WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa wizara, taasisi au mikoa
kuacha mara moja tabia ya kuwatumia waandishi wa habari binafsi katika
utekelezaji wa majukumu yao ya Kiserikali na kuwaacha wale ambao
wameajiriwa na Serikali katika ofisi zao kwa kazi hiyo.
“Kwanza
tabia hii ni hatari kwa usalama wa taarifa za Serikali. Nitumie nafasi
hii kukemea viongozi na watendaji wenye tabia za namna hii kuacha mara
moja tabia hizo zisizo kinyume na matakwa ya maadili ya utumishi wa
umma.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Machi 18, 2019)katika
ufunguzi wa Kikao Kazi cha 15 cha Maafisa Habari, Uhusiano na
Mawasiliano Serikalini, kinachofanyika katika ukumbi wa BOT jijini
Mwanza. Kikao hicho kinahudhuriwa na Maafisa Habari na Mawasiliano
takbaribani 400.
Katika
kuhakikisha suala hilo linakomeshwa Serikalini, Waziri Mkuu ameuagiza
uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
umpelekee majina ya kiongozi au mtendaji wa ngazi yeyote ile ambaye
bila sababu zozote anawapuuza waliajiriwa na Serikali kufanya kazi hiyo.
Waziri
Mkuu amesema Serikali inatumia rasilimali nyingi kuajiri, kuanzisha,
kuiendeleza na kuitunza kada ya maafisa habari Serikalini, hivyo,
maafisa habari waliopo wapewe nafasi ya kutekeleza majukumu yao kama
ilivyokusudiwa na Serikali.
Waziri
Mkuu amesema maafisa hao wanatakiwa wapewe ushirikiano na viongozi wa
taasisi wanazozitumikia ili habari za utekelezaji wa Serikali ziwafikie
wananchi badala ya viongozi na wataalamu wengine kukalia habari hizo. “Mawaziri na Wakuu wa Mikoa, simamieni Maafisa Habari kutimiza wajibu wao”.
Waziri
Mkuu amesema anafahamu changamoto nyingine kwa maafisa habari ambazo
husababishwa na viongozi au watendaji katika taasisi za umma na hasa
katika ngazi za Wizara, Mikoa na Halmashauri za kutotambua mchango wa
sekta ya habari katika maendeleo ya nchi.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema anazo taarifa za baadhi ya maafisa habari ambao
wana vifaa vyote pamoja na ofisi nzuri zenye kuvutia lakini bado
hawatimizi wajibu wao ipasavyo katika kutangaza shughuli za Serikali.
“Wengine
hawajui shughuli zinazofanywa na Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi
na Wakuu wa Sekta kwa siku, wiki hata mwezi…Taasisi haina taarifa.
Badilikeni, nenda mkakusanye taarifa na mzitoe hadharani”.
“Tambueni kwamba Serikali haitowavumilia Maafisa Habari wa namna hii kwani ni wazi kabisa kuwa hawatufai na ni mzigo kwa Serikali. Basi, wale wote wenye mienendo ya namna hiyo chukueni hatua, mjitathmini na mjirekebishe mara moja.
Amesema
maafisa hao ambao wamepata mafunzo ni lazima utendaji wao ukazingatia
maadili na weledi na wakati wote utekelezaji wa majukumu yao ujikite
katika kuboresha masilahi ya umma, kuepuka uchochezi, ushabiki, vijembe
na kuepuka kuandika habari zinazopandikiza chuki katika jamii.
Pia,
ameielekeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupitia
Idara ya Habari-MAELEZO ifanye tathmini ya kina kuhusu utendaji wa
maafisa habari hasa wale wanaoongoza vitengo na watakaoonekana kuwa
hawaisaidii Serikali waondolewe mmoja baada ya mwingine bila kupepesa
macho.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amesema kila nchi inayo misingi, utamaduni na tunu zake,
hivyo amewataka maafisa hao watambue kuwa wao ni sehemu muhimu katika
kusimamia na kuendeleza misingi,utamaduni na tunu za Taifa.
Amesema
maafisa hao hawana budi kuhakikisha wanabeba agenda za Kitaifa katika
utekelezaji wa majukumu yao kwani yapo mambo ambayo ni msukumo wa
kitaifa kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
“Kutokana
na haya kila tunachoandika ni lazima kiwiane na agenda zetu kitaifa
katika sekta mbalimbali. Kwa mfano: Kisiasa msukumo wetu ni amani na
utulivu, kiuchumi msukumo wetu sasa ni ujenzi wa viwanda na kulifikisha
Taifa katika uchumi wa kati. Kiutamaduni msukumo wetu ni kulinda na
kudumisha mila na tamaduni zetu”.
Waziri
Mkuu amesema mambo hayo wao wana wajibu wa kuyapa kipaumbele ili jamii
iweze kuhabarishwa vizuri. Vyombo vingine vya nje haviwezi kuyaandika na
kuyatangaza mambo hayo vizuri na kwa msukumo wa Kitaifa kama wao.
Nawasihi chukueni nafasi yenu katika kuzibeba agenda zetu za Kitaifa.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, MACHI 18, 2019.
Post A Comment: