*Asema lengo ni kuondoa manung’uniko kwa watumishi wa taaluma moja
WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa, ameutaka uongozi wa Hospitali ya Aga Khan uandae
skeli ya mishahara inayofanana kwa watumishi wenye taaluma zinazofafana
ili kuondoa manung’uniko baina ya wafanyakazi wa taasisi hiyo.
Ameyasema
hayo kutokana na malalamiko ya watumishi wa taasisi hiyo ambao wanadai
kuwepo kwa tofauti ya mishahara kwa watumishi licha ya kuwa na taaluma
moja na kufanyakazi kwenye kituo kimoja.
Hayo
yalisemwa jana (Jumamosi, Machi 9, 2019) na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa, wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya
Aga Khan jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.
Waziri
Mkuu alisema suala la maslahi kwa watumishi ni muhimu na linatiliwa
mkazo na serikali hivyo uongozi wa Hospitali ya Aga Khan fanyeni mapitio
ya mishahara hasa kwa watu walio katika taaluma zinazofanana.
“Serikali
imeunda Tume ya Mishahara na Motisha inayofanya mapitio ya ngazi za
mishahara ili kuondoa utofauti wa mishahara kwa watumishi waliosoma
ngazi moja, wenye taaluma moja wanaofanyakazi kwenye kituo kimoja.”
Waziri
Mkuu aliongeza kuwa suala la uwiano wa mishahara kwa watumishi wenye
taaluma zinazofanana ni muhimu na linapaswa lifanywe kwa watumishi wote
bila ya kujali kama mtumishi huyo ni Mtanzania au anatoka nje ya
Tanzania.
Awali,
Waziri Mkuu alitembelea maeneo mbalimbali ya kutolea huduma katika
jengo hilo ikiwemo maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya watoto, wodi ya
wazazi. Ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu sh. bilioni 192, kati yake
sh. bilioni 134 ni mkopo wa muda mrefu wenye masharti nafuu kutoka
Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MACHI 10, 2019.
Post A Comment: