Na Yusuph Mussa
ZAO la mkonge lililetwa hapa nchini mwaka 1893 na Mjerumani Dkt. Richard Hindolf, na kupandwa kwa mara ya kwanza kwenye Shamba la Kikokwe, sasa ni sehemu ya Shamba la Mkonge Mwera, Wilaya ya Pangani mkoani Tanga. Unapozungumzia mkonge kwa wananchi wa Tanga, Tanzania, Afrika Mashariki na Dunia nzima, maana yake unazungumzia maisha ya watu.
Kwani wananchi karibu mikoa yote ya Tanzania na mataifa ya Rwanda, Burundi, Msumbiji, Kenya, Malawi, Zambia na Zimbabwe, walikwenda Tanga kutafuta kazi na vibarua. Huku mataifa ya Ulaya, Asia na Amerika Kusini wakija kuwekeza kwa kufungua viwanda mbalimbali kwenye mikoa ya Tanga na Morogoro ambayo ilishamiri zao la mkonge.
Hadi kufikia mwaka 1964, uchumi wa Mkoa wa Tanga na Taifa, ulibebwa na mkonge, ambapo mwaka huo, Tanzania ilizalisha tani 230,000 hadi tani 240,000 za mkonge kwa mwaka kutoka kwenye mashamba yenye ukubwa wa hekta 487,000. Hata hivyo mashamba hayo yalipoteza uwezo wake wa kuzalisha baada ya Serikali kuyataifisha kutoka kwa mabepari (sasa wawekezaji) wakati wa Azimio la Arusha mwaka 1967, na kuweza kuyaendesha yenyewe kupitia Shirika la Mkonge Tanzania (SMT), na baadae Mamlaka ya Mkonge Tanzania (MMT).
Hata hivyo mashirika hayo yalifilisika, na hadi kufikia mwishoni mwa miaka ya 1990 yalikuwa 'mfu', ndipo mwaka 1997 Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa, alipobinafsisha mashamba hayo na mali zake zote.
Akifanya mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Katani Ltd Juma Shamte, alieleza mafanikio yaliyopatikana kwa miaka 20 tangu kampuni hiyo kununua mashamba matano ya mkonge kutoka serikalini.
"Mwaka 1997 wawekezaji wazawa 85 ambao walikuwa wataalam wa mkonge, waliweka nguvu zao pamoja za kiuchumi na kitaaluma kununua rasilimali ambazo leo ndiyo Kampuni ya Katani Ltd. Mwaka 1998 Katani Ltd, ilikamilisha mkataba wa manunuzi na Serikali pamoja na
mpango wake wa uwekezaji ikiwemo upembuzi yakinifu wa mfumo wa Wakulima wa Mkonge (SISO) ambao ni wa kilimo cha kibiashara.
"Msingi wa SISO ni mkulima na kiwanda
kushirikiana kuzalisha na kuuza pamoja kwa kugawana majukumu kimkataba. Katani Ltd imetoa fursa ya kulima mkonge kwenye SISO kwa wanavijiji, wafanyakazi na Watanzania wote kuweza kuwa kwenye kilimo cha kibiashara na mnyororo wa
viwanda" alisema Shamte.
Alisema Katani Ltd iko kwenye uwekezaji wa uchumi wa viwanda muda mrefu.
Mwaka 1999 utekelezaji wa SISO ulianza na upandaji wa hekta 30 wa kaya 54
katika Shamba la Mkonge Mwelya. Hadi mwaka 2017 upandaji umeongezeka kufikia hekta 8,268 sawa na ekari 20,670 kwa kaya 1,267 za wakulima katika mashamba matano yenye jumla ya hekta 20,000 sawa na ekari 50,000. Uzalishaji wa singa (brashi), umepanda kutoka tani 849 mwaka 2005 hadi tani 4,587 mwaka 2017, sawa na ongezeko la mara tano na nusu.
Katani Ltd imetoa mikopo kwa wakulima yenye thamani ya sh. bilioni nane (8) kwa ajili ya kupanda na kutunza mkonge. Pamoja na hilo, imetoa ruzuku kwa miaka 13 kwa wakulima kutoka kwenye faida yake kuhakikisha wakulima
wanaimarika katika shughuli zao za kilimo. Mwaka 2005 wakulima walipata mapato ya sh.milioni 139 kwa mwaka mzima, na mpaka kufika mwaka 2017, walipata mapato ya sh. bilioni 3.7 kwa mwaka. Wakulima wameweza kupata mapato ya jumla ya sh. bilioni 20 hadi kufika mwaka 2017.
"Wakulima wameweza kujenga nyumba bora za kisasa, kusomesha watoto shule, kutumia huduma za umeme, maji, mawasiliano, fedha na kumiliki vyombo vya usafiri wa binafsi pamoja na kupata huduma za afya na ustawi wa jamii. Kuna wakulima 870 ambao ni wanachama wa hiari wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)" alisema Shamte.
"Katani Ltd imesimamia wakulima kujiunga kwenye vyama vya ushirika vya AMCOS na SACCOS kujenga uwezo wa kusimamia na kugharamia shughuli zao wenyewe na baadae kuchukua hisa katika umiliki wa viwanda vya Katani Ltd. Katani Ltd imejenga viwanda vinne na kukarabati vitatu kati ya kumi kuweza kuwahudumia wakulima kikamilifu kwa kuwa na uwezo wa kusindika mkonge wote uliopo" alisema Shamte.
Katani Ltd inaendesha viwanda kama vituo vya kilimo kwa kutoa huduma za ugani, masoko, fedha, pembejeo, uhandisi, usindikaji na utafiti kuhakikisha wakulima wanapata mahitaji yote ya kuendesha shughuli zao. Pia imehamasisha wakulima kuanza kupanda mkonge nje ya maeneo ya SISO na kupata huduma kwenye viwanda vya kampuni. Katani Ltd imeandaa kampuni kuweza kuwaingiza wakulima kupitia vyombo vyao kwenye umiliki wa hadi asilimia 40 ya viwanda vya kampuni kuweza kushiriki moja kwa moja kwenye masoko kama wamiliki.
Katani Ltd imesimamia utafiti uliozalisha kiwanda cha kwanza duniani cha Nishati ya Mkonge na kilimo bora cha mkonge kilichopo Kiwanda cha Mkonge Hale, wilayani Korogwe, kwani kinazalisha nishati ya umeme kumwezesha mkulima kuongeza mapato. Kumefanyika maboresho ya mikataba ya SISO na kumepatikana mfumo wa
mgawanyo wa mapato kuboresha maslahi ya kibiashara ya pande zote kwakuwepo na asilimia inayozingatia hali halisi ya utendaji wa sasa.
"Katani Ltd inachangia kikamilifu kwenye shughuli za kijamii, utoaji wa ajira na kodi za Serikali kuweza kuwa mwekezaji mkubwa katika Wilaya ya Korogwe, Muheza na Mkoa wa Tanga kwa ujumla.Kuna ubia kati ya Serikali na kampuni (PPP) ambao unawezesha skimu ya SISO kuwa na maendeleo ambayo ni endelevu kwa manufaa ya wadau wote. Katani Ltd imewekeza kwenye hazina ya rasilimali watu yenye taaluma ya uhandisi, uchumi na biashara, kilimo na masoko kuweza kuhudumia SISO kikamilifu na kuleta ubunifu na ushindani" alisema Shamte.
Post A Comment: