Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora Erick Komanya akitoa salamu za Mkoa wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Mpango wa Elimu changamani kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu(IPOSA).
Baadhi ya washiruiki wa uzinduzi wa Kitaifa wa Mpango wa Elimu changamani kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu (IPOSA) leo mjini Tabora.
Mwenyekiti wa Bodi wa Baraza la Usimamizi Taasisi ya Elimu ya Watu Waziri Naomi Katunzi akitoa salamu za Taasisi hiyo wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana walio nje ya Mfumo rasmi (IPOSA) leo mjini Tabora.
Mratibu wa Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana walio nje ya Mfumo rasmi wa Elimu (IPOSA) akitoa ufafanuzi jinsi watakavyoendesha mafunzo kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi leo mjini Tabora.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tixon Nzunda akitoa maneno ya utangulizi kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi ili azindue Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu(IPOSA) leo mkoani Tabora.
Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo akitoa hotuba wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Mpango wa Elimu Changamani kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu (IPOSA) leo Tabora. Picha na Tiganya Vincent
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Seleman Jafo imezitaka Taasisi zinazosimamia mifumo ya elimu kutoweka vikwazo na masharti magumu kwa vijana wenye ufaulu mdogo kuendelea na kozi mbali mbali.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akizindua Kitaifa Mpango wa Elimu Changamani kwa vijana walio nje ya Mfumo rasmi wa Elimu (IPOSA). Jafo alisema kuwakwamisha vijana wenye ufaulu mdogo kuendelea na kozi mbalimbali kwa vigezo vya kuwa na ufaulu wa chini ni kuwanyima vijana haki ya kupata ujuzi.
“Tuache kuweka mifumo yenye roho mbaya inayokwamisha vijana kielimu na ndoto zao za kishiriki uchumi wa viwanda” alisema. Jafo alisema kuwa wapo watalaamu wanakaa Ofisini na kuweka vigezo ambavyo vinalenga kukwamisha vijana kuendelea na mafunzo yakiwemo ya ufundi na kuwafanya kushindwa kushirikia katika ujenzi wa uchumi wa viwanda
Waziri Jafo aliitaka Taasisi ya Elimu ya watu Wazima kuweka mpango kwa vijana ili waweze kuendelea na vyuo vya juu ili taifa liweze kuwa na wataalam wengi. Kuhusu Mpango wa Elimu Changamani ( IPOSA) alisema umekuja kujibu kauli ya utekelezaji wa uchumi wa viwanda kwani unajengwa na vijana wenye Maarifa.
Waziri Jafo amewaagiza Wakuu wa Mikoa nane na wilaya zake ambako mpango wa IPOSA unatekelezwa kusimamia ipasavyo na baadae uweze kuenea nchi nzima kama ilivyokusudiwa. Alisema utekelezaji wa Mpango wa IPOSA usiwe wa zimamoto bali uwe endelevu ili vijana wanufaika waweze kushiriki katika ujenzi wa maendeleo ya Taifa.
Jafo aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutoa fedha kila mwezi kwa ajili ya kugharamia watoto wa kitanzania kupata elimu bila malipo. Alisema jumla ya shilingi bilioni 23.8 zinatolewa kila mwezi kwa ajili ya kugharamia wanafunzi kusoma bila mzazi kulipa ada na kuwataka watoto kutumia fursa hiyo kusoma kupitia mfumo rasmi.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Tixon Nzunda alisema Mpango wa Elimu Changamani kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi unatekelezwa kwa majaribio mikoa nane hapa nchini. Alitaja mikoa hiyo ni Kigoma, Tabora, Dar es salaam, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe na Dodoma.
Nzunda alisema mpango wa IPOSA awamu ya kwanza unatarajia kuwanufaisha vijana wapatao 10,000 kati ya vijana milioni 3.5 waliopo nje ya mfumo rasmi wa elimu. Alisema Ofisi ya TAMISEMI kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kama vile UNICEF walitembelea na kubaini vituo 72 vitakavyotekeleza mradi huo katika mikoa hiyo.
Kwa upande wa Mratibu wa Mpango huo Dkt. Sempheo Siafu alisema kuwa mpango huo utachukua miezi 20 hadi kukamilika huku ufundishaji ukifanyika kwa njia ya nadharia na vitendo ukiwahusisha vijana wenye umri wa miaka 14 hadi 17. Alisema lengo kuu la mpango huu ni kuhakikisha kuwa na vijana walioelimika, wenye maarifa, ujuzi na stadi za kuweza kuchangia kwa haraka maendeleo ya taifa na kuhimili ushindani.
Post A Comment: