Katibu  Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amemjibu Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye amedai anaona kama nchi ina hofu na chuki miongoni mwa baadhi ya wananchi wake.

Hayo yamesemwa l leo Ijumaa, Oktoba 12, 2018 wakati wa Mdahalo wa Wazi wa Kongamano la Kumbukizi ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wasomi, wanasiasa, wanazuoni na wataalam wa masuala ya siasa kutoka ndani na nje ya nchi.

“Mjumbe wa Kamati Kuu amesema habari ya hofu ni kweli, wezi wa mali za umma, wakwepa kodi, matapeli wa kisiasa, walionunua mashirika ya umma bila kuyaendeleza, walioingia kwenye mikataba ya kutuibia mali, madalali lazima wataishi na hofu.

“Watu wenye midomo mirefu, wanaingia kwenye mitandao wa kijamii na kuanza kuwatisha wananchi…wanawapandikizia hofu zao wakidai ni hofu za nchi nzima… hofu zao zinazotokana na uporaji wa mali za wananchi, tutawafuata huko huko hata kama wakikimbilia katika siasa.

“Wakianza kusambaza hofu zao na kuziingiza kwa wananchi tusikubali, hofu za wananchi ni maji safi, ni Elimu bora, haki Mahakamani, ni haki ya Ardhi yao, ni tija ya uzalishaji wao na mapato ya jasho lao ya haki. Ziko hofu za kuchonga, watu wana midomo mirefu mipana, wanaingia kwenye mitandao ya kijamii kutisha wananchi wakati wanahofu zao halisi.

Bashiru amesema suala la usalama lijadiliwe kwa umakini wa aina yake kwa kuangalia muktadha wa dunia ulivyo na kutowakatisha tamaa vijana ambao wanalinda usiku na mchana tena kwa ujira mdogo.

“Mimi ninao vijana ndani ya CCM na CHADEMA wewe utakuwa nao, imekuwa nadra katika ushindani kukaa kusalimiana na kupendana, wanafukuzana unafikiri sio wa nchi moja halafu polisi wawaache, watoboane macho itakuwa ni kutowajibika.

“Mimi kama Katibu Mkuu nitapigia debe bajeti za serikali kwenye vyuo vyetu vikuu vya umma ili vifanye kazi ya kukuza maarifa, vizalishe wasomi watakao tusaidia kutukomboa kifikra na kimaendeleo. Hii ndio namna ya kuiponya nchi yetu, mijadala itatufanya tujisahihishe, tumekosea sana katika nchi hii, tumepotea sana katika nchi hii na mbaya zaidi tumeanza kuogopa kusema ukweli,” alisema Bashiru.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: