Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri  zote nchini kuhakikisha wanatenga asilimia 2 ya bajeti zao  kwa ajili ya kuhudumia watu wenye ulemavu na kuwa suala hilo lipo kisheria.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya Siku  ya Fimbo Nyeupe duniani ambayo Kitaifa hapa nchini yamefanyikia Mkoani Mwanza.

Ndalichako amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais John Magufuli imeendelea  kuboresha mazingira ya watu wenye uleamavu ikiwa ni pamoja na kutoa ajira na kuwa katika ajira za mwaka jana  walimu 70 wasioona waliajiriwa.

“Niwahakikishie Watanzania kuwa Rais John Magufuli ni kiongozi anaejali sana watu wenye ulemavu ndiyo maana Wapo viongozi wenye ulemavu aliowateua kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika Serikali yake wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi,Mabalozi, na wengine ili wamsaidie katika kutekeleza majukumu ya kuliletea Taifa Maendeleo,” alisema Ndalichako.
Waziri Ndalichako pia amewataka Wazazi kuacha tabia ya kuwaficha watoto wasioona na badala yake wahakikishe  watoto  wote waliofika umri wa kwenda Shule wanaandikishwa kwa kuwa hivi sasa Elimu msingi inatolewa bila malipo na kuwa ulemavu siyo kikwazo Cha Maendeleo.

Akizungumza katika Maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye ulemavu nchini Tanzania Benedict Louis  amempongeza na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake wa kutambua jitihada na uwezo wa watu wenye ulemavu  na hivyo kuwateua wenye ulemavu kushika nafasi mbalimbali.

Louis ameeleza kuwa  Siku ya Fimbo Nyeupe  ni muhimu kwa kuwa inatoa fursa kwa wasioona kutathmini jitihada zinazofanywa na serikali katika kuleta ustawi kwa watu wenye ulemavu na kuwa Fimbo hiyo  ni nyenzo muhimu  ambayo inamsaidia asioona kutambua vikwazo vilivyo bmbele yake.

Kauli mbili  ya mwaka huu katika maadhimisho hayo ni “ Mafunzo ya TEHAMA kwa wasioona ni nyenzo Shirikishi ya uchumi wa Viwanda.”

Imetolewa na:
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
25/10/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: