Aliyekuwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyangh’wale mkoani Geita, Carlos Gwamagobe na watumishi wengine watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Geita kwa makosa ya uhalifu na kuisababishia hasara serikali jumla ya shilingi Bilioni 2.8

Washtakiwa hao wanatuhumiwa kutenda makosa matano ambayo ni kughushi nyaraka,kutakatisha fedha, udanganyifu na kusababishia hasara serikali ambapo wamesomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Jovitha Kato.

Washitakiwa hao ni aliyekuwa mkurugenzi Carlos Gwamagobe, Donatus Pangani (Mweka Hazina) Godson Mberwa , Alfred Chabila, Sylvester Kabora , na Gudola Tabu wote wakiwa watumishi wa Halmashauri ya Nyang’hwale.

Akiwasomea mashitaka Wakili wa Serikali Hezron Mwasimba,kwa kusaidiana na wakili wa serikali Erasto Anosisye na Fred Nyaupumbwe, alisema washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka matano.

Alisema washitakiwa wote kwa pamoja katika kosa la kwanza wanadaiwa kuwa kati ya tarehe 1 Januari mwaka 2016 na mwezi Juni 30 mwaka huu, wanadaiwa kujihusisha na mtandao wa udanganyifu kosa ambalo ni kinyume na kifungu cha 4(1), (b), ya jedwali la kwanza na kifungu 57(1) na kifungu cha 60 cha sheria ya uhujumu uchumi.

Wakili Mwasimba alisema kosa la pili washitakiwa wote sita , ambapo wanatuhumiwa kwa kosa la kughushi nyaraka ambalo ni kinyume kifungu cha 333 cha kanuni ya adhabu.

Inadaiwa kuwa mnamo Januari 1 na mwezi Juni 30, katika Halmashauri ya Nyangh’wale mkoani Geita, kwa muda tofauti, watuhumiwa kwa pamoja walitengeneza nyaraka za kughusi zenye thamani ya shilingi 747,375,565/= ambazo zilionyesha kuwa zimetumika kulipa watumishi kwa mahitaji mbalimbali, jambo ambalo halikuwa kweli.

Katika kosa la tatu, inadaiwa kuwa watuhumiwa wote sita, walighushi nyaraka za serikali zenye gharama ya shilingi Bilioni 2, 061,161,889/- nyaraka ambayo ilionyesha kuwa Halmashauri ya Nyang’hwale imetumia fedha hizo kwa ajili ya kuwalipa wananchi katika vijiji vya Bukungu na Ikangala kama malipo ya posho za vikao (sitting allowance), posho za semina na posho za extra duty jambo ambalo siyo kweli.

Aidha Mwasimba aliendelea kuwasomea mashitaka washitakiwa hao ambapo katika kosa la nne, ambalo ni la Utakatishaji wa fedha (Money laundering) ambalo ni kinyume cha sheria kifungu namba 12 (d) na 1(a) cha sheria ya makosa ya utakatishaji fedha.

Inadaiwa kuwa kati ya Januari 1 mwaka 2016, na kati ya June 30, mwaka huu, kwa nyakati tofauti watuhumiwa hao kwa pamoja walijipatia kiasi cha shilingi Bilioni 2,808,987,484/- isivyo halali, mali ya Halmashauri ya wilaya ya Nyangh’wale kosa ambalo ni kinyume cha sheria namba 12(d) na kifungu namba 13(a), cha sheria ya makosa ya utakatishaji fedha.

Watuhumiwa wote walinyimwa dhamana kufuatia kile hakimu Kato kufafanua kuwa kwa mujibu wa shria, kosa namba nne ambalo ni la utakatishaji wa fedha halina dhamana.

Wakili Mwasimba alisema washtakiwa wamekosa dhamana kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa kosa la kutakatisha fedha.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Oktoba 22 ambapo watuhumiwa hao walirudishwa rumande.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: