Naibu Waziri Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima (kushoto) akipata maelezo
ya kitaalamu juu ya hali ya mazingira katika eneo la mradi wa ujenzi wa bwawa
la kufua umeme la Rufiji Hydro Power Project kutoka kwa Dkt. Samuel Gwamaka Mkurugenzi
Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). Naibu
Waziri amefanya ziara ya kikazi kutembelea eneo hilo mwishoni mwa wiki.
Na
Lulu Mussa
Morogoro
Serikali imesema itahakikisha kuwa vyanzo vya maji
vinavyopeleka maji Mto Rufiji havivamiwi kwa shughuli za kilimo na kibinadamu
ili Mradi Mkubwa wa kufua umeme katika bonde la Mto Rufiji uweze kutekelezeka.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima mara baada ya kukamilisha
ziara yake katika Mikoa sita hapa nchini kwa lengo la kukagua maeneo yenye
changamoto za kimazingira pamoja na kutafuta ufumbuzi kwenye ikolojia ya vyanzo
vya maji vinavyo changia maji katika bonde la Rufiji.
Akiwa katika eneo
la mradi litakapojengwa bwawa la kufua umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji Naibu
Waziri Sima amesema amefanya ziara ya kukagua vyanzo vya maji vya Bonde la
Rufiji ambavyo vinahusisha matawi matatu ya mito ambayo ni Mto Ruaha Mkuu,
Kilombero, Luegu, na kutoa wito kwa wananchi kutoharibu vyanzo hivyo ili kuwa
na maji ya kutosha kutekeleza mradi huo mkubwa.
“Ziara yangu
imeanzia Lindi, Ruvuma, Njombe, Mbeya, Iringa na Kilombero kote huko nimelenga
kujione vyanzo hivi vikuu. Mito hii ya Ruaha Mkuu, Kilombero na Luegu inapoungana
ndio inatengeneza Mto Rufiji ambako ndiko kuna maporomoko ya “Stiglers Gorge”.
Na nimeridhishwa na hatua za watendaji katika ngazi zote za Serikali kwa kuwa
mstari wa mbele kukahikisha kuwa vyanzo vya maji vinalindwa na kuhifadhiwa.”
Sima alisisitiza.
Katika ziara yake Naibu Waziri Sima
ameweza kutoa miongozo muhimu yenye kukuza, kulinda na kusimamia mazingira kwa
namna endelevu husunan Ikolojia ya Vyanzo vya maji katika Mikoa aliyopita.
Naibu Waziri Sima amesema Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa kufua
umeme wa Maji wa Rufiji Hydro Power Project ambapo zaidi ya MW 2100 za umeme
zitazalishwa, hivyo kulingana na ukubwa wa mradi huu ni wazi uhifadhi wa
Mazingira katika vyanzo hivyo ni muhimu ukatiliwa mkazo.
“Uhifadhi
wa Mazingira katika Bonde la Rufiji ni wafaida kwa pande zote hasa ustawi wa
wananchi. Wananchi ndio walinzi na wahifadhi wa kwanza katika kutunza
Mazingira, aidha Sheria ya Mazingira, 2004 kifungu cha 6 kimetamka wajibu wa
kila mwananchi kutunza Mazingira kwamba; Mtu yeyote anayeishi Tanzania atakuwa mdau
na atawajibika kutunza na kuendeleza Mazingira na kutoa taarifa kwa mamlaka
husika kuhusu shughuli au jambo lolote ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza
kuathiri mazingira. Hivyo kupitia sheria hii si jukumu la Serikali pekee
kusimamia uhifadhi wa Mazingira, wananchi nao wana wajibu wa moja kwa moja
wa kutunza Mazingira”. Sima alisisitiza.
Kwa upande mwingine
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Nchini Dkt.
Samuel Gwamaka alieambatana na Naibu Waziri Sima katika ziara hiyo amesema kuwa
Baraza limedhamiria kufungua Ofisi katika eneo hilo la mradi ili kurahisisha
utekelezaji wa majukumu ya kila siku za Baraza.
Bonde la Rufiji lina
ukubwa wa KM2 177,420 ambazo ni sawa na asilimia 20 ya Tanzania na linapita katika
mikoa 11 ya Tanzania na Wilaya 32 za Tanzania, Bonde hili ni Mashuhuri kwa
Kilimo, ufungaji, uvuvi na uzalishaji wa umeme katika vituo vya Mtera na
Kihansi.
Post A Comment: