Maafisa wawili wa trafiki katika barabara ya Port-Bumala nchini Kenya wamejikuta katika wakati mgumu baada ya kupokea kichapo cha mbwa kutoka kwa afisa wa polisi mmoja wa kikosi cha kupambana na ghasia 'General Service Unit (GSU)' aliyekuwa na gadhabu baada ya kushuhudia askari wenzake hao wakipokea rushwa  kutoka kwa mwendesha bodaboda.

 Katika ripoti iliyochapishwa na Citizen,tukio limetokea Jumanne, Machi 5,2019 mchana baada ya afisa huyo wa usalama (GSU), ambaye alikuwa anapita katika kizuizi hicho kuwasuta maafisa hao wa trafiki kutokana na jinsi walivyokuwa wakimnyanyasa mwendesha bodaboda na mteja wake. 


 “Mmoja wa maafisa hao wa polisi kwa jina Onyango alimzaba kofi afisa huyo wa GSU jambo ambalo lilimpandisha mori na kumlazimu kumvurumishia Onyango Makonde mazito mazito katika hali ya kujihami," mmoja wa walioshuhudia alisema. 

Kwa mujibu mmoja wa walioshuhudia tukio hilo, afisa huyo wa GSU ambaye ni mkazi wa eneo la Funyula aliwatandika maafisa hao wote wawili, wakati walipomvamia kwa pamoja na kuwalazimu kukimbilia katika eneo la Sio Port walipozidiwa na kichapo.

 Inakisiwa kuwa, Onyango alipatwa na majeraha ya kichwani ambapo alitibiwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Sio Port na kuruhusiwa kwenda nyumbani. 

Tukio hilo liliwasisimua wakazi wa eneo hilo, ambao waliwakashifu kwa vikali maafisa hao wa trafiki kwa mazoea ya kupokea mlungula na kuwahangaisha waendesha boda boda.

Aidha inakisiwa kuwa Onyango ambaye hakuridhishwa na tukio hilo alimfuata afisa huyo wa GSU hadi soko la Funyula akimtaka wakabane koo kwa mara ya pili.

 Hata hivyo, wakazi walimtahadharisha afisa huyo wa GSU kutojiingiza katika mtego wa Onyango kwa kuwa tayari alikuwa ameandamana na wenzake wanne kando na kujihami na kisu.

 Hata hivyo, kamanda wa polisi wa eneo la Busia, John Nyoike, amedhibitisha kisa hicho na kufichua kuwa uchunguzi dhidi ya maafisa hao ambao wanavalia sare za raia umeanzishwa. 
Share To:

msumbanews

Post A Comment: