Mgogoro wa mipaka uliodumu kwa miaka mitano katika Kata ya Zanka, Kitongoji cha Halo Wilayani Bahi umemalizika leo baada ya Wakuu wa Wilaya za Dodoma na Bahi kumaliza mkanganyiko uliokuwepo kwenye eneo hilo kwa muda mrefu.
Toka mwaka 2014 eneo hilo limekua likikabiliwa na mgogoro ambapo baadhi ya wananchi na viongozi wakijitangaza kutii mamlaka ya Wilaya ya Bahi na wengine wakitii Wilaya ya Dodoma Mjini.
Mkutano huo uliofanyika leo ukiongozwa na Wakuu wake wa Wilaya, Mhe. Patrobas Katambi kwa upande wa Dodoma Mjini na Mwanahamis Mungunda wa Bahi ambao waliongozana na wajumbe wa kamati za Ulinzi na Usalama pamoja na wataalamu wa ardhi ambao walithibitisha eneo hilo kuwa ndani ya Wilaya ya Bahi kwa mujibu wa Sheria.
"Kwa muda mrefu kumekuwepo na malalamiko kwenye eneo hili la Halo juu ya mipaka, kesi nyingi zimeshakuja ofisini kwangu na nikazitolea maelekezo, tunafahamu kumekuwepo na viongozi wanaoshinikiza baadhi ya wananchi kulazimisha kuwa Manispaa ya Dodoma ilihali wapo Bahi, mnapaswa kutambua wote ni Watanzania na Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Magufuli inagawa huduma sawa kwa wananchi wake wote hivyo ukiwa Bahi au Dodoma kote utahudumiwa sawa lakini lazima tufuate Sheria za Nchi ambazo zinaelekeza pia juu ya mipaka ya Wilaya na Mikoa yetu," amesema DC Katambi.
Mhe Katambi ameongeza kuwa mgogoro huo ulisababishwa na kutokuelewa ambapo vikao vingi vilikaa bila mafanikio na kuwataka wananchi kuelewa kuwa suala la mipaka haliamuliwa kwa utashi wa mtu bali sheria za Nchi.
*Hiki ni kikao cha sita tunakaa baada ya vikao vingi kufanyika bila kuleta muafaka, nachosema sasa sio Mimi Katambi sheria iko hivi, mwenye mamlaka ya kugawa Nchi katika mikoa, wilaya, tarafa mpaka vitongoji ni Rais na sheria zilizotungwa na Bunge au GN, ukisoma katiba yetu ya mwaka 1977 ibara ya 2(1) na (2), land act S.4, GN GDNEDC No 190 (2007), mamlaka ya miji (mgawanyo kata) GN No. 294 na sehemu ya 27 kata ya Chihanga na mipaka ya wakati huo manispaa ya Dodoma GN No 89 ya 1983 pamoja na ramani za mipaka utajua hakuna mgogoro wowote baina ya wilaya hizi mbili,"* amesema DC Katambi.
Amesema ni suala la kukosa ueleww au uchochezi wa makusudi unaofanywa kisiasa na kuwaonya wote kuwa hakuna mwenye mamlaka ya kubadilisha au kuigawa Nchi isipokua Rais au sheria zilizotungwa na Bunge.
Kwa upande wake DC wa Bahi Mhe. Mwanahamis aliwataka wananchi hao sasa kuungana na Serikali yao kufanya shughuli za kimaendeleo baada ya muafaka kupatikana na kuwaomba kushirikiana nae kuhakikisha Wilaya ya Bahi inasonga mbele na kuwa ya mfano kwa Wilaya zingine.
"Sasa naamini leo kila mmoja ataondoka hapa akiwa ameridhika baada ya wataalamu wetu wote wa Dodoma na Bahi kutuonesha kuwa eneo hili la Halo lipo Bahi na hiyo ni kwa mujibu wa vipimo vya GN, niwatake sasa kuacha migogoro isiyo na lazima na kuungana na Serikali yenu katika kufanya kazi, tumuunge mkono Rais wetu Dk Magufuli kwa kufanya kazi na siyo kuchochea migogoro," amesema DC Mwanahamis.
Nao wananchi wa eneo hilo kwa pamoja waliwashukuru wakuu hao wa Wilaya Kwa kufika huku wakisema ni Mara ya kwanza kwa wakuu wa Wilaya hizo mbili kufika katika eneo hilo na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mipaka yao na kuahidi kutii mamlaka ya Wilaya ya Bahi kwa kushirikiana na Serikali yao kuleta maendeleo kama sehemu yao ya kumuunga mkono Rais Magufuli.
Imetolewa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Dodoma
Post A Comment: