KUINGIA NCHINI BILA KIBALI,
Mnamo tarehe 21.03.2019 saa 16:30 jioni huko eneo na Kata ya Lupa Tingatinga, Tarafa ya Kipambawe. Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Polisi walimkamata OMARY JUMA @MWAMI [21] raia wa nchi ya Burundi akiwa ameingia nchini bila kibali na kufanya shughuli za kilimo cha Tumbaku. Upelelezi unaendelea.
UNYANG’ANYI WA KUTUMIA NGUVU
Mnamo tarehe 21.03.2019 saa 00:30 usiku huko maeneo ya Veta Kata ya Ilemi, Tarafa ya Iyunga ndani ya Jiji na Mkoa wa Mbeya. IMAN ANDISON [20] Dereva bodaboda na mkazi wa Simike alinyang’anywa pikipiki yake yenye namba za usajili MC 833 BVS aina ya Kinglion na watu watatu wasiofahamika.
Mbinu iliyotumika ni kwamba muhanga akiwa amepaki pikipiki yake maeneo ya Kiwira Motel alitokea abiria mmoja na kutaka apelekwe Veta na ndipo alipomfikisha maeneo hayo walijitokeza watu wengine wawili na kumvamia kisha kumjeruhi kichwani na watu hao kutokomea na pikipiki hiyo. Majeruhi amelazwa Hospitali ya Rufaa Mbeya. Uchunguzi/upelelezi unaendelea kuwabaini waliohusika katika tukio hilo.
KUINGIZA NCHINI BIDHAA BILA KULIPIA USHURU.
Mnamo tarehe 22.03.2019 saa 07:00 asubuhi huko Uwanja wa Siasa uliopo Kata ya Mbugani, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya, Polisi wakiwa Doria walimkatama mtu mmoja aitwaye ZACHARIA MWANGUKULU [28] Mkazi wa Mbugani akiwa ameingiza nchini bidhaa mbalimbali bila kulipia ushuru.
Bidhaa alizokamatwa nazo mtuhumiwa ni:-
Mipira ya kiume [Condoms] aina ya Chishango Boksi 45.
Juisi aina ya BAK’S Boksi 27
Mafuta ya Kula aina ya Cook Well ndoo moja yenye ujazo wa lita 10
Mifuko ya Plastiki aina ya Soft vifurushi 03
Bidhaa hizo zilikuwa zikisafirishwa kwenye gari lenye namba za usajili T.532 CGU aina ya Toyota Noah iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aitwaye ABRAHAM MWARABU [32] Mkazi wa Njisi Kasumulu Kyela ambaye naye amekamatwa.
Bidhaa hizo zimeingizwa nchini zikitokea nchi jirani ya Malawi kwa kutumia njia na vivuko visivyo halali. Taratibu za kuzikabidhi bidhaa hizo Mamlaka ya Mapato Tanzania zinafanyika.
Imetolewa na:
ULRICH O. MATEI – SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA
Post A Comment: