Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas
Katambi amefanya ziara kwenye shule mbili za Msingi na moja ya
Sekondari ambazo ziliezuliwa paa zake kufuatia mvua kubwa iliyonyeesha
hivi karibuni Wilayani humo.
DC Katambi amefanya ziara hiyo katika shule za msingi Nzuguni na Ihumwa na Sekondari ya Ihumwa ambapo aliambatana na
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na maafisa elimu msingi na
Sekondari na kutoa maagizo kwa mhandisi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha
madarasa yaliyokumbwa na dhahama hiyo yanafanyiwa matengenezo haraka ili
wanafunzi waweze kuendelea na masomo yao kama kawaida.
"Nimesikitishwa na hii kadhia mliyoipata na ndio maana
nikafika hapa ili niweze kujionea mwenyewe, Serikali ya awamu ya tano
chini ya Rais Magufuli imedhamiria kutoa elimu bure hivyo changamoto
kama hizi zinazojitokeza lazima tuzitatue kwa haraka, hivyo nitoe
maagizo kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji kupitia kwa Mhandisi kuhakikisha
majengo yaliyoharibiwa yanafanyiwa ukarabati upesi ili vijana wetu
waweze kuendelea na masomo yao" amesema DC Katambi.
DC Katambi pia aliwataka waalimu wa shule hizo
kuhakikisha wanadhibiti utoro pamoja na tatizo la mimba kwa wanafunzi wa
kike na kuagiza kutoa ripoti ofisini kwake kwa mtu yeyote ambaye
atabainika kumpa mimba mwanafunzi.
"Ndugu zangu jukumu la kuzuia mimba mashuleni ni letu
sote, wote tuwe walinzi wa hawa vijana wetu, kama tutawalea vizuri basi
hapa ndipo tutakapowatengeza wakuu wa Wilaya , Mikoa na Mawaziri wa
baadaye," amesema DC Katambi.
Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Dodoma,
Joseph Mabeyo amemshukuru DC Katambi kwa kutembelea shule hizo pamoja
na kutoa maelekezo kwa Mhandisi ili aweze kufanyia matengenezo madarasa
yaliyoharibika na kumuomba aendelee kutolea macho sekta ya elimu kwani
ndipo yalipo mafanikio ya nchi zote zilizoendelea duniani.
Mimi nakushukuru sana Mhe DC kwa kuacha shughuli zako
ofisini na kufika kutuona, tumefarijika sana na hakika hii inatufanya
tuone Serikali yetu chini ya Rais Magufuli inafanya kazi kwa wananchi
wake, tunashukuru kwa maelekezo yako ambayo umeyatoa," amesema Mabeyo.
*Imetolewa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Dodoma.*
Post A Comment: