Na Mwandishi Wetu – New York Marekani
Tanzania
ni nchi mmojawapo duniani iliyofanikiwa kupiga hatua katika kuwawezesha
wanawake kijikwamua kiuchumi kwa kuwasaidia kupata mikopo isiyo na riba
inayowawezesha kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.
Hayo
yamesemwa leo na Mh Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, katika Mkutano Mkuu wa 63 wa Kamisheni ya Hali
ya Wanawake Duniani unaoendelea New York, Marekani.
Waziri
Ummy alieleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika uwezeshaji wa wanawake
kiuchumi kwa kuwapatia fursa za mikopo na kufanyia marekebisho Sheria
ya Fedha za Serikali za Mitaa ya mwaka 2018 ambayo imefuta Riba kwa
mikopo yote inayotolewa kwa wanawake kupitia Halmashauri.
Alisema
Halmashauri zimekuwa zikichangia asilimia 5 ya mapato yao ya ndani kwa
ajili ya mikopo kwa wanawake, matokeo yake kiwango cha fedha
zinazotolewa na Halmashauri kwa ajili ya mikopo ya wanawake kimeongezeka
kutoka bilioni 3.4 mwaka 2015/16 kufikia bilioni 16 mwaka 2017/18.
Waziri
Ummy alieleza kuwa tangu mwaka 2015 Tanzania imepiga hatua kubwa kwa
kutoa elimu bure ya Msingi na Sekondari na kufanya ongezeko la asilimia
80 katika uandikishaji wa watoto wa shule za msingi na ongezoko la
asilimia 20 kwa Sekondari.
Ameongeza
kuwa katika kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu bila vikwazo
vyovyote mwaka 2018 Serikali imefuta tozo ya kodi katika taulo za kike
(pads) na hivyo kupelekea upatikanaji wake kuwa rahisi na kwa gharama
nafuu ambapo mwanzo watoto wengi wa kike walikuwa wanakosa vipindi
madarasani kutokana na kukosa taulo hizo.
Katika
huduma za afya, Tanzania imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za
afya hususan huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na maboresho ya
miundombinu ya afya na chanjo. Kwa mwaka 2018/19 Kati ya vituo vya afya
518, vituo 304 vimekarabatiwa ili kuboresha huduma za afya ya mama na
mtoto ikiwa ni pamoja na huduma za upasuaji na hivyo kuwa na jumla ya
vituo 459 nchi nzima vinavyotoa huduma za dhalura na uzazi ukilinganisha
na vituo 109 mwaka 2015.
Na
katika sekta ya nishati Waziri Ummy alieleza kuwa Tanzania kupitia
mradi wa umeme vijijini (REA) imeweza kusambaza umeme katika vijiji
zaidi ya 7000 kati ya vijiji 15000 sawa na asilimia 46 ya vijiji vyote
nchini hili limesaidia sana kuwawezesha wanawake kupata fursa mablimbali
kutokana na upatikanaji wa nishati hiyo kwa urahisi kuanzisha miradi ya
kiuchumi ikiwemo viwanda vidogo vidogo.
Ameongeza
kuwa kwa mujibu wa Taarifa ya Utafiti wa Upatikanaji wa Nishati
Tanzania ya mwaka 2016 asilimia 32.8 ya kaya Tanzania bara zina Umeme,
na asilimia 44.2 Zanzibar. Upatikanaji wa umeme umewezesha huduma za
afya kupatikana kwa wepesi hasa huduma za uzazi, upatikanaji wa maji na
kurahisisha shughuli zingine za uzalishaji mali kwa wanawake.
Mkutano
wa 63 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa wa Hali ya Wanawake Duniani kwa
mwaka 2019 unaendelea jijini New York Nchini Marekani ukiwa na Kaulimbiu
inayosema "Mifumo ya Hifadhi ya Jamii, Huduma za Umma na Miundombinu
Endelevu kwa Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake na Wasichana".
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
(Kushoto) akiwa katika katika Mkutano Mkuu wa 63 Kamisheni ya Hali ya
Wanawake Duniani unaoendelea katika jiji la New York nchini Marekani.
Post A Comment: