Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Shinyanga kimemkana aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja kuwa hakuwa mwanachama wa chama hicho ila alikuwa kama mshenga wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Ijumaa Machi 8, 2019 Katibu wa Chadema mkoa wa Shinyanga, Zakaria Obadi alisema Mgeja hakuwa mwanachama wa Chadema ila alikuwa mshenga tu wa Lowassa hivyo walishangaa kuona anatangaza kwa waandishi wa habari anahama Chadema na kuhamia CCM.

Obadi alisema Mgeja ametangaza akisema alihamia mwaka 2015 lakini chama kinajua alikuja kama mshenga kwa sababu hakukabidhiwa hata kadi ya Chadema hivyo chama kilikuwa hakimtambui kama ni mwanachama.

Alisema wao kama viongozi wa mkoa wana haki ya kumjibu Mgeja kwani hastahili kujibiwa makao makuu, kwa sababu hakuwepo hata kwenye taarifa za chama hata kuvaa mavazi ya Chadema hajawahi, wao wanawatambua wanachama.

Mgeja alitangaza kuhamia Chadema mwaka 2015 mara baada ya Lowassa kufanya hivyo Julai 28, 2015 lakini hivi karibuni, Lowassa alitangaza kurudi CCM na sasa Mgeja naye amechukua uamuzi kama wa Lowassa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: