Watanzania wametakiwa kushikamana kwa kufanya Kazi kwa bidii kwa lengo la kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ili Taifa liweze kutumiza malengo ya kufikia uchumi wa kati hadi ifikapo mwaka 2025.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya 19 ya hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere linalofanyika katika chuo Cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Waziri Ndalichako amesema Wizara itaendelea kukienzi Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ili kiendelee kuwa Kitovu cha maadili katika kuwajenga Viongozi na vijana ikiwa ni pamoja na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho Prof. Shadrack Mwakalila amewataka viongozi na wanafunzi kuhakikisha wanakitumia chuo hicho kwa ufanisi ili kupata mafunzo yanayohusu uzalendo, uadiifu na kuwa mafunzo yanayotolewa chuoni hapo ni yale ya muda mfupi na mrefu.
Prof. Mwakalila amesema kila mwaka chuo hicho huandaa maadhimisho ya kumbukizi ya Hayati wa Baba wa Taifa kwa Lengo la kujitathmini kama Taifa, tumetoka wapi na tuko wapi.
Katika kumbukizi hilo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo ile inayohusu Uhuru na Maendeleo katika kuelekea uchumi wa Kati, umuhimu wa uzalendo na uadilifu, umuhimu wa misingi ya Azimio la Arusha katika kustawisha Viwanda vya ndani.
Imetolewa na:
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
10/10/2018
Post A Comment: