WANASAYANSI na wanataaluma wanadaiwa kushindwa kutumia fursa za upatikanaji machapisho na majarida yaliyomo kwenye mitandao ili yawasaidie katika kazi za ufundishaji na utafiti.
Takwimu zimebainisha kwamba machapisho yaliyo kwenye mitandao yamekuwa yakitumika chini ya asilimia 30 tangu mwaka 2002 yalipoanza kuwekwa kwenye mitandao.
Kutokana na changamoto hiyo, Umoja wa Mataifa (UN), ulianzisha mradi utakaowawezesha wanasayansi kujengewa uwezo wa namna ya kupata na kutumia machapisho na majarida yaliyomo kwenye Benki ya Teknolojia.
Akizungumza wakati wa kuwajengea uwezo wasayansi na wanataaluma, katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Makamu Mkuu wa Chuo cha Biashara (CBE) na Mratibu wa Mradi huo Professa Tandi Lwoga alisema, mradi huo utawezesha kufikia malengo ya Tanzania ya viwanda.
Alisema mafunzo hayo yalilenga watafiti, wakutubi na wanaohusiana na masuala ya TEHAMA ili waweze kupata machapisho yaliyo kwenye mitandao (online) na kuwasaidia katika kazi za ufundishaji na utafiti.
“Tulianza Julai mwaka huu tumewajengea uwezo wanasayansi na wanataalumu zaidi ya 170 tumeyafikia Mashirika na Taasisi za elimu zaidi ya 60,” alisema Prof. Lwoga na kuongeza:
“Tangu mwaka 2002 hawa washirika wa utafiti (Research4life) waliopo Marekani wakishirikiana na wachapishaji walihakikisha nchi zinazoendelea zinapata machapisho haya kwenye mitandao,”
“Ndio maana mwaka jana UN iliamua kuanzisha Benki ya Teknolojia itakayowajengea uwezo wa kuangalia watafiti wanahitaji machapisho gani na jinsi ya kuyapata kupitia Tehama,” alisema.
Alisema mradi huo umelenga kuhakikisha machapisho yanapatikana kwa urahisi na gharama nafuu kwani kwa chuo kimoja kununua machapisho na majarida gharama zake hufikia Sh milioni 20 hadi 40 kwa kanzi data moja.
“Kwa kushindwa kupatikana machapisho husababisha tafiti zisifanyike wakati machapisho yapo mitandaoni ila hayatumiki kwamba wanasayansi hawajui kama yapo au namna ya kuyapata,”
“Research4 Life wana mitandao yenye machapisho kuhusu afya, kilimo, mazingira na masuala ya kisheria.Mradi utawezesha kuingia na kuyatumia kwenye shughuli za kitafiti na taaluma kisha kutatu matatizo ya jamii,” alisema Prof. Lwoga.
Alisema mradi huo umeanza kutekelezwa kwa mwaka huu katika nchi 12 za Afrika na Asia na utaendelea kwenye nchi 47 huku ghrama zake zikiwa chini ya Umoja huo wa mataifa kupitia Benk Teknoloji.
Akifungua kongamano hilo Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi ya Nelson Mandela Taaluma, Tafiti na Ubunifu Prof. Antony Mshandete aliwataka watafiti kutumia fursa hiyo kutatua matatizo yanayoizunguka jamii.
“Upatikanaji machapisho Kieletroniki utasaidia dhana ya Afrika tunayoitaka mwaka 2063 ambayo inaweka msukumo kwenye kuangalia ni namna gani tunaweza kutumia TEHAMA kuboresha kilimo,” alisema Prof. Mshandete.
Naye Mkuu wa Maktaba Taasisi ya Nelson Mandela Dk. Neema Mosha alisema kongamano hilo lilishirikisha vyuo na taasisi mbalimbali kutoka Kilimanjaro na Arusha.
“Tulizoea machapisho kwenye mafaili ya karatasi, mradi huu unatujengea uwezo wa kuwa na machapisho Kieletroniki, tunaamini elimu zaidi itaendelea kutolewa kwa wanasayansi na wanataaluma,” alisema Dk. Mosha.
Post A Comment: