Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Mwakyembe
Na Shamimu Nyaki – WHUSM
Wadau mbalimbali wameishauri Serikali kufikiria namna ya kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia shuleni ili kukuza na kuendeleza lugha hiyo ambayo ndio utambulisho wa Taifa letu.
Ushauri huo umetolewa leo Jijini Dodoma katika Mdahalo wa Kumbukizi ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius K.Nyerere uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha ST.Jonhs of Tanzania ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadilia na washiriki.
Awali Mhe.Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Mwakyembe akifungua mdahalo huo alisema kuwa lugha ya Kiswahili ndio lugha kuu ya mawasiliano hapa nchini na ndio lugha inayowatambulisha watanzania Ulimwenguni. “Kiswahili hivi sasa ni lugha kubwa sana duniani na inazungumzwa na watu wengi hivyo ni lazima watanzania wakawa mstari wa mbele kukikuza na kukiendeleza kwa kukizungumza kwa ufasaha”.Alisema Dkt Mwakyembe.
Aidha Dkt. Mwakyembe amemuagiza Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw.Godfrey Muingereza kuhakikisha kuwa katika mashindano yajayo ya ulimbwende washiriki wanatumia lugha ya Kiswahili katika mashindano ya ndani na watakapoiwakilisha nchi kimataifa.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bibi. Susan Mlawi ameongeza kuwa mdahalo huo ni muendelezo wa Kampeni ya Uzalendo na Utaifa inayotarajiwa kufikia kilele chake Disemba 08 mwaka huu ambapo itatanguliwa na matukio tofauti kiwemo Mijadala,makongamano na nyimbo mbalimbali na kauli mbiu mwaka huu ni “Kiswahili Uhai wetu,Utashi wetu.”
Pia katika mdahalo huo Kaimu Mkuu wa Chuo cha St. Johns University of Tanzania Prof.Yohana Msanjila aliiomba Serikali kuona umuhimu wa kutumia lugha ya Kiswahili katika somo la Uraia kwakua ndio somo linalozungumzia Utamaduni wa nchi pamoja na Uzalendo jinsi mtu anayoweza kuipenda na kuilinda nchi yake.
Vilevile mwanafunzi Edmund Kakoi kutoka shule ya Sekondari Dodoma alieleza kuwa ni lazima vijana kutambua kuwa luga ya Kiswahili sio lugha iliyopitwa na wakati bali ni lugha ambayo inaipa heshima nchi katika mataifa mbalimbali.
Katika mdahalo huo mada tatu ziliwasilishwa ikiwemo “Maisha na Uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius K.Nyerere yanavyoakisi Uzalendo na Utaifa” iliyowasilishwa na Dkt. Alfred Sebahene kutoka Idara ya Taaluma na Rushwa ya chuo hicho.
Mada nyingine “Mchango wa Lugha ya Kiswahili katika kukuza Uzalendo na Utaifa” iliyowasilishwa na Dkt. Stella Faustine kutoka Idara ya Kiswahili chuo kikuu cha Dodoma na mada ya tatu ilikua “Dhima ya Uzalendo na Utaifa katika Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda” iliyowasilishwa na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Dodoma.
Post A Comment: