Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango (Mb) (kushoto) akizungumza jambo na
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James,
katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma kabla ya kuwasilishwa Mapendekezo
ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa , Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya
Serikali kwa mwaka 2019/20.
Waziri wa nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angela Kairuki, akizungumza jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango Bw. Doto James, baada ya kuwasilishwa kwa Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango na
Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza jambo na Mbunge wa Ludewa Mhe. Deo Ngalawa, kabla ya kuwasilishwa kwa Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20, ambapo mikopo ya Ndani inatarajiwa kuwa Sh. bilioni 4,960.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, akizungumza jambo na Mbunge wa Ilala, Mhe. Mussa Azzan Zungu, kabla ya uwasilishaji wa Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa, Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20, ambapo Sh. bilioni 2,783.7 za mikopo nafuu zinatarajiwa kutoka kwa washirika wa maendeleo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kushoto) na Kamishna
wa Bajeti, Bi. Mary Maganga (kulia) wakizungumza jambo katika viwanja vya Bunge
Jijini Dodoma, kabla ya kuwasilishwa kwa
Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa , Kiwango na Ukomo wa
Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20, ambapo Sh. bilioni 20,856.8 zinatarajiwa
kutumika katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na maandalizi ya uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2020.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango (Mb) (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.
Joyce Ndalichako , katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.
Doto James, katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma .
MAELEZO
YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB)
AKIWASILISHA MAPENDEKEZO YA
SERIKALI
YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA
NA YA
KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA
SERIKALI
KWA MWAKA 2019/20
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, awali
ya yote napenda kuchukua fursa hii
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha
wabunge wote kukutana tena hapa Jijini Dodoma, kupokea mapendekezo ya Serikali
ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali
kwa mwaka 2019/20, kwa mujibu wa Kanuni ya 97 fasili ya (1) na (2) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge Toleo la Januari 2016. Aidha, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kuendelea kuijalia nchi yetu umoja na amani.
2.
Mheshimiwa
Mwenyekiti,
naomba kutumia fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki (Mb),
Mheshimiwa Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb), Mheshimiwa Prof. Palamagamba
Aidan Kabudi (Mb), Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb), Mheshimiwa Joseph
George Kakunda (Mb) na Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) kwa kuteuliwa
na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mawaziri ili kuongoza
wizara mbalimbali. Ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa Mawaziri mlioteuliwa na Waheshimiwa
Wabunge wote mtaendelea kunipatia ushirikiano katika kuijenga nchi yetu kwa
manufaa ya Watanzania wote.
3.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, taarifa hii
inawasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya
kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2019/20 ambayo imegawanyika
katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni tathmini ya mwenendo wa hali ya
uchumi. Sehemu ya pili ni Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa
mwaka 2018/19 na Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa
mwaka 2019/20. Sehemu ya tatu ni tathmini ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2018/19
na mapendekezo ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20.
SEHEMU
YA KWANZA
TATHMINI
YA MWENENDO WA HALI UCHUMI
4.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, kutokana na
juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli katika kuiandaa nchi kuelekea uchumi wa kipato cha kati, uchumi
umeendelea kuimarika. Pato la Taifa kwa
kutumia mwaka wa kizio 2015 linaonesha kuwa katika robo ya tatu (Julai hadi
Septemba) ya mwaka 2018, Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.8
ikilinganishwa na asilimia 5.0 kipindi kama hicho mwaka 2017. Shughuli za
kiuchumi zilizokuwa kwa kasi kubwa ya ukuaji ni afya (asilimia 13.2), usafirishaji
na uhifadhi mizigo (asilimia 12.4); Maji (asilimia 10.7); Ujenzi (asilimia
7.4); Habari na Mawasiliano (asilimia 7.3); viwanda (asilimia 7.3); na Biashara
na Matengenezo (asilimia 7.3).
5.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika mwaka 2018,
mwenendo wa mfumuko wa bei nchini uliendelea kuwa tulivu katika wigo wa
tarakimu moja kutokana na kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini na
nchi jirani pamoja na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti za
Serikali. Mfumuko wa bei ulipungua kutoka wastani wa asilimia 4.0 Januari 2018,
hadi kufikia asilimia 3.4 Juni 2018 na kuendelea kupungua zaidi hadi asilimia
3.0 Januari 2019.
6.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika kipindi
cha mwaka unaoishia Januari 2019 thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nchi za
nje ilikuwa dola za Marekani milioni 8,300.0 na thamani ya bidhaa na huduma
zilizonunuliwa kutoka nje ilikuwa dola za Marekani milioni 10,462.6. Kwa upande
wa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nchi za
nje ilikuwa dola za Marekani milioni 2,982.2 kutokana na kuongezeka kwa thamani
ya bidhaa za mitaji zilizoagizwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya miradi mikubwa
ya maendeleo. Kwa matokeo hayo akiba ya fedha za kigeni ni Dola za Marekani
milioni 4,884.4 Januari 2019, kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma
kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha takribani miezi 4.8. Kiwango hiki ni zaidi
ya lengo la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la miezi 4.5.
7.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Ujazi
wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka kwa wastani wa asilimia 6.6
katika mwaka 2018 ikilinganishwa na ongezeko la wastani wa asilimia 5.5 katika
kipindi cha mwaka 2017. Mwenendo huo ulichangiwa na kuimarika kwa ukuaji wa
mikopo kwa sekta binafsi kulikotokana na jitihada za Serikali kupitia Benki Kuu
katika kuchochea ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi. Riba za dhamana za muda mfupi za Serikali
zilipungua hadi wastani wa asilimia 6.4 ikilinganishwa na wastani wa asilimia
11.1 mwaka 2017. Vile vile, riba za mikopo ya benki za biashara kwa sekta
binafsi zimeendelea kupungua kutoka wastani wa asilimia 17.8 mwaka 2017 hadi
wastani wa asilimia 17.4 mwaka 2018.
8.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mikopo kwa sekta binafsi iliendelea kuimarika kufuatia
utekelezaji wa sera ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi pamoja na jitihada
zilizochukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu katika kuchochea ongezeko la
mikopo kwa sekta binafsi. Kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi imeendelea
kuongezeka ambapo Januari 2019 ilikuwa asilimia 7.3 ikilinganishwa na asilimia
2.1 Januari 2018. Sehemu kubwa ya mikopo kwa sekta binafsi imeendelea
kuelekezwa katika shughuli binafsi (asilimia 27.9 ya mikopo yote) ikifuatiwa na
shughuli za biashara zilizopata asilimia 18.4, uzalishaji viwandani (asilimia
11.6) na kilimo (asilimia 7.8).
9.
Mheshimiwa
Mwenyekiti, mwenendo wa
thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani umeendelea kuwa tulivu ambapo
katika mwaka 2018, Dola moja ya Marekani ilinunuliwa kwa wastani wa Shilingi
2,263.8. Hii ni kutokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha, usimamizi thabiti
wa mapato na matumizi ya Serikali, matumizi ya gesi asilia na umeme wa maji badala
ya mafuta katika kuzalisha umeme na baadhi ya viwanda nchini kuzalisha bidhaa
ambazo awali zilikua zikiagizwa kwa wingi kutoka nje.
10. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano, itaendelea kutekeleza sera
madhubuti za fedha na bajeti ili kuhakikisha uchumi wa nchi yetu unaendelea
kuimarika.
SEHEMU
YA PILI
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2018/19 NA MAPENDEKEZO YA
MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2019/20
A.
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2018/19
11. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/19, Serikali ilitenga Shilingi bilioni
12,007.3 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, zikijumuisha Shilingi bilioni
9,876.4 fedha za ndani na Shilingi bilioni 2,130.9 fedha za nje. Hadi Januari
2019, jumla ya Shilingi bilioni 2,788.5 zilitolewa kwa ajili ya kugharamia
miradi ya maendeleo. Aidha, Shilingi bilioni 144 zilipokelewa kutoka kwa Washirika
wa Maendeleo na kupelekwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo
inayotekelezwa kwenye Wizara, Taasisi na Wakala za Serikali, Sekretaieti za
Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Vile vile, Shilingi bilioni 3,803.4
zimetumika kulipa mikopo iliyotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Serikali imeshatenga na inatarajia kutoa kiasi cha Shilingi bilioni 1,433.8 kwa
ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, ukiwemo mradi wa kufua
umeme kwa kutumia nguvu ya maji Mto Rufiji (MW 2,115).
12. Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa baadhi ya
miradi ya maendeleo katika mwaka 2018/19 ni kama ifuatavyo:
(i)
Ujenzi wa Reli ya Kati kwa
kiwango cha Standard Gauge: Ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) unaendelea vizuri kama
ilivyopangwa, ambapo shughuli zinazoendelea ni ujenzi wa madaraja, makalavati,
daraja lenye urefu wa km 2.54 katikati ya jiji la Dar es Salaam, ukataji wa
miinuko, ujazaji wa mabonde na utandikaji wa reli. Katika kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422), kazi
zinazoendelea ni pamoja na ukataji wa miinuko na ujazaji wa mabonde, usanifu wa
njia na ujenzi wa kambi za Kilosa na Ihumwa. Kwa upande wa kipande cha Isaka – Rusumo (km 371), hatua
iliyofikiwa ni kukamilika kwa mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali
wa njia ya reli. Aidha, taratibu za ununuzi wa mabehewa, injini na mitambo
itakayotumika kutoa huduma ya usafiri kwenye reli ya Standard Gauge zipo katika hatua za mwisho.
Katika miradi inayogharamiwa na mfuko wa reli, shughuli
zilizofanyika ni: kununua vichwa 11 vya treni kwa ajili reli ya kati; kuendelea
na ukarabati wa reli ya Tanga - Arusha (km 439) ambapo kipande cha Tanga –
Mombo (km 129) kimeanza kufanya kazi ya kusafirisha mizigo na ukarabati wa vipande
vya Mombo – Same (km124) na Same – Arusha (km 186) unaendelea. Aidha, kazi ya
ukarabati wa mabehewa inaendelea ambapo hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa
ukarabati wa mabehewa 15.
(ii)
Mradi wa Kufua Umeme wa Maji Rufiji - MW 2,115: Hatua iliyofikiwa ni: kupatikana kwa mkandarasi wa mradi
wa kufua umeme utokanao na nguvu ya maji katika Mto Rufiji ambaye ni Kampuni ya
Ubia kati ya Arab Contractors na Elsewedy Electric S.A.E kutoka Misri
ambapo mkataba wa ujenzi umesainiwa na mkandarasi alikabidhiwa eneo la mradi
mwezi Februari 2019. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ukamilishaji wa
ujenzi wa miundombinu wezeshi ikijumuisha njia ya umeme wa msongo wa kV 33
kutoka Msamvu hadi eneo la mradi; mifumo ya huduma ya maji na ya mawasiliano ya
simu; kukamilika kwa ujenzi wa nyumba 10 na kuendelea na ukarabati wa nyumba 28
za iliyokuwa kambi ya RUBADA; ujenzi wa barabara za Kibiti - Mloka – Mtemere –
Matambwe Junction – Mto Rufiji (km
210) na Ubena Zomozi – Mvuha – Kisaki – Mtemere Junction (km 178.39) zimekamilika.
(iii) Kuboresha
Shirika la Ndege Tanzania: Hatua iliyofikiwa ni: kuwasili
kwa ndege nyingine tatu, moja ikiwa ni aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na mbili
zikiwa ni Airbus A220-300, na hivyo kufanya idadi ya ndege zilizonunuliwa kuwa
sita; kulipa sehemu ya gharama za ununuzi wa ndege moja aina ya Boeing 787-8
Dreamliner na Bombadier Q400 zinazotarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwaka
2019. Kufuatia hatua hiyo, ATCL itaanzisha safari za ndege kwenda nchini China
na India ambazo kimkakati ndizo masoko mapya ya utalii.
(iv)
Miradi ya Umeme: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa njia ya kusafirisha
umeme yenye urefu wa km 250 ya msongo wa kV 220 Makambako – Songea pamoja na vituo vitatu vya kupoza umeme vya
Makambako, Madaba na Songea, hivyo kuwezesha mikoa ya Njombe na Ruvuma
kuunganishwa katika Gridi ya Taifa; kuendelea na mradi wa kusafirisha umeme wa
msongo wa kV 400 wa Singida – Arusha – Namanga wenye urefu wa km 414; kuendelea
na miradi ya kusafirisha umeme ya Geita – Nyakanazi (kV 220), Rusumo –
Nyakanazi (kV 220) na Bulyankulu – Geita (kV 220); kuendelea na utekelezaji wa
mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini na
Makao Makuu ya Wilaya ambapo vijiji 1,782 na wateja 96,832 wameunganishiwa
umeme hivyo kufikia jumla ya vijiji 1,039 vilivyounganishwa na umeme;
kukamilisha utengenezaji wa mitambo minne ya kufua umeme na kupelekwa mitambo
miwili ya kufua umeme katika eneo la mradi wa Kinyerezi I Extension – MW 185; Mradi wa Kufua Umeme wa Rusumo MW 80: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika
kwa ujenzi wa barabara za kuingia eneo la mradi; kukamilika kwa ujenzi wa
kikinga maji; kuanza kazi ya kuchimba handaki la kupitisha maji; kuendelea na
uchimbaji wa eneo itakapofungwa mitambo; na kukamilika kwa ujenzi wa nyumba mbili
kati ya tano za wafanyakazi.
(v)
Huduma za Maji Mijini na Vijijini: miradi 65
imekamilika na kufanya jumla ya miradi yote iliyokamilika kufikia 1,659 na vituo vya kuchotea maji
kuongezeka hadi 131,370 na kuhudumia wananchi 25,359,290. Upatikanaji wa huduma
za maji Jijini Dar es Salaam umefikia asilimia 85, katika mikoa mingine
asilimia 80, miji midogo asilimia 64 na vijijini asilimia 64.8. Aidha, utekelezaji
wa miradi ya maji katika maeneo mengine unaendelea katika hatua mbalimbali
ikiwa ni pamoja na mradi wa maji wa Ziwa Victoria – Igunga - Nzega na Tabora, mradi
wa maji katika jiji la Arusha na Same – Mwanga - Korogwe. Vile vile,
utekelezaji wa mradi wa maji katika miji 28 wenye thamani ya Dola za Kimarekani
Milioni 465 upo katika hatua za kumpata Mtaalamu Mwelekezi na Mkandarasi wa
mradi.
(vi)
Miradi ya Afya: Serikali imeendelea kuimarisha
huduma za afya kwa kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea
huduma za afya kwa asilimia 96. Hatua nyingine zilizofikiwa ni pamoja na: kukamilika
kwa ujenzi wa jengo la vifaa vya uchunguzi (X–Ray Building) na kununua vifaa vya tiba ya mionzi katika
Hospitali ya Rufaa ya Mbeya; na kuongeza utoaji wa chanjo kufikia asilimia 97.
Aidha, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya afya katika ngazi zote ikijumuisha
ujenzi na ukarabati wa hospitali za rufaa za mikoa, kanda na kitaifa; ujenzi wa
hospitali za halmashauri 67; ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya 352; kuajiriwa
kwa watumishi wa sekta ya afya 7,680; ujenzi wa nyumba 310 za watumishi wa
afya; ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwa Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali
za halmashauri, Vituo vya Afya na Zahanati. Serikali imeendelea kuimarisha
huduma za matibabu ya kibingwa kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma,
ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na hivyo kupunguza rufaa za wagonjwa nje ya
nchi katika hospitali za Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI),
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Taasisi ya Mifupa (MOI), hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya
Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi – Mloganzila.
(vii)
Miradi ya Elimu: Serikali imeendelea
kugharamia elimumsingi bila ada ambapo kila mwezi kiasi cha shilingi bilioni
24.4 kinatumika. Hatua nyingine zilizofikiwa ni: ujenzi na ukarabati wa
miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ikijumuisha madarasa 870, matundu ya
vyoo 1,958, mabweni 210, mabwalo 79; ukarabati wa shule kongwe; ujenzi na ukarabati
wa miundombinu katika vyuo vya ualimu Ndala, Shinyanga, Patandi, Mpuguso na
Murutunguru; kukamilisha maboma ya madarasa, mabweni na nyumba za walimu 39; ukarabati
wa vyuo vya kati 20 kati ya 54 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs), nyumba za
walimu 39; kukamilika na kuzinduliwa kwa Maktaba ya Kimataifa yenye uwezo wa
kuhudumia wanafunzi 2,600 kwa wakati mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
ujenzi wa mabweni katika Chuo Kikuu cha Mzumbe yenye uwezo wa kuchukua
wanafunzi 1,000; ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika vyuo vikuu vya
Sokoine na Dar es Saaalm; na mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu 119,214;
uimarishaji wa vyuo 10 vipya vya VETA na kukuza ujuzi kwa vijana; na ujenzi wa
shule kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika chuo cha Ualimu
Patandi.
(viii) Kilimo: Utoshelevu wa Chakula kwa mwaka 2018/19
umefikia asilimia 124. Aidha, Serikali imeanza utekelezaji wa Programu ya
Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II) na mkazo umewekwa katika
kuendeleza mazao ya kimkakati yakiwemo Kahawa, Pamba, Chai, Korosho, Tumbaku,
Alizeti, Michikichi, Mpunga na Mahindi. Ili kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo,
Serikali inaendelea kuimarisha shughuli za ushirika, ujenzi wa maghala na
vihenge vya kisasa vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 250,000 katika kanda saba,
kuongeza uzalishaji wa mbegu za mafuta hususan alizeti na michikichi,
kuimarisha shughuli za utafiti wa mazao, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo
kwa kufufua vinu vya kusindika mazao ya nafaka na mafuta, kudhibiti visumbufu
vya mazao, kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo na kuimarisha
mifumo ya masoko ya mazao. Vile vile, Serikali imeanza kuboresha mifumo ya
takwimu za kilimo kwa kuanza usajili wa Wakulima.
(ix)
Mifugo: Hatua iliyofikiwa ni kuendelea
kuimarisha vituo 3 vya kuzalisha vifaranga vya samaki vya Kingolwira
(Morogoro), Mwampuli (Igunga) na Ruhila (Songea) kwa kuzalisha na kusambaza
vifaranga vya samaki kwa wafugaji wa samaki
wakiwemo vijana. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na sekta Binafsi imeweza
kuzalisha jumla ya vifaranga 17,301,076 kama ifuatavyo: kambamiti 11,080,000,
sato 5,072,800 na kambale 1,148,276. Vile vile, jumla ya wananchi 6,995
wamepatiwa elimu ya ugani katika ukuzaji wa viumbe maji.
(x)
Mradi wa
Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania): Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa tathmini ya athari
za mazingira na jamii kwa upande wa Tanzania; kukamilika kwa tafiti za
kijiolojia katika eneo la Chongoleani; kukamilika kwa tathmini za Kijiolojia na
Kijiofizikia katika eneo la mkuza wa bomba; na kutwaa ardhi eneo la Bandari –
Tanga (Chongoleani) kutakapojengwa miundombinu ya kuhifadhi mafuta.
(xi)
Miradi ya Viwanda: Kiwanda cha
Kuunganisha Matrekta (TAMCO, Kibaha): Hatua iliyofikiwa ni: kuingiza
matrekta 822 aina ya URSUS (semi knocked down) ambapo matrekta 571
yameunganishwa na matrekta 339 yameuzwa; Kituo
cha Zana za Kilimo na Ufundi Vijijini – CAMARTEC: kutengeneza zana
zikijumuisha mashine 64 za kupandia mbegu za pamba, kusaga karanga, kukausha
mbogamboga na kukata majani pamoja na
ujenzi wa mitambo 55 ya biogas;
SIDO: kuendelea na ujenzi wa majengo
ya viwanda 11 katika Mikoa ya Dodoma, Geita, Kagera, Katavi, Manyara, Mtwara na
Simiyu na ujenzi wa ofisi za SIDO katika mikoa mipya ya Geita na Katavi.
(xii)
Miundombinu ya Biashara ya Madini: Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu
ya kuboresha mazingira ya biashara kwenye sekta ya madini ikihusisha: vituo vya
umahiri katika mikoa saba, vituo vitatu vya mfano, jengo la taaluma la madini
katika chuo cha madini, One Stop centre
Mirerani, Brokers house Mirerani,
uanzishwaji wa masoko ya madini mikoani, na uwekaji wa mfumo wa ulinzi wa
kidigitali Mirerani, ununuzi wa mtambo wa uchorongaji miamba kwa ajili ya
kusaidia wachimbaji wadogo kupitia STAMICO.
(xiii)
Ardhi na Makazi: Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na: kuandaliwa na
kusajiliwa kwa Hati Milki 110,000 na Hati za Kimila 133,000; kuandaliwa kwa
mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 263 katika Wilaya 45; kuandaliwa kwa
Mipango Kabambe ya miji mikuu ya mikoa ya Arusha,
Mwanza, Mtwara, Mara, Singida, Iringa na Pwani, Ruvuma, Tabora na Simiyu;
kuendelea na hatua za maandalizi ya Mipango Kabambe ya miji mikuu ya mikoa ya
Dar es Salaam, Morogoro, Rukwa, Shinyanga, Manyara, Dodoma, Tanga, Mbeya,
Kagera, Kigoma, Katavi, Lindi, Kilimanjaro, Njombe na Geita; kuanzishwa kwa Mfumo
Unganishi wa Taarifa za Ardhi; na kuongezeka kwa idadi ya benki na taasisi za
fedha zinazotoa mikopo ya nyumba kufikia 31 na kuwanufaisha wananchi 4,174.
Aidha, Mfuko wa Mikopo Midogo Midogo ya Nyumba ulio chini ya Benki Kuu
umeongezewa mtaji wa dola za Marekani milioni 18 ambapo taasisi za fedha tano
(5) zimepatiwa mtaji wa shilingi bilioni 13.87 kwa ajili ya kukopesha wananchi
wa kipato cha chini kwa masharti nafuu.
(xiv)
Ujenzi wa Barabara Dar es Salaam: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa ujenzi wa barabara
ya juu katika makutano ya TAZARA (Mfugale flyover); kuendelea na ujenzi wa
barabara za muingiliano Ubungo; mradi wa kuendeleza Jiji la Dar es Salaam km 210
za barabara kwa kiwango cha lami; na kuendelea na ujenzi wa barabara ya
Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (km 19) kwa njia nane.
(xv)
Ujenzi wa Meli: Hatua iliyofikiwa ni: kuendelea na Ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa
kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika ziwa Victoria; kufikia
asilimia 82 ya ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na
mizigo tani 200 za mizigo katika ziwa Nyasa; na kukamilika kwa ujenzi wa
matishari mawili katika Ziwa Nyasa. Kwa upande wa Ziwa Tanganyika,
Ujenzi wa Meli Mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo,
ambapo uandaaji wa mikataba kwa ajili ya ujenzi wa meli hiyo pamoja na
ukarabati wa meli ya MV Liemba umekamilika. Miradi mingine ni kukamilika kwa
ujenzi wa kivuko kipya cha Kigongo – Busisi; kukamilika kwa ukarabati wa kivuko
cha MV Pangani II; kuendelea kukarabati vivuko vya MV Sengerema, MV Kigamboni
na MV Misungwi.
(xvi)
Viwanja vya Ndege: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa asilimia 90.7 ya
ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal III) katika kiwanja cha ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere; kuendelea na upanuzi wa maegesho ya ndege, ujenzi
wa jengo la mizigo, uzio wa kiwanja, maegesho ya ndege za mizigo na jengo la
kuongozea ndege katika kiwanja cha ndege cha Mwanza. Aidha, ujenzi na ukarabati
wa viwanja vya ndege vya mikoa vikiwemo vya Sumbawanga, Kigoma, Shinyanga, Mtwara,
Songea, Mara, Songwe, Mbeya, Mwanza, Kigoma, Tabora na Iringa unaendelea.
(xvii)
Mawasiliano: Hatua iliyofikiwa ni: kuendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano ambapo vituo vitatu (3) vya Mkongo katika maeneo ya Tukuyu, Kibaha
na Kahama vimejengwa na kuvipa nguvu vituo vitatu (3) vya mkongo (Optical Line
Amplifier (OLA) katika maeneo ya Ifakara, Kidatu na Mafinga; na kuendelea
kutekeleza mradi wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi umetekelezwa kwa
kubandika vibao vya namba za nyumba katika Halmashauri 12. Vile vile, Mfumo wa
Usimamizi na Ufuatiliaji wa Mawasiliano ya Simu (TTMS) umekabidhiwa rasmi
kutoka kwa Mkandarasi SGS/GVG ambapo katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Februari,
2019 jumla ya miamala 2,004,196,139 imepita katika mitandao ya simu na wastani
wa fedha zilizopita ni Shilingi bilioni 12,202.7.
(xviii) Uendelezaji
wa Bandari: Bandari ya Dar es Salaam: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa
ujenzi na kuanza kutumika kwa gati Na.1; na kuendelea na ujenzi wa sakafu ngumu
katika gati la kupakua na kupakia magari; Bandari
ya Tanga: ukarabati wa miundombinu ya barabara kuelekea lango Na. 2
umekamilika; Bandari ya Mtwara:
ujenzi wa gati la mita 300 la kuhudumia shehena mchanganyiko unaendelea. Aidha,
ujenzi wa Bandari katika Maziwa Makuu (Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa)
unaendelea.
(xix)
Ujenzi wa Barabara na Madaraja Makubwa: kazi zilizofanyika ni kujengwa kilomita 140.42 za barabara kuu na kilomita 12.43 za barabara za
mikoa kwa kiwango cha lami. Aidha, kwa upande wa madaraja hatua iliyofikiwa ni
kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Mlalakuwa (Dar es Salaam); kuendelea na
ujenzi wa madaraja ya Momba (Rukwa) ambapo utekelezaji umefikia asilimia 94,
Sibiti (Singida) asilimia 88.35, Mara (Mara) asilimia 85; na Ruhuhu (Ruvuma) asilimia
76; na kuanza ujenzi wa Daraja Jipya la Selander na barabara unganishi zenye
urefu wa kilomita 5.2.
(xx) Ufungaji wa rada nne za kuongozea ndege za kiraia JNIA, KIA,
Mwanza na Songwe: Hatua iliyofikiwa ni: JNIA: Kukamilika kwa asilimia 95 ya
miundombinu ya rada. Mwanza: Ujenzi wa miundombinu ya rada unaendelea vizuri. KIA: Ujenzi
wa miundombinu ya rada unaendelea na
umefikia asilimia 90. Songwe: taratibu za ujenzi wa miundombinu
zinaendelea. Aidha, mitambo itafungwa miundombinu itakapokamilika.
(xxi) Miradi
ya Mahakama: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa ujenzi wa
Mahakama za Wilaya za Bukombe, Chato, Ruangwa, Geita na Kilwa; kukamilika kwa
ujenzi wa Mahakama za Mwanzo za Magoma (Korogwe) na Mlowo (Mbozi); kuendelea na
ujenzi wa Mahakama za mikoa ya Njombe, Katavi, Lindi na Simiyu; kuendelea na
ujenzi wa Mahakama za Wilaya za Kasulu, Sikonge, Kilindi, Bunda, Longido,
Kondoa, Njombe, Rungwe, Chunya, Wanging’ombe, na Makete; kuendelea na ujenzi wa
Mahakama Kuu Kigoma na Mara ambao umefikia asilimia 80; ujenzi wa Mahakama za
Mwanzo za Mkunya (Newala), Uyole (Mbeya), Ngerengere, Mlimba na Mang’ula
(Morogoro); ukarabati mkubwa wa nyumba tatu za kufikia Majaji Mtwara; na
kukamilika kwa uboreshaji wa mfumo wa ukusanyaji takwimu na kusajili mashauri,
kuingiza taarifa muhimu za wadaawa ikiwa ni pamoja na kutuma taarifa kwa ujumbe
mfupi (sms) kwa wadaawa kuhusu mwenendo wa mashauri. Aidha, imeanzishwa huduma
ya mahakama zinazotembea (mobile court, kwa kuanzia na mikoa ya Dar es salaam
na Mwanza, magari ambayo yamezinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwezi Februari 2019.
(xxii)
Miradi ya Kimkakati ya kuongeza mapato katika
Halmashauri: Hatua iliyofikiwa ni utekelezaji wa miradi ya kimkakati 37 ya
kuongeza mapato ya halmashauri na kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka Mfuko
Mkuu wa Serikali ikijumuisha Soko la kisasa – manispaa ya Morogoro, soko la
kisasa – halmashauri ya mji Kibaha, Pwani, ghala la kisasa – halmshauri ya
wilaya ya Ruangwa, kituo cha mabasi Mbezi Louis – Halmashauri ya jiji la Dar es
Salaam, soko la Mburahati – manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, ujenzi na
upanuzi wa kiwanda cha kutengeneza chaki na kiwanda cha vifungashio –
halmashauri ya wilaya ya Maswa, Simiyu, stendi ya mabasi Korogwe. Miradi hii
inatekelezwa katika halmashauri 29 na ipo katika hatua mbalimbali.
(xxiii) Uwekezaji: Sekta ya Uwekezaji imeendelea kukua ikilinganishwa na
nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani
zinaonesha Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji kati ya nchi za Afrika
Mashariki. Kwa mfano, Ripoti ya Uwekezaji ya Dunia ya mwaka 2018 inayotolewa na
Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) inaonesha kuwa
Tanzania imevutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 1,180,
ikifuatiwa na Uganda Dola za Kimarekani milioni 700 na Kenya Dola za Kimarekani
milioni 672. Aidha, ripoti ya “Where to Invest in Africa” ya mwaka 2018
inayojulikana kama RMB’s Investment
Attractiveness Index inayoonesha nchi zinazovutia zaidi kwa uwekezaji
barani Afrika, Tanzania imeendelea kuwa katika kumi bora kwa kushika nafasi ya saba
(7) kati ya nchi 52 ikipanda kutoka nafasi ya 9 mwaka 2017.
Aidha, jitihada za Serikali kuhamasisha ujenzi wa viwanda
nchini zimewezesha kuongezeka mitaji katika viwanda mwaka hadi mwaka. Kwa
mfano, mtaji uliowekezwa chini ya Mamlaka ya EPZ umeongezeka kutoka Dola za Marekani
bilioni 1.422 mwaka 2016 hadi Dola za Marekani bilioni 2.23 hapo Novemba, 2018,
ikiwa ni ongezeko la Dola za Marekani milioni 808 (sawa na ongezeko la asilimia
56.8). Mwenendo wa mauzo ya bidhaa za viwanda hivyo nje ya nchi yamekuwa
yakiongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.194 hapo
Novemba 2018, kutoka Dola za Marekani bilioni 1.1 mwaka 2016, ikiwa ni ongezeko
la asilimia 99.45. Mtaji mkubwa umewekezwa katika viwanda vya kuongeza thamani
mazao (agro processing) ambapo ina asilimia 38 ya mtaji wote; zikifuatiwa na
viwanda vya kuunganisha mitambo (assembling & engineering) asilimia 31 ya
mtaji, mavazi na nguo asilimia 21 ya mtaji na uchakataji madini asilimia 10 ya
mtaji. Aidha, viwanda 71 ni vya makampuni ya kigeni, viwanda 58 ni vya
makampuni ya ubia na viwanda 45 ni vya makampuni ya ndani.
(xxiv)
Kuhamishia Utekelezaji wa Majukumu ya Serikali Makao Makuu
Dodoma: Serikali imetekeleza
azma yake ya kuhamia Makao Makuu ya Nchi, Dodoma ambapo mpaka hivi sasa Wizara
zote zimeshahamia Dodoma na jumla ya Watumishi 8,883 wanatekeleza majukumu yao
wakiwa hapa Dodoma (Watumishi hao ni kutoka Ofisi/Wizara na Vyombo vya Ulinzi
na Usalama). Vile vile, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na
Naibu Mawaziri pia wameshamia Dodoma. Uendelezaji wa eneo la Mji wa Serikali –
Ihumwa umeanza na jumla ya majengo 22 ya Ofisi za Wizara na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali yako katika hatua za mwisho za ujenzi.
(xxv)
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana: Serikali imeendelea kuwawezesha Vijana kiuchumi ili
waweze kujiajiri katika nyanja za uzalishaji mali na kutoa huduma ambapo hatua
iliyofikiwa ni: kutolewa kwa mikopo nafuu yenye thamani ya Shilingi bilioni
2.74 kwa vikundi vya vijana 523, vyenye wanachama 3,661 katika Halmashauri 128
za Tanzania Bara; na kuanzishwa kwa SACCOS 127 za Vijana kati ya 184
zinazotarajiwa kuanzishwa hadi kufikia mwaka 2020.
(xxvi)
Mafanikio
mengine ni kuendelea kuimarika kwa
Amani, utulivu na usalama nchini hivyo, kuwezesha kukua kwa shughuli za
kiuchumi na kijamii. Katika kutimiza jukumu hilo, Jeshi la Polisi limeendelea
kuweka juhudi katika kudhibiti uhalifu sanjari na kuendelea kutoa elimu kwa
umma kupitia njia mbalimbali ili jamii ibadilike na kuachana na matukio ya
uhalifu.
(xxvii)
Mazingira:
Serikali imetekeleza hughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha mfumo wa
ikolojia ili kuhimili mabadiliko ya tabia nchi, kujenga uwezo w taasisi na
jamii kuhimili changamoto za mazingira na athari za mabadiliko ya tabia nchi na
kuboresha kanuni za kutoa leseni za tathmini ya mazingira kwa kuanzisha
utaratibu wa kutoa leseni za muda kabla ya kuanza mradi.
(xxviii)
Miradi ya Sekta Binafsi: Sekta hii imeendelea kushiriki katika ujenzi wa viwanda ambapo katika
kipindi cha 2015 hadi 2018, jumla ya viwanda 3,530 vilijengwa na kuanza
uzalishaji.
B.
MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2019/20
13. Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mpango wa Maendeleo wa
Taifa 2019/20 ni wa nne katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka ya kutekeleza
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21, wenye dhima ya
Kujenga Uchumi wa Viwanda ili Kuchochea Mageuzi ya Uchumi na Maendeleo ya Watu.
Maandalizi ya Mpango huu yamezingatia azma ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa
ya Maendeleo 2025; na Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
14. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa
wa Mwaka 2019/20 yanatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ambavyo ni:
(i)
Viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi
wa viwanda: Miradi itakayotekelezwa
katika eneo hili ni ile yenye lengo la kujenga viwanda vinavyotumia malighafi
zinazopatikana nchini hususan kilimo, madini na gesi asilia. Miradi hiyo ni
pamoja na Ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia, Uanzishwaji na
Uendelezaji wa Kanda Maalamu za Kiuchumi na Kongane za
Viwanda, viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo na
uvuvi, kuongeza thamani ya madini na usimamizi endelevu wa rasilimali za
misitu;
(ii)
Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi itakayotekelezwa katika eneo hili ni ile yenye
lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na ujuzi, upatikanaji
wa chakula na lishe bora na huduma za maji safi na salama. Shughuli
zitakazotiliwa mkazo ni pamoja na kugharamia utoaji wa elimu msingi bila ada,
kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi, utekelezaji wa Programu
ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu (Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika
Elimu), ujenzi na ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi nchini, kuboresha huduma
za maji vijijini;
(iii)
Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara
na Uwekezaji: Miradi
itakayotekelezwa katika eneo hili ni ile yenye lengo la kuendeleza ujenzi na
ukarabati wa miundombinu (reli, bandari, nishati, viwanja vya ndege, barabara).
Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Kufua Umeme wa Maji Rufiji MW 2,115;
Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania; Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge; na kuendelea na utekelezaji
wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara na Uwekezaji. Aidha,
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20 umeweka msukumo katika kuboresha
mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza ikiwemo kupitia upya mfumo wa
kitaasisi, kisera na kisheria pamoja na kanuni zake ili kuvutia wawekezaji wa
ndani na nje ya nchi katika kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo; na
(iv)
Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango: Miradi inayotekelezwa katika eneo hili inalenga
kuimarisha mifumo na taasisi za utekelezaji wa Mpango, kuweka mfumo
utakaowezesha upatikanaji wa uhakika wa rasilimali fedha na kuweka vigezo vya
upimaji wa mafanikio ya utekelezaji.
SEHEMU
YA TATU
TATHMINI
YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2018/19 NA MAPENDEKEZO YA KIWANGO NA UKOMO WA
BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2019/20
A.
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2018/19
15. Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018/19, Serikali ilipanga kukusanya na
kutumia jumla ya shilingi bilioni
32,476.0. Kiasi hicho kinajumuisha: mapato ya ndani shilingi bilioni 20,894.6;
misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo shilingi bilioni
2,676.6; na mikopo yenye masharti ya kibiashara kutoka vyanzo vya ndani na nje
shilingi bilioni 8,904.7. Aidha, matumizi ya kawaida yalikadiriwa kuwa shilingi
bilioni 20,468.7 na matumizi ya maendeleo shilingi bilioni 12,007.3.
16. Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019, mapato ya kodi
yalikuwa shilingi bilioni 9,111.9, mapato yasiyo ya kodi shilingi bilioni
1,522.9 na mapato yaliyokusanywa na Halmashauri yalikuwa shilingi bilioni
371.7.
17. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za
kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji kama ilivyoainishwa ndani
ya Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara na Uwekezaji (Blueprint) kwa lengo la kuchochea ukuaji
wa uchumi na kuongeza mapato ya Serikali. Hatua hizo ni pamoja na: Kupunguza
kodi kwa wachimbaji wadogo wa madini; Ugawaji wa vitambulisho kwa
wafanyabiashara wadogo wadogo; Kupunguza kiwango cha ushuru wa bidhaa unaotozwa
kwenye pombe kali zinazotengenezwa nchini kwa kutumia zabibu zinazozalishwa
nchini; Kuweka utaratibu mpya wa ukusanyaji wa kodi ya majengo; Kuboresha
mifumo ya TEHAMA ya kukusanya kodi na maduhuli ikiwemo Electronic Fiscal Device
Management System (EFDMS) ambao hupokea na kutunza kumbukumbu za utoaji wa
risiti za mauzo.
18. Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Januari 2019, Washirika wa Maendeleo walitoa jumla
ya shilingi bilioni 1,034.8. Kati ya kiasi kilichotolewa, misaada na mikopo nafuu
ya Kibajeti ilikuwa shilingi bilioni 125.4 na miradi ya maendeleo shilingi
bilioni 782.0. Mifuko ya Kisekta ilipokea shilingi bilioni 127.4.
19. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019,
Serikali ilikopa shilingi bilioni 2,025.0 kutoka soko la ndani. Aidha, katika
kipindi hicho, Serikali ilifanya majadiliano na taasisi mbalimbali za kifedha
za kimataifa na kupata shilingi bilioni 458.6 kutoka Benki ya Credit Suisse
mwezi Februari 2019 na shilingi bilioni 247.7 zinatarajiwa kupatikana kutoka
benki ya HSBC hivi karibuni. Vile vile, Serikali ipo katika hatua za mwisho za
majadiliano na baadhi ya wakopeshaji walioonesha nia ya kuikopesha Serikali kwa
mwaka 2018/19.
20. Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019, Serikali
ilitoa ridhaa ya matumizi ya jumla ya shilingi bilioni 13,750.6. Kati ya kiasi
hicho, shilingi bilioni 10,962.1 zilitolewa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na
shilingi bilioni 2,788.5 zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Mahitaji yaliyopewa kipaumbele katika utoaji wa fedha ni pamoja na: Ulipaji wa
deni la Serikali ikijumuisha michango ya mwajiri katika Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii shilingi bilioni 5,465.9 ambapo Shilingi bilioni 3,803.4 zimetumika
kulipa mikopo iliyotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo; na mishahara
ya watumishi wa Serikali shilingi bilioni 3,890.0. Serikali imeshatenga na
inatarajia kutoa kiasi cha Shilingi bilioni 1,433.8 kwa ajili ya kugharamia
miradi mbalimbali ya maendeleo, ukiwemo mradi wa kufua umeme kwa kutumia nguvu
ya maji Mto Rufiji (MW 2,115).
21. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za
kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi wa matumizi ili kufikia malengo ya
bajeti ya mwaka 2018/19. Miongoni mwa mikakati hiyo ni: Kuhamasisha ulipaji wa
kodi kwa hiari kupitia vipindi mbalimbali vya elimu kwa umma; Kutekeleza
mwongozo wa ushirikiano baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo; Kuendelea
kusisitiza nidhamu ya matumizi katika utekelezaji wa bajeti kwa kuzingatia
Sheria ya Bajeti Na. 11 ya Mwaka 2015; kulipa
madai yote yaliyohakikiwa ya makandarasi; Kuanza kutumika kwa Mfumo wa
Kielektroniki wa Stampu za kodi (ETS) ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa
kodi; na Kutekeleza Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mapato ya Ndani (IDRAS) ili
kuongeza ufanisi katika usimamizi wa makusanyo ya kodi za ndani.
B.
SERA ZA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2019/20
22. Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera za mapato kwa mwaka 2019/20 zitalenga: Kuboresha
mazingira ya kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji, ukuaji wa biashara
ndogondogo na za kati pamoja na ukuaji wa uchumi endelevu; Kuboresha mazingira
ya ulipaji kodi kwa hiari, upanuzi wa wigo wa kodi na matumizi ya mifumo ya
TEHAMA katika usimamizi wa kodi; Kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili
kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato; Kuwianisha
na kupunguza tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wakala za Serikali na
Mamlaka za Udhibiti; na Kuwajengea uwezo maafisa wa Wizara, Idara
Zinazojitegemea, Wakala na Halmashauri ili kuimarisha uwezo wa ukusanyaji wa
mapato yasiyo ya kodi.
23. Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji wa mazingira haya utawezesha kwa kiasi kikubwa
kuongezeka kwa uwekezaji, uzalishaji, ajira na miamala ya biashara ambayo kwa
ujumla itachangia kuongezeka kwa vyanzo vya mapato. Aidha, kwa upande wa
misaada na mikopo nafuu, Serikali itaendelea kuimarisha mahusiano kupitia
utekelezaji wa Mkakati wa Ushirikiano na Washirika wa Maendeleo.
Post A Comment: