Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara

Kumekuwa na dhana ya kila mkulima wa korosho kulalamika kuwa hajalipwa fedha za korosho zake jambo hili limeibua sintofahamu katika jamii.

Katika hali hiyo serikali sasa imeamua kuja na mkakati kabambe wa kubandika majina ya wakulima wote waliolipwa fedha zao ili kuondokana na kadhia ya lawama za wakulima wasioitakia mema serikali.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametoa agizo hilo leo tarehe 18 Machi 2019 wakati akizungumza mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge, Mifugo na Maji kwenye kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.

Agizo hilo limetolewa kwa wataalamu wanaoongoza timu ya Oparesheni Korosho kubandika majina ya wakulima wote waliolipwa ili kuondoa sintofahamu katika jamii.

“ Mimi nashangaa sana kila mkulima akiulizwa anasema hajalipwa jambo hili sio sawa nadhani wanafanya hivi kukwepa madeni wanayodaiana huko vijiji, sasa naitaka timu ya wataalamu wa Oparesheni korosho kuhakikisha majina yote ya wakulima waliolipwa yanabandiikwa kwenye ofisi za vijiji ” Alikaririwa Mhe Hasunga

Alisema kuwa wanapaswa kubandika orodha ya majina ya watu waliolipwa na kiasi cha korosho walicholipwa.

“Mpaka sasa Tani 222,684 zimekwisha kusanywa huku hadi kufikia tarehe 14 Machi 2019 tayari jumla ya Shilingi Bilioni 596.9 zilikuwa zimekwishalipwa kwa wakulima kati ya Shilingi Bilioni 723 lakini nashangaa wakulima wanasema hawajalipwa hili sio sawa” Alisema Mhe Hasunga



Sambamba na hayo Waziri Hasunga alisema kuwa Serikali imejipanga hadi kufikia tarehe 31 Machi 2019 wakulima wote watakuwa wamelipwa fedha zao kwani uhakiki umekamilika kwa kiasi kikubwa.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli inapaswa kuungwa mkono kwa maamuzi magumu kwenye korosho kwa kuamua kuwalipa wakulima shilingi 3300 kwa kila kilo moja ya korosho.

Kadhalika, ameshangazwa na Mkoa wa Mtwara ambao unazalisha kwa karibu nusu ya korosho zote nchini lakini imebaini idadi ndogo ya wafanyabiashara wanaofanya biashara ya Korosho kinyume na sheria maarufu kama kangomba ukilinganisha na mkoa wa Lindi ambao una idadi kubwa ya Kangomba.

“ Nashangaa sana Mkoa wa Mtwara una Kangomba 10 lakini ndio wazalishaji wakubwa wa korosho huku Mkoa wa Lindi ambao unafuatia kwa uzalishaji wa korosho ukiwa na idadi kubwa ya Kangomba ambao wapo zaidi ya 400” Alisema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe Dkt Christine Ishengoma amempongeza Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga kwa kuanzisha zoezi la usajili wa wakulima nchini.

“ Nakupongeza sana Waziri Hasunga kwa hili lakini hakikisha unalisimamia kwa weledi jambo hili ili liwe na matokeo chanya na wakulima waweze kutambulika kote nchini kwani kufanya hivyo serikali itakuwa na uwezo wa kuwahudumia kwa ufasaha” Alisema

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakiongozwa na Mhe Dkt Christine Ishengoma wameanza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Mtwara wakikagua miradi ya maendeleo katika sekta husika za Kilimo, Mifugo na Maji.

MWISHO


Share To:

Post A Comment: