Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Patrobas Katambi amefungua rasmi mashindano ya maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wasichana na Tehama ikiwa ni mkakati wa Kimataifa wa kuchochea uelewa juu ya kuwawezesha na kuwahamasisha wasichana wadogo ili wachague mchepuo wa fani ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

DC Katambi amesema katika mashindano hayo jumla ya wanafunzi 96 wa Shule za Sekondari kutoka mikoa 12 watapatiwa mafunzo ya msingi ya uandishi wa program za Kompyuta ambapo baadae watashindanishwa na kupatikana washindi 12 watakaoenda kushindana ngazi ya Kitaifa.

“ Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru waandaaji wa mashindano haya ambao ni Mfuko wa Mawasiliano kwa juhudi kubwa mliyoionesha kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na walimu wote waliofanikisha shughuli hii.

“ Nitoe rai kwa wanafunzi mliopo hapa kuondoa dhana ya kwamba masomo ya Sayansi ni ya watoto wa kiume tu, wengi mnaamini ni magumu lakini kama mtaamua kwa dhamira ya dhati basi ni imani yangu kuwa mafunzo hata mtakayojifunza yataacha alama mioyoni mwenu na kuja kuwa msaada mkubwa kwa Taifa letu.

“ Niwatie moyo na niwahakikishie kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wetu, Dk John Magufuli imedhamiria kwa dhati kuwapa kipaumbele watoto wa kike na kuhakikisha kuwa inatoa fursa mbalimbali za kujifunza ili kuongeza ufanisi na kutengeneza kizazi bora cha watoto wa kike,” Amesema DC Katambi
Share To:

msumbanews

Post A Comment: