Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma imezuia kufanyika kwa uchaguzi katika jimbo la Arumeru Mashariki hadi kesi ya maombi madogo ya kufungua kesi ya msingi ya kuomba kutengua uamuzi wa Spika wa kumfutia ubunge Joshua Nassari itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Akizungumza leo jijini hapo, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Dayness Lyimo amesema kesi hiyo namba 22 ya mwaka 2019 inasikilizwa na Jaji Latifa Mansoor.
Amesema pia wajibu maombi ambao ni Spika na mwanasheria mkuu wa Serikali wamepewa siku saba kupeleka kiapo kinzani cha maombi hayo.
“Jaji pia ameagiza kusifanyike uchaguzi wowote (jimboni) hadi hapo maombi hayo yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi,” amesema.
Nassari ambaye alikuwapo mahakamani hapo asubuhi anawakilishwa na mawakili watu ambao ni Hekima Mwasipe, Jonathan Mndeme na Fred Kalonga.
Upande wa walalamikiwa unawakilishwa na wakili wa Serikali Masunga Kawahanda.
Kesi hiyo itakwenda tena mahakamani Machi 27 kwa ajili ya kusikilizwa.
Mei 14 Spika wa Bunge, Job Ndugai alimwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage kumtaarifu jimbo la Nassari liko wazi kutokana mbunge huyo kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge.
Post A Comment: