitaa na majimbo yaliyokwenda upinzani.
Kampeni hiyo inalenga kuweka mikakati kwa kuanzia ngazi za
jumuiya zote za mkoa huo, kuanza kujipanga kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Akizugumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika Chuo
Kikuu Kishirikishi cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa
Dar es Salaam, Mussa Kilakala, amesema kuwa kampeni hiyo itachochea ustawi
zaidi wa CCM katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuzidi kukita mizizi katika ngazi
zote kuanzia mkoa hadi majimbo, wilaya hadi kata, na matawi hadi mitaa.
“Leo tunazindua kampeni yetu ya “Dar es Salaam ya Kijani
kuelekea serikali za mitaa 2019”, kampeni kabambe kwa ajili ya kuirejeshea CCM
mitaa iliyopotea katika uchaguzi uliopita ambayo kwayo itatusaidia kupata
ushindi mkubwa kimkoa katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 wa udiwani, ubunge na urais.
“Sote tu-mashuhuda kwamba katika uchaguzi uliopita wa 2014
wa Serikali za Mitaa na ule Mkuu wa 2015 tulipoteza baadhi ya mitaa, kata na
majimbo yaliyokuwa yakishikiliwa na CCM.
“Na sababu za kupoteza huko zinajulikana, sina haja ya
kuzirejea sasa. Hivyo sisi vijana wa CCM tunatambua kuwa ndiyo damu na roho ya
chama chetu, na kwamba tunao wajibu wa asili wa kusafisha njia katika kutimiza
malengo ya uwepo wa vyama vya siasa kikatiba ya kushika dola,” amesema Kilakala
Mwenyekiti huyo wa UVCCM, amesema kuwa CCM inahitaji
ushindi mkubwa kwa kuweka mikakati ya awali kwa kuwahusisha wanachama wa chama hicho
wa ngazi zote.
“Kampeni yetu hii itashuka katika wilaya, kata na matawi
yote katika Mkoa wetu ili kuwa na ufahamu wa pamoja na kuhakikisha kila Kijana
wa UVCCM anawajibika ipasavyo kuhakikisha falsafa ya Dar es Salaam ya kijani
yaani Dar es Salaam ya CCM inaenea kwa wanachama na wananchi ili ikifika wakati
wa uchaguzi tuvune wapiga kura wa kutosha.
“Nitakuwa mchoyo wa
fadhila kama sitatoa pongezi zangu za dhati kwa niaba ya Mkoa wa Dar es Salaam
kwa Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa na Rais Dk. John Magufuli kwa kutuongoza vyema
kupitia Serikali yetu ya CCM katika jukumu la kutatua changamoto za watanzania
na kuwaletea maendeleo.
“Tumejionea dhahiri shahiri namna yale yaliyochelewa
yakiwahishwa, yaliyoshindikana yakiwezekana, magumu yakiwa mepesi, yaliyokwama
yakikwamuliwa,”amesema Kilakala
Kwa upande wake mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa UVCCM, Mwal.
Raymond Mwangwala, amesema ameridhishwa na kasi kubwa inayofanywa na vijana wa
Dar es Salaam ya kuhakikisha chama kinapata heshima katika chaguzi zote.
“Leo ninachokiona hapa, hii ndiyo UVCCM ninayoijua na sina
shaka na uongozi wa mkoa kwani unafanyakazi kubwa na nzuri, ninachoweza kusema
kwenu ninawaomba sana vijana tukilinde chama na kuhakikisha tunapata ushindi
katika chaguzi zote.
“Na ikiwezekana si waachieni (upinzani) asimilia mbili tu
ya mitaa na pindi ikibidi hata hakikisheni tunachukua asilimia yote 100. Vijana
tushikamane na tulinde heshima ya chama
chetu,” amesema Mwal. Mwangwala
Mwisho
Post A Comment: