Serikali imekipongeza Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kwa kusimamia kwa ufanisi ukarabati wa Chuo cha Ualimu Tandala kilichopo Wilayani Makete Mkoani Njombe.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.William Ole Nasha wakati akikagua ukarabati wa Miundombinu ya Chuoni hapo mradi ambao unafadhiliwa na Wizara hiyo.

“Chuo Kikuu Cha Sayansi na Teknolojia Mbeya wamekuwa wakifanya kazi nzuri zakuridhisha katika miradi yao yote waliokabidhiwa Wizara na hivyo ndivyo inavyotakiwa, Serikali inapotoa fedha kwa ajili yakurejesha hadhi ya Miundombinu ya Shule, vyuo na Miundombinu mingine zilenge kukamilisha kazi hizo na sio kutanguliza maslahi binafsi na kuingiza Serikali kwenye hasara,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha.

Naibu Waziri huyo amezitaka Taasisi nyingine za Serikali kuwa waadilifu katika matumizi ya fedha pindi Serikali inapotoa fedha kwa ajili yakuboresha miundombinu ili malengo  yaliyokusudiwa yaweze kutimia huku akiwataka  wanafunzi wa Chuo hicho kusoma kwa bidii na kufaulu kwa kiwango cha juu

Kiongozi huyo ameeleza kuwa  Serikali ilisitisha kutoa ajira kwa wingi kwa lengo la kupitia mifumo ya ajira upya kwani iliyokuwepo ilizalisha wafanyakazi hewa na wenye vyeti feki hivyo ilikuwa ni lazima kufanya hivyo ili kuiepusha serikali kuingia katika hasara.

Nae Mkuu wa Chuo cha Ualimu Tandala Philip Khamisi alisema mpaka sasa Chuo hicho kina wanachuo 225 huku wakitegemea kupokea wanachuo 342 ambapo itafanya idadi ya wanachuo kufika 567.

Wizara ilitoa zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya Chuo Cha Tandala ambacho Miundombinu yake ilikuwa imechaka.

Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
4/10/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: