Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Arusha, kimemtaka Mbunge Joshua Nassari, aliyevuliwa ubunge na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kukusanya vielelezo vyote ili shauri hilo lipelekwe kwenye mikono ya sheria.

Agizo hilo lilitolewa mjini hapa jana na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha ambaye pia ndiye Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa.

Akizungumza kwa njia ya simu juu ya sakata hilo la kuvuliwa ubunge Nassari, Golugwa, alisema watapeleka vielelezo hivyo ili mikono ya sheria itafsiri uamuzi uliofanywa na Spika Ndugai.

 “Chama na Nassari tupo naye imara kuhakikisha tunachukua hatua za haki. Ndio maana tumemwambia akusanye vielelezo vyote vya taarifa alizoandika kwetu na kwa Spika,” alisema Golugwa na kuongeza:

“Sisi hatuoni utoro hapo wa kutohudhuria vikao vya Bunge kama taarifa inavyojieleza, kwani alikuwa anatoa taarifa za kuhudhuria masomo nje ya nchi pamoja na matibabu ya mke wake.

“Kwenye mikono ya sheria tunaamini hakuna wanasheria wala majaji watakaovumilia jambo hili.

“Lakini alikuwa akihudhuria vikao vya Kamati za Bunge, uthibitisho upo posho alizokuwa analipwa kwenye vikao vya Kamati ushahidi upo, pengine kesho Nassari atazungumza na wanahabari,” alisema.

Golugwa aliendelea kufafanua kwamba, kati ya wabunge vijana waliofanya vizuri kwenye majimbo yao ni pamoja na Nassari kwani amekuwa na kumbukumbu nzito kwa masuala ya kuhudumia jamii.

“Nassari si mtafuta sifa, ni kijana amekuwa karibu na wananchi, anajituma kutafuta wadau wa maendeleo watakaoleta miradi ya macho, maji, madarasa kwenye eneo lake.

 “Hapa hatutetei ubunge tu, tunaangalia kwa upana mzima kwamba unawaondolea wananchi mwakilishi wao kwa utaratibu gani, ili tu uchaguzi uitishwe tena kwa mamilioni ya fedha,” alisema Golugwa.

Nassari alivuliwa ubunge juzi kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo, huku mwenyewe akisema amepokea taarifa hiyo akiwa kwenye kazi za kibunge mkoani Kilimanjaro na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Share To:

Post A Comment: