Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akitoa ufafanuzi kuhusu malipo ya wakulima wa Korosho wakati akizungumza katika ukumbi wa mikutano kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Leo tarehe 16 Machi 2019. (Picha zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Sehemu ya wakulima wa korosho Mkoani Lindi wakifatilia ufafanuzi wa malipo kutoka kwa Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akizungumza katika ukumbi wa mikutano kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Leo tarehe 16 Machi 2019.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe Godfrey Zambi akitoa maelezo ya awali kuhusu sekta ya kilimo, mifugo na maji mbele ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Leo tarehe 16 Machi 2019.
Wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakikagua mtambo wa kutengeneza kimininika cha Nitrojeni inayohifadhi Mbegu wakati wakiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Lindi, Leo tarehe 16 Machi 2019.
Wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakikagua chanzo cha Maji na mfumo wa kutibu maji katika kijiji cha Ng'apa wakati wakiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Lindi, Leo tarehe 16 Machi 2019.
Wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakikagua kiwanda cha kubangua Korosho katika eneo la Mnazimmoja wakati wakiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Lindi, Leo tarehe 16 Machi 2019.
Na Mathias Canal, Wizara ya
Kilimo-Lindi
Serikali imewahakikishia
wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuwa kufikia
tarehe 31 Machi 2019 wakulima wote watakuwa wamelipwa fedha zao kwani uhakiki
umekamilika kwa kiasi kikubwa.
Hakikisho hilo mbele ya
kamati hiyo limetolewa leo Tarehe 16 Machi 2019 na Waziri wa Kilimo Mhe
Japhet Hasunga (Mb) katika ukumbi wa mikutano kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
wa Lindi wakati akitoa ufafanuzi katika mkutano uliowakutanisha wajumbe wa
kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wake Dkt Christine Ishengoma, Mkuu wa
Mkoa wa Lindi, Naibu Katibu Mkuu wizara ya Kilimo, wataalamu serikalini
sambamba na wakulima.
"Kumekuwa na urasimu mkubwa
tangu kuanza kwa zoezi hili la uhakiki lakini sasa tumeamua kama serikali kabla
ya mwisho wa mwezi huu wa tatu wakulima wote wawe wamelipwa malipo yao ili
kuondoa adha wanazokumbana nazo" alikaririwa Mhe Hasunga
Alisema pamoja na kwamba
malipo ni mchakato unaohitaji kupitia katika hatua nyingi za mchakato ikiwemo
uhakiki lakini kila jambo lenye mwanzo ni lazima kuwa na ukomo.
Alisema mpaka sasa Tani
222,684 zimekwisha kusanywa huku hadi kufikia tarehe 14 Machi 2019 tayari jumla
ya Shilingi Bilioni 596.9 zimekwishalipwa kwa wakulima kati ya Shilingi
Bilioni 723
Katika hatua nyingine
Waziri Hasunga amewahakikishia wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo,
Mifugo na Maji kuwa pamoja na mchakato huo wa malipo ya Korosho kuendelea
lakini pia Wizara imepitia katika michakato mbalimbali ya kumpata Mkurugenzi
mpya wa Bodi ya Korosho ili kuendelea na majukumu ya Bodi hiyo.
Kuhusu wanaofanya biashara
ya zao hilo kinyume na sheria maarufu kama Kangomba Waziri Hasunga alisema kuwa
tayari serikali imewabaini na wote watachukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumzia Pembejeo feki
Mhe Hasunga alisema kuwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa kwa wafanyabiashara
wote waliofanya hujuma kwa kuwauzia wakulima Mbegu na mbolea feki ambapo hatua
kali zimeanza kuchukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kutolipwa fedha
wanazodai kwa kusambaza Pembejeo hizo.
Katika hatua nyingine
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameuagiza uongozi wa Taasisi ya
Utafiti wa viuatilifu Vya Tropiki (TPRI) kutuma wataalamu Mkoani Lindi ili kuchukua
sampuli za viuatilifu kwa wakulima na kuvipima ili kubaini kadhia ya usambazaji
wa viuatilifu feki kwa wakulima.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Kamati ya kudumu ya Bunge Dkt Christine Ishengoma (Mb) amemuagiza Waziri wa
Kilimo kuhakikisha kuwa taarifa ya malipo ya wakulima wote wa Korosho inafika
bungeni tarehe 2 Aprili 2019.
MWISHO
Post A Comment: