Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo
Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema haiwezi kuzungumzia chochote
kuhusu gharama za usajili wa mitandao ya kijamii inayotoa maudhui
mtandaoni kwa sababu ni sheria na ili kupunguza gharama hizo lazima
mchakato wa kisheria ufuatwe kwa kupitia bungeni.
Kauli
hiyo imetolewa jana na Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis
Mihayo wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya utangazaji kupitia
Televisheni na Redio za kawaida na mitandaoni (Blogs & Online Tv)
kutoka Kanda ya Ziwa Victoria uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu
wa Mkoa wa Mwanza.
Mhandisi
Mihayo alitoa kauli hiyo akijibu swali la Mmiliki wa Malunde Media
(Malunde 1 blog), Kadama Malunde aliyeiomba TCRA kupunguza gharama za
usajili wa Mitandao ya Kijamii ili kuwasaidia vijana walioamua kujiajiri
kupitia mitandao waendelee kutoa huduma za maudhui mtandaoni.
"Hizi
gharama wanazotozwa hawa watoa huduma za maudhui mtandaoni ni ndogo
ukilinganisha na zile gharama zinazolipwa na watu wa Televisheni na
Radio, kwanza watu wa Mtandaoni wana leseni ya kimataifa, anapochukua
habari anaenda kuzipakia kwenye mtandao zinaonekana dunia nzima lakini
nyinyi (Tv na Radio) mna leseni kulingana na eneo husika",alisema
Mhandisi Mihayo.
"Kwa
hiyo Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) hatuwezi kuzizungumzia chochote hizi
gharama za usajili kwa sababu ni sheria,sisi tunatekeleza sheria,kwa
hiyo hizi gharama nafikiri ukitaka zipungue ni lazima mchakato wa
kisheria ufuatwe kwa sababu lazima upitie bungeni",alieleza Mihayo.
Awali
akitoa taarifa ya vituo vya utangazaji wa maudhui Kanda ya Ziwa,
Mhandisi Mihayo alisema mpaka sasa TCRA inasimamia vituo 36 vya Redio,
Televisheni 3 na watoa huduma wanne wa maudhui mtandaoni waliosajiliwa
kwa mujibu wa sheria ambao ni Mohab Online Tv, Geita Online Tv, Binagi
Blog na Malunde Media.
"TCRA
inaendelea na zoezi la kuwabaini watoa huduma mtandaoni ambapo mpaka
sasa Kanda ya Ziwa tulishawatambua 24 na kuwatahadharisha kuacha kuvunja
sheria kati yao wapo waliotii agizo la Mamlaka kwa kusitisha kwa muda
upakiaji wa habari mtandaoni na wanaendelea na taratibu za
usajili",alisema.
"Wengine
wameendelea kukaidi agizo la mamlaka na kuendelea kuvunja sheria kwa
kisingizio eti wanaandika habari za viongozi mbalimbali wa mikoa na
wilaya,niwakumbushe viongozi hao kuwa sheria ya usajili wa watoa huduma
mtandaoni za Online Tv, Blogs,Online radio,simulcasting online Tv na
Radio,Weblogs ipo kwa ajili ya wote zikiwemo taasisi za serikali.
Hivyo
basi TCRA inawashauri viongozi waache kusaidia kuvunja sheria ama kwa
kujua au kwa kutojua kwa kuwatumia waandishi wanaopakia habari za
matukio mbalimbali yanayowahusu kwenye mitandao ya kijamii inayotakiwa
kusajiliwa,tutaendelea kuwachukua hatua za kisheria ili kila mtoa huduma
mtandaoni anafanya kazi kwa kufuata sheria"
"TCRA
inawafahamu watu wote wanaopakia maudhui mtandaoni hivyo wale
wanaoendelea kutoa maudhui mtandaoni ni lazima wafuate taratibu za
kisheria ikiwemo kujisajili,tunaendelea kuwafuatilia na watashughulikiwa
na vyombo vya kisheria",aliongeza.
"Kuna wale ambao wameamua kuhamishia kazi za blogs Instagram na Facebook, hawa nao tutawashughulikia",alisema Mhandisi Mihayo.
Post A Comment: