Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule akitoa nasaha wakati wa kufungua kikao cha utambulisho wa mradi wa Lishe Endelevu unaofadhiliwa na watu wa Marekani (USAID). |
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule
amepongeza ufadhili wa mfuko wa watu wa Marekani (USAID) kwa kuujumuisha Mkoa wa
Rukwa katika mradi wa Lishe Endelevu, ili kupunguza na kuondoa hali ya udumavu,
Ukondefu, upungufu wa damu kwa watoto na wanawake pamoja na upungufu wa uzito
kwa watoto wachanga katika Mkoa.
Amesema kuwa kwa muda mrefu mkoa wa Rukwa umeendelea
kusikitishwa na takwimu za Utafiti wa Afya na Idadi ya Watu Tanzania (TDHS) chini
ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2015/2016 zinazoonyesha Mkoa wa
Rukwa kuwa na kiwango cha asilimia 56.3 ya udumavu kwa watoto walio chini ya
miaka mitano huku asilimia 5.3 wakiwa na ukondefu na asilimia 23 wakiwa na uzito
mdogo.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha mkoa unajipanga
kukabiliana na hali hiyo hadi sasa Mkoa tayari umefanikiwa kuandaa mpango
mkakati wa lishe wa mkoa wa miaka mitatu ambao umeanza utekelezaji wake mwaka
2018 na kutegemewa kukamilika mwaka 2021, amabapo mpango huo umeainisha
vipaumbele vya mkoa katika kukabuliana na utapiamlo ili kuondokana na udumavu.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa
amesaini Mkataba wa usimamizi na ufuatiliaji
wa shughuli za lishe na wakuu wa wilaya.
Kwa kila robo mwaka taarifa za utekelezaji wa Mkataba huu hujadiliwa
katika Kikao cha mapato na Matumizi cha mkoa. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ndio
mwenyekiti wa kikao hichi na pia agenda ya lishe imekuwa ni ya kudumu katika
vikao vya kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) pamoja na vikao vya kamati za ushauri
za Wilaya (DCC),” Alisema.
Ameyasema hayo katika kikao
cha utambulisho mradi wa Lishe Endelevu unaofadhiliwa kwa msaada wa
watu wa Marekani unaosimamiwa na shirikia lisilo la Kiserikali la Save the
Children kwa kushirikiana na Delloitee, PANITA, Manoff, na AAPH ambapo alimwakilisha
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliyepaswa kuwa mgeni rasmi katika kikao hicho
kilichowajumuisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, wenyeviti wa
halmashauri waganga wakuu wa wilaya na wataalamu kutoka ofisi ya Mkoa na
wawakilishi wa mashirika yanayojihusisha na maendeleo ya afya katika mkoa.
Akielezea namna ya kushirkiana na uongozi wa Mkoa pamoja
na wasimamizi wa mradi Mwenyekiti wa Halmashuri ya Wilaya ya Kalambo Mh. Daudi
Sichone alilisisitiza kutomuangusha mkuu wa wilaya katika kutekeleza malengo ya
mkoa kuhakikisha udumavu unapungua ili watoto waweze kulisaidia taifa katika
miaka ijayo na hivyo kuwaasa wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu.
“Ntawataka wananchi wote katika halmashauri ya wilaya ya
Kalambo na maeneo mengine ambapo mradi huu utapita tuhakikishe tunafuata
taratibu ambazo tutaelekezwa na wataalamu kwamba vyakula hivi ndivyo vinaweza
vikatutoa katika hali tuliyonayo na kwenda katika hali ambayo ni salama
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mradi huo Bi. Joyceline
Kaganda alisema kuwa mradi huo tayari umeshatambulishwa katika mikoa mingine
mitatu ya Dodoma, Iringa na Morogoro na hivyo kuja kumalizia katika Mkoa wa
Rukwa ambapo uzinduzi rasmi wa mradi huo kitaifa utafanyika Mkoani Rukwa.
“Asilimia 56.3 ya watoto chini ya Miaka mitano wamedumaa
hiyo siyo hali nzuri hata kidogo, hicho ndio kizazi ambacho tunategemea
kitakutana na uchumi wa viwanda, Tanzania inataka kufikia Uchumi wa Kati,
tunataka kwenda kwenye uchumi wa Viwanda, sasa kama hawa watoto wamedumaa, nani
atafanya kazi kwenye hivyo viwanda? Tutafika kwenye lengo? Ndio maana mkoa
umechukulia katika hali ya Uzito,” Alisema.
Malengo ya mradi huo ni kupunguza udumavu kwa asilimia 15
huku malengo ya mkakati wa lishe wa Mkoa ni kuhakikisha mkoa unashuka kutoka
asilimia 56.3 hadi kufikia asilimia 40 ya udumavu ifikapo mwaka 2021.
IMETOLEWA NA
OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA
E-mail: ras@rukwa.go.tz
Website: www.rukwa.go.tz
Twitter: @Rukwakwetu
Simu Na: 025-/2802138/2802144
Fax Na. (025) 2802217
Post A Comment: