Afisa Mkuu Mwandamizi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Rose Mahendeka (kushoto) akiwaeleimisha baadhi ya Wafanyabiashara wa Tunduma wakati wa Kampeni ya Usajili na Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea Mkoani Songwe.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) (kushoto) wakiwasajili na kuwapatia elimu ya kodi Wafanyabiashara wa Tunduma wakati wa Kampeni ya Usajili na Elimu kwa Mlipakodi inayoendelea Mkoani Songwe.(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-TRA).
Na. Benedict Liwenga-TRA.
WAFANYABIASHARA Mkoani Songwe wametakiwa kujitokeza kwa katika Kampeni ya Usajili na Elimu kwa Mlipakodi inayoendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kauli hiyo imetolewa leo na Afisa Kiongozi wa Kituo cha Huduma cha TRA mjini Tunduma wakati wa Kampeni ya Usajili na Elimu kwa Walipakodi mkoani hapo ambapo amewataka Wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kuweza kupatiwa huduma hiyo pasipo gharama yoyote.
Bwana Mwita ameeleza kuwa, mwitikio wa wafanyabiashara katika kampeni hiyo ni mkubwa, ambapo wengi wa Wafanyabiashara ambao walikuwa hawana Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (TIN) wameshasajiliwa na kupatiwa TIN hizo.
“Zoezi hili ni zuri na mwitikio wa watu ni mkubwa, niwaombe Wafanyabiashara waendelee kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupatiwa TIN na elimu kuhusu masuala ya kodi”, alisema Mwita.
Kwa upande wake Kiongozi wa msafara kutoka TRA Makao Makuu ambaye pia ni Afisa Mkuu Mwandamizi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Bi. Rose Mahendeka amesema kwamba, zoezi la usajili na utoaji elimu kwa mlipakodi litadumu mkoani Songwe kwa muda siku sita, ambapo wafanyabiashara wanahimizwa kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
“Kampeni hii katika Mkoa huu wa Songwe litadumu kwa muda wa siku sita na tayari tumeshaanza na maeneo mbalimbali kama vile Vwawa, Mlowo, Tunduma na baadaye tunaendelea na maeneo ya Mkwajuni, Ileje pamoja na Saza lengo ni kuwahamasisha wananchi hususan wafanyabiashara kuitikia wito wa kampeni hii”, alisea Mahendeka.
Afisa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi toka TRA, Bi. Maya Magimba anafafanua kuwa, zoezi la utoaji huduma katika kampeni hiyo limeonekana kuwavutia wakazi wengi wa mjini hapo ambapo mpaka sasa hawajakumbana na changamoto yoyote kubwa.
“Kwakweli mpaka sasa kampeni hii inaendelea vizuri na tumepata wateja wengi wenye uhitaji wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi na tayari tumewasajuli na kuwapatia TIN zao lakini pia tumewapa elimu. Kuhusu changamoto katika kampeni hii ni chache sana ambapo hazijatukwamisha kuendelea na zoezi letu la kuwahudumia walipakodi wetu”, alisema Magimba.
Kwa upande wao baadhi ya Wafanyabiashara katika Wilaya ya Momba mjini Tunduma wameeleza kufurahishwa na kampeni hiyo huku wakiiomba TRA kuendelea kuwapatia elimu kwani wengi wao walikuwa hawana elimu ya kutosha kuhusu masuala ya kodi na kuahidi kuwa mabalozi wa kuwahamisha wengine kulipa kodi kwa hiari.
Kampeni ya Usajili na Elimu kwa Mlipakodi katika Mkoa wa Songwe inalenga kuongeza idadi ya Walipakodi wapya ikiwemo kuwapatia elimu wafanyabiashara kuhusu masuala mbalimbali ya kodi, ambapo mpaka sasa jumla ya wafanyabiashara zaidi 100 mkoani hapo wamesajiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ambapo zoezi hilo bado linaendelea mpaka mwisho wa wiki hii.
Post A Comment: