Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Patrobas Katambi amesema hatomvumilia mtu yeyote ambaye atawaonea wanawake wajane na kuwataka wanawake hao kufika ofisini kwake pindi wanapokutana na changamoto za unyanyasaji.

DC Katambi ameyasema hayo alipokua akizindua semina ya Ujasiriamali iliyoandaliwa na Chama cha Wanawake wa Filamu Tanzania ambapo aliwaahidi kushirikiana nao katika kutatua changamoto zinazowakabili kina Mama hao ikiwemo kutafuta wadau ambao watawasaidia kina mama hao katika nyanja mbalimbali.

“ Hiki mlichokifanya leo Dada zangu na Mama zangu wa Bongo Movie ni jambo ambalo Serikali ya awamu ya tano inaliunga mkono, na naamini hata Rais Magufuli atafurahia hichi mlichokifanya na kwa sababu ni Rais wa wanyonge basi ataona namna ya kuweza kuwasaidia kupitia Wizara zake,” amesema DC Katambi.

DC katambi pia alitumia nafasi hiyo kugawa msaada wa baiskeli za walemavu ‘Wheelchair’ pamoja na magodoro kwa akina mama wajane wenye uhitaji.

Katika hatua nyingine DC Katambi amezindua mradi wa kuwawezesha wanawake kuendeleza sekta ya kilimo na biashara ambapo amesema umuhimu wa sekta ya kilimo katika Mkoa wa Dodoma utabaki hivyo kwa muda mrefu kabla ya chanzo cha kipato kwa walio wengi hakijahamia katika sekta nyingine za kiuchumi.

“ Niwapongeze waandaaji wa mradi huu ambao ni Taasisi ya SAT na sisi kama Serikali tutahakikisha mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi na kuweza kutoa matokeo yaliyokusudiwa na nitoe maagizo kwa wataalam wetu kushirikiana nanyi katika kufanikisha jambo hilo ambalo litawakomboa wanawake wengi wa Dodoma,” amesema DC Katambi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: