*Ni baada ya ushindi wa mechi dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda
*Asema wameleta heshima na sifa kwa nchi, wanastahili zawadi

Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii

KWA ushindi huu, wote tunawapa viwanja! Hivyo ndivyo Rais Dk.John Magufuli ambavyo amewaambia wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars ' kutokana na ushindi wa 3-0 ambao wameupata dhidi ya Timu ya Taifa ya Uganda 'The Cranes' .

Kw ushindi wa Taifa Stars , Tanzania itashiriki kwenye michuano ya AFCON mwaka 2019 yanayofanyika nchini Misri na kutokana na kazi nzuri ambayo wachezaji wameifanya Rais Magufuli amesema kuna kila sababu ya kutambua kazi iliyofanywa na wachezaji na ni bora na hivyo ametoa ndogo ya zawadi kwa wachezaji wote.

Rais Magufuli ametoa zawadi hiyo leo Machi 25, 2019,  Ikulu jijini Dar es Salaam wakati anazungumza na wachezaji wa Taifa Stars, Bondia Hassan Mwakinyo (aliyempiga bondia wa Agetina), Kamati ya Uhamasishaji , viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu wa Tanzania(TFF) pamoja na wadau wa soka walioalikwa kwenye mazungumzo hayo.

Amefafanua kilichofanywa na Taifa Stars pamoja na bondia Mwakinyo na mwalimu wake ameona kwa niaba ya Watanzania ameamua kutoa zawadi hiyo ya viwanja kwa wachezaji wote. "Sina chochote kikubwa cha kuwapa, ila nimeguswa na nimeona nitoe zawadi ndogo.Tutawapa viwanja vya kujenga nyumba. Wachezaji wote wa Taifa Stars ,Hassan Mwakyonyo,mwalimu wake, Peter Tinno pamoja na Leordiga Tenga wote wapate viwanja.Viwanja hivi vitakuwa Dodoma ambako ndiko Makuu makuu ya nchi.

"Kila mmoja apate kiwanja chake, kama Serikali ilitoa viwanja kwa mabalozi wa nchi nyingine, hatuoni sababu ya mabaloz wa Taifa letu (Taifa Stars na Hassan)kwanini wasipatiwe viwanja. Haiwezekanani baada ya kustaafu wanabaki hawana kitu , lazima tutambue kazi ambayo wameifanya kwa niana ya nchi yetu ,"amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema anatambua mchezaji wa kimataifa na Nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta ameondoka nchini jana kurudi kwenye timu yake lakini naye asisahaulike kwenye zawadi ya kiwanja huku akitumia nafasi  kutoa maagizo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kusimamia upatikanaji wa viwanja hivyo.

Kuhusu mchezo wa jana amesema amefurahishwa na uchezaji wa Taifa Stars kwani wamejituma sana uwanjani na ukweli ni kwamba walikuwa wanapiga pasi nzuri na kwamba licha ya kuwa yeye si Mwalimu Kashasha lakini ameona pasi zinavyopigwa.

"Pasi jana zilikuwa nzuri na mimi sio Mwalimu Kashasha lakini pasi zilikuwa nzuri,nilianza kuogopa baada ya kuona wanarudisha rudosha nyuma.Wametangaza jina la Tanzania na wameipa heshima nchi.Hata waliolewa ndio raha yenyewe,wapo waliotoka tupumzike yote hiyo ni kwasababu tu ya kuonesha furaha.

"Kwa niaba ya Watanzania wote wapenda michezo na kwa niaba ya Watanzania wapenda maendeleo nawapongezeni.Kuna timu nyingi sana zimefanya kazi za kuhamasisha watu viwako vyombo vya habari, madereva teksi na makundi mengine mbalimbali yote yameonesha umoja na mshikamano,"amesema.

Ameongeza "Uzelendo wetu ndio utatuvusha,mshikamano ambao tumeuonesha jana basi tuuoneshe kwenye sekta nyingine.Umoja wetu ndio njia pekee ambayo itatufanya tufanikiwe.Jana imekuwa siku yetu kama Taifa. Siku nyingine pia ziwe siku zetu".

Wakati huo huo Rais Magufuli amesema furaha aliyonayo kwa ushindi wa Taifa Stars moyo wake umeridhika na sasa ametangaza kutoa Sh.bilioni moja kwa ajili ya maandalizi ya timu ya Taifa ya Vijana ya Serengeti Boys chini ya miaka 17."Sikuwa na fedha kwa ajili ya kusaidia maandalizi, nimepigiwa simu na Waziri Mkuu, Makamu wa Rais lakini sikuwa nimesema chochote lakini kwa furaha tuliyonayo nitatoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya maandalizi ya timu yetu,"amesema Rais Magufuli.

Pia amesema kuwa Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan amemkabidhi  timu ya Taifa ya Wanawake Taifa Queens'  ili nayo kuhakikisha inafanya vizuri katika mashindano mbalimbali. "Makamu wa Rais nakukabidhi hii timu ya Taifa ya Wanawake,wasaidie katika mahitaji yao mbalimbali.Sijaifuatilia na kujua iko nafasi gani lakini naambiwa nayo inafanya vizuri."

Ametumia nafasi hiyo kufafanua Watanzania wanapenda michezo na timu zao zinapofanya vibaya wanaumia sana.Hivyo kuna kila sababu ya wadau wa michezo kuhakikisha michezo inakuwa juu kwani haiwezekani kila mara timu za Tanzania zinashindwa kufanya vema kwenye michuano mbalimbali ya kimataifa.
Share To:

Post A Comment: