Wadau wakiwa katika mkutano wa kutatua migogoro kati ya wawekezaji na Chama cha Ushirika wa wakulima wa Kahawa Wilayani Hai, Mkoani Kilimanjaro |
Na Josephine Majura na Peter Haule, WFM, Kilimanjaro
Serikali imeitaka Kampuni ya Tudeley Estates
Limited kutoka Uingereza iliyoingia mkataba na vyama vya Ushirika
Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro vinavyojishughulisha na uwekezaji wa Kilimo cha
Kahawa (Murososangi), kurudi nchini ili kufanikisha utatuzi wa mgogoro uliosababishwa
na kuibuka kwa mwekezaji mpya ambae mkataba wake haujulikani.
Hayo yamebainishwa na
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angela Kairuki walipofanya mkutano na
Wawekezaji, Vyama vya Ushirika na Wadau wengine kuhusu mgogoro na Mwekezaji
huyo Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.
Dkt. Mpango alisema kuwa, Vyama
vya Ushirika vya Murososangi, viliingia mkataba na Kampuni ya Tudeley Estates
Limited ya nchini Uingereza ambapo washirika hao wenye mashamba eneo la Kibo na
Kikafu wilayani Hai, yenye ukubwa wa
hekari 2054 walimpa Mwekezaji huyo ili kuendeleza zao la kahawa kuanzia mwaka
1998.
Alisema kuwa baada ya mwekezaji huyo, Bw. Conrad Legg, kuonesha nia ya
kutoendelea na uwekezaji huo aliondoka nchini, wakaja wawekezaji wengine kutoka
Ujerumani ambao waliingia mkataba na Kampuni ya Tudeley Estates Limited, kwa kununua
hisa bila kuvishirikisha Vyama vya
Ushirika vilivyoingia mkataba wa awali jambo lililosababisha sintofahamu kwa wana
ushirika hao.
“Aliyeingia mkataba na
Murososange, arudi nchini ili kutatua mgogoro huo ili kuona Wananchi wanawezaje
kuingia mkataba mwingine na mwekezaji mpya ambao utalinda maslahi ya wananchi
wenye mashamba hayo na pia mwekezaji”, alisema Dkt. Mpango.
Alisema Wanaushirika hao
wanataka Mwekezaji wa kwanza arudi nchini ili wavunje mkataba wa awali kwa kuwa
mkataba huo haujaisha muda wake hivyo hawawezi kuingia mkataba na mwekezaji
mpya wakati ule wa awali bado unaendelea.
Aidha, alisema kuwa mwekezaji
mpya kutoka Ujerumanim Bw. Marcus Shiber, alianza kuleta fedha katika eneo la uwekezaji na kulipa baadhi ya kodi za mtangulizi wake,
madeni, mishahara na kuboresha miundombinu ya mashamba hayo bila kupata muafaka
na Vyama vya Ushirika jambo ambalo liliendelea kuleta mgogoro.
Dkt. Mpango alisema kuwa,
wamepata maelezo kutoka pande zote na baadhi ya maelezo hayo yanahitaji ushauri
wa kisheria hivyo tumeiomba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuyafanyia kazi mambo
hayo ili kuweza kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, namna
bora ya kumaliza mgogoro huo bila kuingizia Serikali hasara.
Aliwatahadharisha watendaji
wakuu wa serikali kutotumia ubabe na vitisho kwa wawekezaji ili kutoharibu
taswira ya taifa katika masuala ya uwekezaji unaopigiwa chapuo hivi sasa na
Serikali ya Awamu ya Tano, ili kuvutia mitaji, mapato ya serikali, ajira kwa
vijana na kuvutia teknolojia za kisasa kwa maendeleo ya Taifa.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu, Angela Kairuki, alisema kuwa kutokana na mgogoro huo wa
kiuwekezaji akaunti za Mwekezaji mpya kutoka Ujerumani ikiwemo ya Kampuni ya
Kuza Afrika inayojishughulisha na kilimo cha parachichi Mkoani Mbeya ilifungwa
na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kuhusiana na masualaya kodi, jambo
lililosababisha baadhi ya shughuli za Mwekezaji huyo kukwama.
Alisema kuwa kikosi chao
kupitia Waziri wa Fedha na Mipango aliyetumwa na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli
kutatua mgogoro huo, wameangalia iwapo taratibu za kufungwa akaunti hizo zilifuatwa
na kutafuta njia bora ya kutatua tatizo hilo na pia kuona ni Mwekezaji yupi
anafaa kuingia mkataba na Vyama vya Ushirika vya Murososangi, nia ikiwa ni kuona
Vyama hivyo vinanufaika na Uwekezaji unakua nchini.
Kwa Upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Kilimanjaro Bi. Anna Mgwira, aliishukuru Serikali kwa hatua yake ya
kutuma Mawaziri ili kutatua mgogoro huo wa muda mrefu ambao utatuzi wake
utasaidia Wananchi kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Mkurugenzi Mkuu wa Kituo
cha Uwekezaji nchini-TIC, Bw. Geofrey Mwambe, alisema kuwa katika mkutano kati
ya Mawaziri, Wawekezaji na Vyama vya Ushirika wamebaini kuwa utaratibu
walioukuta Wawekezaji kutoka Ujerumani haukuwa sawa na ule ambao waliwekeana na
Mwekezaji wa kwanza kutoka Uingereza, hivyo kuleta ugumu kiutendaji kwa
Mwekezaji wa pili.
Alisema kuwa, Serikali
inahitaji uwekezaji katika Sekta ya Kilimo ili
kupata malighafi ya viwanda nchini, kuongeza mnyororo wa thamani na
kukuza pato la Taifa, hivyo inafanya jitihadi za kuvutia wawekezaji watakaoleta
mitaji na teknolojia ya kisasa ili Taifa liweze kukabiliana na ushindani wa
bidhaa katika soko la Kimataifa.
Mwakilishi wa mwekezaji
mpya kutoka Ujerumani Bw. Robert Clowes, alimshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, kwa kuwatuma Mawaziri wake kuja kutatatua mgogoro huo, alisema
Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji hivyo yupo tayari kuendelea kuwekeza
zaidi nchini kwa lengo la kupata manufaa kwa pande zote ikiwa ni pamoja na
Kampuni yake na vyama vya ushirika wa kilimo cha Kahawa Wilayani Hai Mkoani
Kilimanjaro.
Post A Comment: