Pichani ni daraja la Kijiji cha Getamok linalosuasua kukamilika kwake kutokana na changamoto mbalimbali
Na, Vero Ignatus,
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameiagiza kampuni ya Kiure Engineering Ltd kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa daraja uliogharimu Sh. milioni 250 fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo eneo la Getamok.
Gambo aliyasema hayo wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa daraja hilo ambalo ni muhimu kwaajili ya wakazi wa maeneo hayo.
Alisema kampuni ya Kiure Engineering Ltd imekuwa kikwazo kikubwa cha kutokamilisha ujenzi wa daraja hilo kwa muda uliopangwa hali iliyopelekea kuongezewa muda wa miezi nane ili wamalize ujenzi huo.
Amesisitiza kuwa lazima wakandarasi wazawa wakajithamini pale wanapoomba kazi za ujenzi wa aina mbalimbali za miradi ya maendeleo na kama hawana uwezo huo wa kufanya kazi ni vyema wakaacha kuepusha kuingia matatani kwani serikali inapotoa fedha kwaajili ya jambo fulani ni lazima likamilike kwa wakati.
“Tunawapa hadi Oktoba 23 mwaka huu daraja hili liwe limeshakamilika, na ikifika saa kumi jioni Mkuu wa Wilaya hii atakuja na OCD kuangalia kama mmekamilisha kinyume na hapo tutatumia nguvu za ziada kusukuma jambo hili”alisema Gambo
Pia niwaonye nyinyi wakandarasi wazawa mjitathimini maana mnaomba kazi halafu mnaleta ubabaishaji wa mara kwa mara na hamkamilishi kazi zenu kwa wakati, kama hamuwezi kazi acheni ” alisema Gambo.Naye Msimamizi wa Mradi huo kutoka kampuni ya Kiure Engineering Ltd, Said Idd alikiri ni kweli wamechelewesha kukabidhi daraja hilo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo mvua kubwa kunyesha mwezi Machi mwaka huu pia walipokuwa wakichimba udongo walikumbana na chemchem kubwa ya maji hali iliyopelekea kuchelewa kutekeleza ujenzi wa daraja hilo.
Alisema kwa sasa daraja hilo limekamilika kwa asilimia 90 na kazi iliyobaki hivi sasa ni kusambaza mawe na kuweka kingo za maji ikiwemo kurekebisha kasoro mbalimbali kwaajili ya kukabidhi kwa DC wa Karatu Bi. Theresia Mahongo.
Naye DC, Mahongo alisema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa daraja hilo na mara kwa mara alikuwa anaenda eneo hilo kuangalia ujenzi wake na kusisitiza kuwa ni vyema sasa wakandarasi wakapima uwezo wa kazi wanazotaka kuzifanya kwani uzembe wa mkandarasi huyo umepelekea kukatwa fedha zake za mradi huo baada ya kuzembea kazini.
Post A Comment: