Mwanamke mmoja nchini Uganda, ameshangaza wengi baada ya kujioa mwenyewe. 

Lulu Jemimah, mwanamke mwenye umri wa miaka 32 alijioa mwezi Agosti mwaka huu jijini Kampala na kudai kuwa kwa miaka kadhaa watu wamekuwa wakimuuliza kwamba lini angefunga ndoa. 

“Nikiwa na miaka 16, baba yangu aliandika hotuba yake kwa ajili ya kuisoma siku ya harusi yangu…kila nilipokuwa nasherehekea siku yangu ya kuzaliwa mama yangu alikuwa akiniombea na kwa miaka ya karibuni, maombi yake yalikuwa pamoja na kupata mume bora, ambaye atanifaa,” anasema.

Mwaka jana Jemimah alichaguliwa kujiunga na masomo ya juu ya uandishi na ubunifu katika chuo kikuu maarufu cha Oxford nchini Uingereza. 

Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo ya kielimu anasema bado watu waliendelea kumuuliza anapanga kuolewa lini, ili aanzishe familia na kupata watoto. 

“Hawaamini kuwa kinachonifanya kuwa macho usiku si hofu ya uwezekano wa kutopata bahati ya kutembea altarini kwenda kufunga ndoa,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, Jemimah anasema aliamua kuchukua uamuzi wa kuwatuliza.

“Nilipotimiza miaka 32, nikaamua kujioa… naamini nitajitunza na kujipa amani mwenyewe,” anasema.

Harusi yenyewe ilimgharimu kiasi cha dola za Marekani 2.62 tu, ambazo ilikuwa ni gharama ya usafiri mpaka mahali harusi hiyo ilipofanyika. 

“Rafiki yangu mmoja aliniazima gauni la harusi, mwingine akijitolea kuniremba… dada yangu aliniazima vito na kaka akaoka keki,” anasema. 

Waalikwa wote walielekezwa wapi pa kwenda na huko walitakiwa wajilipie gharama za vinywaji na chakula kwa pesa zao. 

“Ndoa ni kielelezo cha upendo na msimamo thabiti wa maisha, lakini kwa watu wengi nyumbani (Uganda) ni njia pekee ya mwanamke kujihakikishia usalama wa kifedha…hata mie nahitaji hivyo vitu, lakini tofauti pekee hapa ni kuwa nitajipata mwenyewe,” anasema.

Jemimah ameandika maelezo hayo ya maisha yake katika ukurasa wa mtandao wa kukusanya pesa kwa watu wenye uhitaji unaofahamika kama Go Fund Me. 

Tayari ameshakamilisha mwaka wa kwanza wa masomo kwa msaada wa watu 279, wakiwemo marafiki na watu asiowafahamu kabisa. 

Ili kumaliza masomo yake hayo ya uzamili, anahitaji pauni 10,000 kwa ajili ya ada na mahitaji mengine ya ziada. 

Mpaka kufikia mwanzoni mwa mwezi huu, tayari alishapata msaada wa pauni 4,000 zilizochangwa na watu 69.

Jemimah alianzisha maombi yake hayo wiki iliyopita. Awali alishawahi kulala maktaba kutokana na kukosa pesa ya kodi ya chumba.

Anasema haikuwa dhamira yake kuomba msaada, lakini hofu ya kufutwa chuo kutokana na kukosa fedha imemlazimu afanye hivyo.

“Uandishi ndio kitu pekee kinachonifanya niilewe dunia, ni mapenzi yangu, nimepata bahati ya kuwa katika chuo bora chenye wanafunzi makini na walimu wenye weledi mkubwa,” anasema na kuongeza:

“Nimefikia hapa kutokana na msaada wa marafiki na watu nisiowafahamu…kwa mara nyingine tena naomba msaada wenu.” anasema. 

BBC

Via>Nipashe
Share To:

Anonymous

Post A Comment: