Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda (aliyeshika tofali) akitoa maelezo kwa Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo wakati wa ziara fupi ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya hiyo ulioanza mapema mwaka huu na kutakiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi wa sita mwaka 2019.
 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (rainboot za kijani) akiangalia uimara wa matofali yaliyojengewa msingi katika moja ya majengo saba ya hospitali ya wilauya ya Sumbawanga inayojengwa katika bonde la ziwa Rukwa, kata ya Mtowisa. (mwenye shati ya kitenge) Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza wakuu wa Wilaya za Mkoani Rukwa kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa pamoja katika kutembeleana na kuelezana changamoto na mafanikio katika maeneo ya mradi wa ujenzi wa hospitali za wilaya ili kujenga hospitali hizo katika hadhi sawa na hatimae kupeana ujuzi wa utekelezaji wa mradi huo.
Amepongeza ushirikiano unaoonyeshwa na uongozi wa wilaya ya Nkasi unaoongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo mh. Said Mtanda pamoja na wabunge, madiwani na mkurugenzi na kusifu mafunzo waliyoyapata na kuyarekebisha wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa vituo vitatu vya afya katika wilaya hiyo na kuonyesha dalili za kutojirudia kwa makosa waliyoyafanya wakati wakitekeleza ujenzi wa vituo hivyo.
“Wakuu wa Wilaya waweke program ya kutembeleana kwa pamoja ili kujifunza, wanakuja kwa mfano (wilaya ya) Nkasi, wanakwenda wilaya ya Sumbawanga, Wanakwenda wilaya ya Kalambo halafu watakaa chini wafanye tafakari ili waone ni namna gani wanweza wakasimamia vizuri hizo hospitali zetu za wilaya kwasababu tunapaswa tuwe na kitu bora, hospitali zote tatu ziwe bora ndani ya mkoa wetu,” Alisisitiza.
Alisema kuwa halitakuwa jambo jema kwa wilaya moja kuwa na ufanisi sana ilihali wilaya nyingine inakuwa na changamoto na hivyo vyema wakaungana kama timu na kutembelea miradi hiyo ya ujenzi wa hospitali za wilaya ili kila mmoja aweze kujifunza kutoka kwa mwenzie.
Ameyasema hayo baada ya ziara yake ya kutembelea ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nkasi pamoja na ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga ili kujionea changamoto mbalimbali zinazoukabili mradi huo ambao unatakiwa kuisha mwishoni mwa mwezi wa sita mwaka huu.
IMETOLEWA NA 
OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA
Share To:

Post A Comment: