Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) na Mwakilishi Mkazi wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bw Michael Dunford wakiwasha soketi ya mtambo wa kusafisha nafaka ikiwa ni ishara ya uzinduzi katika hafla iliyofanyika makao makuu ya NFRA, Jijini Dodoma leo tarehe 14 Machi 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe Patrobas Katambi wakikagua mtambo wa kusafisha nafaka katika hafla iliyofanyika makao makuu ya NFRA, Jijini Dodoma leo tarehe 14 Machi 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akihutubia katika hafla ya kukabidhi mtambo wa kusafisha nafaka kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kutoka kwa Mpango wa Chakula Duniani (WFP), makao makuu ya NFRA, Jijini Dodoma leo tarehe 14 Machi 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) na Mwakilishi Mkazi wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bw Michael Dunford wakizindua mtambo wa kusafisha nafaka katika hafla iliyofanyika makao makuu ya NFRA, Jijini Dodoma leo tarehe 14 Machi 2019.
Sehemu ya washiriki wakifatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akizungumza katika hafla ya kukabidhi mtambo wa kusafisha nafaka kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kutoka kwa Mpango wa Chakula Duniani (WFP), makao makuu ya NFRA, Jijini Dodoma leo tarehe 14 Machi 2019.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umetakiwa kuhakikisha kuwa katika msimu huu wa mwaka 2019/2020 unanunua mahindi kwa zaidi ya Tani 500,000 kwa wakulima ili kutimiza azma ya serikali ya kuimarisha masoko ya wakulima.

NFRA pia imetakiwa Kubadili mfumo wa ununuzi wa mahindi ili kupunguza gharama kubwa zinazojitokeza wakati wa msimu wa ununuzi.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 14 Machi 2019 katika hafla ya kukabidhi mtambo wa kusafisha nafaka kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kutoka kwa Mpango wa Chakula Duniani (WFP), makao makuu ya NFRA, Jijini Dodoma.

Hasunga alisema kuwa NFRA imekuwa ikinunua nafaka kidogo kwa wakulima kwa ajili ya kuhifadhi pekee badala yake wametakiwa kufanya biashara ya kununua na kuuza nafaka kwa wingi.

Alisema WFP imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo nchini kwa muda mrefu na kwa upande wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, ushirikiano huo umedumu tangu mwaka 2012. WFP na NFRA wamekuwa wakishirikiana kikamilifu katika kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mpango Mkakati wa WFP wa miaka mitano (Country Strategy Plan 2017-2021) unaendana na mipango ya Serikali inayolenga kufikia Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs), hususani lengo la kutokomeza njaa (Zero Hunger) ifikapo mwaka 2030.

Aliongeza kuwa, mkakati wa WFP wa kuwasaidia wakulima wadogo kupitia mpango wa Farm To Market Alliance (FTMA) unashabihiana na Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini (ASDP II), kwa kuwa mikakati yote imelenga katika kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuongeza thamani ya mazao na kufikia masoko.


Mhe Hasunga alisema kuwa kutokana na mkakati huo, Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, inathamini na kuipongeza WFP katika kuimarisha usalama wa chakula na lishe hapa nchini.

Aidha, alisema serikali inaishukuru WFP kwa kuichagua Tanzania kuwa moja wapo ya Kituo cha Usimamizi wa Bidhaa za Kimataifa (Global Commodity Managed Facility) ambacho kinasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa masoko ya mazao ya chakula kwa wakulima nchini.

Vivevile, Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) alimuhakikishia Mwakilishi Mkazi wa WFP Michael Dunford kuwa WFP haikukosea kuichagua Tanzania kuwa Kituo cha Usimamizi wa Bidhaa za Kimataifa (GCMF) kuwa, ukiacha faida za kijiografia, Tanzania inajivunia kuwa na kiwango kizuri cha utoshelevu wa chakula. Mfano, katika mwaka huu, nchi ina kiwango cha utoshelevu wa chakula kwa 124%, hivyo, nchi ina ziada ya chakula, hii inadhibitisha na kuwahakikishia kuwa Tanzania ina uwezo wa kuuza kwa WFP tani zaidi ya 200,000 wanazohitaji za chakula ambapo ni hitaji lao la kila mwaka.

MWISHO.
Share To:

Post A Comment: