Msimamizi msaidizi wa mradi wa maji wenye thamani ya Shs. 152 milioni, Baltazar Mtenga (kushoto) kutoka kampuni ya Ifango General Enterprises, akielezea changamoto za kukwama kwa mradi huo mbele ya Mwenyekiti wa CCM Tawi la Mbagala Charambe Machinjioni, Shaibu Omari Naputa (kulia) na Mwenyekiti wa Mtaa wa Machinjioni A, Mkonge Hassan Katani (wa pili kulia) wakati Halmashauri Kuu ya tawi hilo ilipofanya ziara kukagua miradi ya maendeleo mwishoni mwa wiki.

Na Mwandishi Wetu
HALMASHAURI ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tawi la Charambe Machinjioni katika Jimbo la Mbagala mkoani Dar es Salaam imeonyesha kukerwa na ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi miwili ya maji yenye thamani ya zaidi ya Shs. 170 milioni.

Akizungumza mwishoni mwa wiki katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo iliyoko katika Mtaa wa Machinjioni A, Mwenyekiti wa CCM wa tawi hilo, Shaibu Omari Naputa, alisema kutokamilika kwa miradi hiyo muhimu kunaitia doa Serikali ya CCM, ambayo imedhamiria kuwaletea wananchi maendeleo.
Miradi hiyo ya maji, mmoja ukitekelezwa na Halmashauri ya Wilaya na mwingine ukiwa umefadhiliwa na Ofisi ya Jimbo, ingeweza kuwahudumia wakazi zaidi ya 30,000 jimboni humo, ambao kwa sasa wanapata shida kubwa ya kupata huduma hiyo.
“Miradi hii ilikuwa ikamilike zaidi ya mwaka mmoja ulipita, lakini mpaka sasa ujenzi unasuasua huku mradi unaofadhiliwa na Ofisi ya Jimbo ukiwa umekwama na vifaa kung’olewa,” alisema Naputa.
Katika mradi wa kwanza ambao ulikuwa chini ya taasisi ya CHADEA kabla ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kuuchukua, ulitengewa takriban Shs. 152 milioni ili kuupanua kwa kujenga tenki kubwa na vituo vitano vya kusambazia maji pamoja na pampu, lakini badala ya kukamilika Mei mwaka 2018, mpaka sasa hata ujenzi wa tenki haujakamilika.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Mkonge Hassan Katani ambaye aliongoza ziara hiyo, alisema kwamba, kwa vile wasimamizi wakubwa ni Halmashauri ya Manispaa yeye hana mamlaka ya moja kwa moja ya kuwahimiza wakandarasi wamalize haraka ujenzi, kwani licha ya mradi huo kuwepo mtaani kwake, hajui hata mikataba yao ikoje.
“Nimekuwa nikiwaulizia tu wakandarasi, lakini wanatoa sababu kwamba hawajapatiwa fedha kutoka halmashauri, sasa kwa sababu halmashauri wenyewe ndio wasimamizi, inakuwa vigumu kwangu kuwahimiza," alisema.
Msimamizi msaidizi wa mradi huo kutoka kampuni ya Ifango General Enterprises, Baltazar Mtenga, alisema kinachokwamisha ni fungu la fedha kuchelewa kutoka halmashauri.
Alikiri kwamba, mradi huo ulikuwa ukamilike tangu Mei 2018, lakini mkandarasi akaomba kuongezewa muda kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kuchelewa kupewa fedha na halmashauri.
“Fedha zinatolewa kwa awamu, kila tunapojenga lazima waje wakague halafu waidhinishe fungu jingine, lakini kuna kipindi tulisubiri kwa karibu miezi mitatu bila kupata fedha, jambo ambalo linakwamisha utekelezaji.
“Tukipata fedha tunaweza kukamilisha ujenzi ndani ya mwezi mmoja,” alisema Mtenga wakati ujenzi wa tenki lenye uwezo wa kujaza lita 45,000 za maji ukiendelea.
Kwa upande wake, Naputa amemuagiza mkandarasi kuhakikisha anakamilisha mradi huo ndani ya mwezi mmoja kwani mpaka sasa ni mwaka mzima tangu mradi huo ulipokuwa ukamilike.
Aidha, amemuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa kuhakikisha anaidhinisha fedha kwa wakati ili wananchi wasiendelee kuteseka kutafuta huduma ya maji.
Kuhusu mradi wa maji uliokuwa utekelezwe na Ofisi ya Jimbo, Mwenyekiti wa Mtaa Bw. Katani alisema kwamba, ulitumia kiasi cha Shs. 24 milioni, lakini tangu kisima kilipochimbwa miaka mitatu iliyopita hakikuweza kutumika hadi Mei 2018 walipofunga pampu.
“Pampu ilipofungwa ikaanza kuvuta tope badala ya maji, kwahiyo hapa maji hayajatoka ingawa miundombinu yote ilikuwa imekamilika ikiwemo tenki na kituo cha kutolea maji.
“Baada ya kuona hivyo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala, Ally Mangungu, aliamua kuja kung’oa pampu na nyaya za umeme kwa kuhofia zingeweza kuibiwa, lakini mpaka sasa sijui vifaa hivyo vilivyong’olewa viko wapi japokuwa alisema angeibadilisha pampu,” alisema Katani.
Kwa upande wake, Naputa alisema kwamba, anaamini fedha hizo za Mfuko wa Jimbo hazijawasaidia wananchi wa Mbagala, akaitaka Ofisi ya Jimbo iwajibike kwa sababu hasara iliyotokea imetokana na uzembe.
Miradi mingine iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa Ofisi ya Serikali ya Mtaa na Barabara ya Charambe-Buza ambao haujaanza licha ya kwamba tayari wakazi wote wamekwishalipwa fidia kupisha barabara hiyo.
Katani alisema, ikiwa barabara hiyo yenye urefu wa takriban kilometa 3 itakamilika basi itakuwa mkombozi kwa wananchi wengi na kupunguza msongamano, kwani magari, hasa yanayokwenda Tandika, Buza na Uwanja wa Ndege hayatalazimika kuzungukia Temeke.
Kuhusu ujenzi wa Ofisi ya Serikali ya Mtaa, wana-CCM hao wameonyesha mashaka ya matumizi ya Shs. 8 milioni zilizotolewa na Halmashauri ya Manispaa na kusimamiwa na Ofisi ya Kata, kwani gharama zilizotumika zinaonekana kuwa ndogo kuliko fedha zilizotolewa.
Naputa amesema watamwandikia barua Katibu wa CCM wa Kata ili kumtaka Ofisa Mtendaji wa Kata aeleze mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo kwa kuwa wanahisi kuna ufisadi mahali.
Mwenyekiti wa Mtaa, Bw. Katani, alisema mpaka kuezekwa jengo la ofisi hiyo zimetumika Shs. 13 milioni na kwamba kuna upungufu wa Shs. 7 milioni ili ofisi hiyo ikamilike pamoja na miundombinu yake.

Mwenyekiti wa CCM Tawi la Mbagala Charambe Machinjioni, Shaibu Omari Naputa (katikati) na Mwenyekiti wa Mtaa wa Machinjioni A, Mkonge Hassan Katani (kushoto) wakiwa katika kituo cha kutolea maji katika mradi wa maji uliofadhiliwa na Mfuko wa Jimbo la Mbagala ambao umekwama.

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya tawi la Charambe Machinjioni katika Jimbo la Mbagala wakiwa katika Ofisi wa Serikali ya Mtaa wa Mmachinjioni A ambayo haijakamilika.


Maendeleo Vijijini Blog (Kwenye Rasilimali Kulikosahaulika) Twitter: @MaendeleoVijiji Instagram: #Maendeleo_Vijijini Cell: +255 - 0656 - 331 974 Whatsapp: +255 - 656 - 331 974
Share To:

Post A Comment: