Na Felix Mwagara, MOHA, Morogoro.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amefanya operesheni kubwa ya kukagua na kupima ulevi wa pombe kwa madeveva wa mabasi na malori mjini Morogoro, jana.
Lugola pia alizungumza na abiria wa mabasi hayo, pamoja na viongozi wa madereva waliopo stendi kuu ya mabasi Msamvu, mjini humo, ambapo walimwelezea kero mbalimbali zinazowakabili.
Ukaguzi wa mabasi na malori hayo ulifanyika barabara kuu itokayo Dodoma kuja Morogoro-Dar es Salaam ambapo Waziri huyo akiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa huo (RPC), Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa huo (RTO), alisimamisha vyombo hivyo vya moto vilivyokuwa vinaingia Mizani iliyopo eneo la Kihonda, nje kidogo ya Mji wa Morogoro.
Akizungumza na madereva, kondakta, wapiga debe na abiria mara baada ya kufanya ukaguzi huo, Lugola alisema ni wajibu wake kufanya hivyo katika hatua ya kupunguza kwa kasi ajali mbalimbali zinatokana kwa uzembe wa madereva nchini.
“Mimi ni Waziri wa vitendo, nikiagiza nataka nitekelezwe, na pia nikiahidi lazima nilifuatilie, niliwaambia nitakua nakuja kufanya ukaguzi muda wowote ambao hamuujui, na ninafanya hivi kwa lengo moja tu, kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa ikiwa ni hatua ya kumaliza kupunguza au kumaliza kabisa ajali za barabarani hapa nchini,” alisema Lugola.
Aliongeza kuwa, kwasasa ajali zimepungua nchini, hasa Mkoa wa Morogoro, kwasababu ya askari wa usalama barabarani kufanya kazi zao kiweledi, na pia madereva kufuata sheria za usalama barabarani.
Lugola aliwataka madereva nchini, kuacha uendeshaji wa mashindano, kuwa na leseni na pia kuhakikisha wanapokuwa barabarani wanakua makini kwasababu ya kuwabeba abiria au mizigo mbalimbali wanayoisafirisha sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi.
“Madereva wa mabasi na malori ambao nimefanikiwa kuwapima kilevi leo, ambao wasiopungua sita, sijawakuta na kilevi, wapo makini na hii inaleta nguvu na imani kuwa madereva wanaelewa na kuzingatia sheria za usalama barabarani, na pia ndani ya mabasi niliyokuwa nayakagua nimezungumza na abiria wakaniambia madereva wanaendesha vizuri na pia niliwakuta wamevaa mikanda, naamini safari yetu ya kuondoa ajali za barabarani tunazidi kufanikiwa,” alisema Lugola.
Wakizungumza kwa wakati tofauti katika stendi kuu ya mabasi, madereva walilipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, kwa usimamizi mzuri ambao umewaunganisha na kuwafanya waifurahie kazi wanayoifanya.
Dereva Juma Rashidi wa basi linalosafiri kutoka Ifakara kuja Morogoro, alisema wanajisikia furaha kubwa kwa uongozi mpya wa Jeshi la Polisi ulioletwa Mkoani Morogoro hivi karibuni.
“Naomba niseme ukweli, RPC na RTO hakika wanatuongoza vizuri, hakuna kero za ajabu kama zamani, tupo huru kufanya kazi zetu, hii inaonyesha viongozi hawa wanataka tufanye kazi ili tuweze kupata riziki zetu kwa njia halali bila usumbufu wa kusumbuana kama ulivyokuwa siku za nyuma,” alisema Rashidi.
Lugola alifanya ziara katika kituo hicho, na baadaye kutoka nje ya kituo hicho kuyakagua mabasi na malori, mara baada ya kumaliza ziara yake aliyoifanya Wilayani Kilosa ya kutatua migogoro ya ardhi ya wananchi wa Tarafa ya Kimamba wilayani humo, juzi.
Post A Comment: