Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatarajia kufanya zoezi la uandikishaji wa Wapiga Kura
kwa majaribio katika Kata mbili za Kibuta iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya
ya Kisarawe, Mkoani Pwani na Kihonda katika Halmashauri ya Manispaa ya
Morogoro, Mkoani Morogoro.
Taarifa
iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume Jaji (Rufaa) Semistocles Kaijage Jijini Dar
es Salaam leo (Jumanne Tarehe 26. 03. 2019) imesema Uandikishaji huo wa
Majaribio utakaoanza Machi 29, hadi Aprili 04, 2019 utafanyika katika vituo 20
vya kuandikisha Wapiga Kura ikiwa ni vituo 10 katika kila Kata.
Taarifa
hiyo imeeleza kuwa uandikishaji huo unalenga katika kuvifanyia majaribio vifaa
na mfumo wa Uandikishaji Wapiga Kura ili kubaini changamoto kabla ya kuanza rasmi
kwa zoezi hilo.
Imezitaja
sifa za watu watakaoandikishwa katika uandikishaji huo kuwa ni raia wa Tanzania
aliyetimiza umri wa miaka 18 au atakayetimiza umri wa miaka 18 siku ya
Uchaguzi Mkuu ujao.
Aidha
uandikishaji huo hautawahusu raia walio chini ya kiapo cha utii wa nchi
nyingine, aliyebainika kuwa hana akili timamu au yuko kizuizini kama mhalifu
mwenye ugonjwa wa akili au yuko kizuizini kwa ridhaa ya Rais.
Taarifa
hiyo imeendelea kutaja watu ambao hawatahusika katika majaribio hayo ya uboreshaji
kuwa ni mtu aliyehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama au anatumikia kifungo
kinachozidi miezi sita pamoja na mtu aliyepoteza sifa za kuandikishwa kuwa
Mpiga Kura chini ya Sheria za Uchaguzi au Sheria nyingine yoyote inayohusu makosa
ya uchaguzi.
Tume ya
Taifa ya Uchaguzi pia inawajulisha wakazi wa Kata hizo zinazofanya Uandikishaji
wa Majaribio na ambao walijiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
mwaka 2015 kuwa wanaweza kutumia fursa hiyo kuhakiki taarifa zao katika vituo
walivyojiandikishia.
Wakati
huo huo Tume inatoa fursa kwa Vyama vya Siasa kuweka Wakala mmoja katika kila kituo cha Kuandikishia Wapiga
Kura kwa lengo la kushuhudia na kujiridhisha juu ya taratibu zitakazotumika
pamoja na changamoto zitakazojitokeza ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kabla ya
zoezi rasmi la Uandikishaji.
Tume
imevitaka Vyama vyenye nia ya kuweka Mawakala katika uandikishaji huu wa
Majaribio kuwasilisha orodha ya majina ya Mawakala na vituo walivyopangiwa kwa
Maafisa Waandikishaji wa Halmashauri za Kisarawe na Manispaa ya Morogoro.
Kadhalika
Vyama vimetakiwa kuwasilisha nakala mbili za barua za utambulisho zikiwa na
picha mbili na nakala mojawapo kati ya Kitambulisho cha Taifa au Kadi ya Mpiga
Kura, Pasi ya Kusafiria au Leseni ya Udereva na kwamba kila Chama kitagharamia
Wakala wake.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo wakati wa uandikishaji huo wa majaribio Tume ya Taifa ya
Uchaguzi itatumia runinga, redio, mitandao ya kijamii na magari ya matangazo
kwa ajili ya kutoa Elimu ya Mpiga Kura ili kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa
wingi na kushiriki katika zoezi hilo.
Mwenyekiti
wa Tume Mheshimiwa Kaijage kupitia taarifa hiyo amewaomba wakazi wa Kata za
Kibuta na Kihonda kujitokeza kwa wingi katika Uandikishaji huo wa majaribio na
kutoa ushirikiano kwa Tume wakati wote wa utekelezaji wa jukumu hilo muhimu kwa
mustakabali wa demokrasia ya Taifa.
Tume ya
Taifa ya Uchaguzi hufanya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa
mujibu wa Ibara ya 74 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoipa
Tume mamlaka ya kusimamia na kuratibu uandikishaji wa Wapiga Kura katika
Uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Madiwani kwa
Tanzania Bara.
Tume
kwa mujibu wa Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na
Kifungu cha 21(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292
inapaswa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya Uchaguzi
Mkuu mmoja na unaofuata.
MWISHO
Post A Comment: