Mbunge wa Kigoma Mjini na kiongozi wa Chama Cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe amedai makosa anayoshtakiwa yanafanana na makosa ambayo walishawahi kushtakiwa baadhi ya waasisi wa bara la Afrika.
Kwa mujibu wa Zitto Kabwe, amedai kuwa kesi za namna hiyo ndizo zilizowahi kuwakumba baadhi ya waasisi, akiwemo muasisi wa Taifa la afrika kusini, Nelson Mandela pamoja na muasisi wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza mara baada ya kupatiwa dhamana, Zitto Kabwe amesema ; “kesi za namna hii wamefungwa wakina mandela, na mwalimu kwa hiyo sio jambo linalopaswa kuwatisha watu. Ila nasikitika sana jana sikushiriki kongamano la chuo kikuu cha Dar es salaam.
“Naamini lazima tuweze kutoa tafsiri mbadala juu ya kile kilichotokea jana, pia niwatake watanzania tuwe na mshikamano ili kuhakikisha nchi yetu inakuwa imara.”
Mbunge huyo wa Kigoma mjini anashtakiwa kwa makosa matatu ya uchochezi, ambapo katika kesi yake upande wa Jamhuri unawakilishwa na Wakili, Tumaini Kweka na upande mshtakiwa unawakilishwa na wakili Peter Kibatala.
Zitto alikamatwa na Jeshi la Polisi jijini Dar es salaam oktoba 31 mwaka huu kufuatia mkutano wake na waandishi wa habari ambapo alitoa madai ya kuawawa kwa zaidi ya raia 100 katika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma.
Kesi ya Mbunge huyo inatarajiwa kuendelea tena Novemba 12 mwaka huu.
Post A Comment: