Na WAMJW - DSM

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefanikiwa kuokoa takribani kiasi cha shilingi Bilion 10 kwa mwaka ambazo zingetumika katika kuhifadhi chanjo za watoto pamoja na vifaa, kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa bohari ya taifa ya chanjo iliyogharimu kiasi cha shilingi bilion 1.2.

Ameyasema hayo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu pindi alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la bohari ya Taifa ya Chanjo, akiongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt .Zainab Chaula.

Kwa kiasi kikubwa Waziri Ummy ameridhishwa na hali ya ujenzi huo, hususan katika ujenzi wa vyumba vya kuhifadhia chanjo (stoo), jambo litalosaidia wananchi hususan Wazazi wenye watoto wadogo kupata Chanjo kwa wakati.

Pia,  Waziri Ummy amempongeza Meneja Mpango wa taifa wa chanjo Dkt.Dafrosa Lyimo kwa kushirikiana na Mkandarasi kwa usimamizi mzuri wa jengo hilo hadi kufikia hatua ya mwisho.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara kuu ya Afya Dkt Zainab Chaula ameahidi kuendelea kusimamia vizuri shughuli zote ili kuendelea kuboresha Sekta ya Afya kwa kasi ili wananchi wa hali zote wanufaike.

Kwa upande mwingine Dkt. Zainab Chaula amesisitiza juu ya ushirikiano baina ya Watumishi katika Sekta ya Afya ili kurahisisha utendaji kazi kwa urahisi katika ngazi zote, hali itayosaidia wananchi kupata huduma bora.

Kwa upande wake Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo Dkt.Dafrosa Lyimo amesisitiza kwamba jengo hilo litakapokamilika  litaleta faida nyingi katika kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo kurahisisha usambazaji wa chanjo katika ngazi ya Mkoa, na kurahisisha upatikanaji wa chanjo hizo katika ngazi zote kwa wakati wowote.

Dkt.Lyimo ameahidi kuendelea kusimamia kwa ukaribu shughuli zote za mpango huo ikiwemo upatikanaji wa Chanjo kwa wakati wote na mahali popote ili wananchi waendelee kupata huduma hiyo.

Mwisho.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: