Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uwindaji ya Otterlo Business Corporation{OBC} iliyopo Loliondo wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha Isack Mollel{59} amepandishwa kizimbani kujibu mashitaka kumi ikiwemo uhujumu uchumi,utakatishaji fedha haramu,kugushi na kutoa maelezo ya uongo ya kukwepa kodi ya mabilioni ya pesa.

Akisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Serikali,Osward Tibabyekomya akisaidiwa na Materius Marandu na Dismas Mwigunyiza mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha ilidaiwa kuwa mtuhumiwa alitenda makosa hayo kati ya mwaka 2011 hadi 2018 kinyume cha sheria ya makosa ya jinai vifungu namba 333,335 na 337 vya kanuni ya adhabu na kufanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Tibabyekomya alidai kuwa shitaka la kwanza linalomkabili Mollel ni kosa la kugushi nyaraka kwani kati ya septemba 15 mwaka 2017 na aprill 7 mwaka jana ndani ya Jiji la Arusha Mollel aligushi ivoince namba 9091 ya septemba 15 mwaka 2017 ikieleza kuwa kampuni ya OBC ilinunuwa gari la kifahari lenye namba za Chassis WDB62433615367735 kutoka kampuni ya magari ya Evarest Motors{FZD} ya Dubai kwa gharama ya dola za kimarekani 12,800 .

Shitaka la pili ni kugushi nyaraka tarehe hiyo hiyo mwaka 2017 na mwaka jana aligushi invoice namba 9092 ikionyesha kuwa OBC ilinunuwa gari aina ya Man Truck yenye chassis namba WMA 5500231W007547 kutoka kampuni ya magari ya Evarest Motors ya Dubai kwa thamani ya dola za kimarekani 12,000.

Tibabyekomya alisoma shitaka la tatu linamkabili Mollel kama Mkurugenzi Mtendaji wa OBC ni pamoja na kutoa taarifa za uongo march 7 mwaka jana kuwa akiwa Holili Mkoani Kilimanjaro mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Kenya mtuhumiwa anatuhumiwa kutoa taarifa za uongo kwa Mamlaka ya Mapato Nchini{TRA} idara ya ushuru wa forodha yenye lengo la kukwepa kulipa kodi ya serikali.

Ilidaiwa kuwa Kampuni ya OBC ilikwepa kulipa kodi sahihi na kuamuwa kuidanganya serikali na kuingizia hasara ya mamilioni ya fedha kwa kuingiza nchini magari matatu ya kifahari Man Truck chassis WMA5500231W007547,Mercedes Benz chassis namba UWDB62433615367735 na Mercedes Benz Chassis namba UWDB62430415145210 kutoka kampuni ya magari ya Dubai.

Shitaka la nne linalomkabili Mollel pamoja na kampuni ya OBC akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni ilidaiwa kuwa julai 2011 na julai 2015 kwa pamoja katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro waliingiza nchini magari 31 ya utalii na uwindaji na kukwepa kulipa kodi ya serikali zaidi ya shilingi bilioni 2.2.

Mwendesha mashitaka alisoma shitaka la tano linalomkabili Mollel ni kutoa taarifa za uongo kwa TRA mei 25 mwaka 2013 na februali 4 mwaka 2015 na kuisababishia hasara serikali ya zaidi ya shilingi milioni 299 na kuingiza nchini magari sita bila ya kulipa ushuru wa serikali kutoka kampuni ya magari ya Evarest Motor iliyopo nchini Dubai,

Tibabyekomya alidai kuwa shitaka la sita ni Mollel kutuhumiwa kutoa taarifa za uongo na kukwepa kulipa kodi ya serikali zaidi ya shilingi milioni 111 na kuingiza nchini magari mawili ya kifahari Land Cruisser Pick Up chassis namba JTELB71J707112476 na Ford Ranger Chassis MNCLS329558W735840 yaliyonunuliwa kutoka kampuni hiyo ya Dubai.

Alisoma shitaka la saba ni Februali 18 mwaka 2017 Jijini Dar es salaam Mollel anatuhumiwa kukwepa kulipa kodi ya serikali ya zaidi ya shilingi milioni 199 kwa kuingiza magari mawili ya kifahari ya Nissan Patroll chassis namba JN8FY1NY3EX002626 na Mercedes Benz chassis namba WDCYR48F78X173956.

Mwendesha mashitaka wa serikali alisoma shitaka la nane la utakatishaji fedha haramu ilidaiwa kuwa aprill 3 mwaka jana Holili Mkoani Kilimanjaro Mollel alificha umiliki na mali kwa kutumia jina la kampuni ya OBC kwani aliandikisha jina la gari aina ya Man Truck chassis WMA5500231W007547 yenye namba za usajili T141DNM iliyosajiliwa kwa jina la kampuni wakati gari hilo ni mali yake.

Tibabyemkomya alisoma shitaka la tisa la utakatishaji fedha haramu kwani inadaiw akuwa Mollel na OBC waliidanganya serikali kwa kuingiza magari na kubadilisha umiliki kutoka kampuni hadi umiliki wake wakati akijuwa wazi kufanya hivyo ni kosa kisheria na kuisababishia serikali hasara.

Shitaka la kumi ni uhujumu uchumi kwani ilielezwa mahakamani hapo kuwa januari 2010 hadi 2018 Mkoani Arusha na Kilimanjaro ,Mollel na kampuni ya OBC waliingizia hasara serikali ya zaidi ya shilingi bilioni 2.8 kwa kutoa maelezo ya uongo TRA juu ya uingizwaji wa magari 31 hapa nchini.

Hakimu Mwakatobe alimweleza mtuhumiwa kuwa hakutakiwa kujibu chochote juu ya mashitaka hayo kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na kesi hiyo ilihairishwa hadi marc 18 mwaka huu.

Mollel anatetewa na mawakili watatu maarufu Jijini Arusha wakiongozwa na Method Kimomogolo akisaidiwa na Daud Haraka na Godluck Peter.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: