Unaweza kusema yaliyotabiriwa na mbunge wa Ukerewe (Chadema), Joseph Mkundi juu ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere yametimia.
Ndivyo unavyoweza kusema baada ya jana mchana kivuko hicho kuzama katika Ziwa Victoria mita 50 kabla ya kutia nanga huku abiria 37 waliokuwa kwenye kivuko hicho wakifariki dunia hadi zoezi la uokoaji lilipositishwa jana jioni.

Kivuko hicho kilichokuwa kikitokea katika Kisiwa cha Bugolora kuelekea Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe, kinadaiwa kilikuwa kimepakia zaidi ya abiria 100, wengi wakiwa wanaelekea kwenye gulio.

Katika moja ya swali alilouliza bungeni hivi karibuni, Mkundi alitaka kupata kauli ya Serikali jinsi itakavyoshughulikia kivuko hicho ili kisije kusababisha maafa.

Video inayomuonyesha mbunge huyo akiuliza swali hilo bungeni ilianza kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii jana jioni baada ya kivuko hicho kuzama.

“Naomba kupata kauli ya Serikali, ni suala ambalo tumekuwa tunalishughulikia mara kwa mara, tuna kivuko kinachounganisha Ukerewe na kisiwa cha Ukara, kivuko hiki kinahudumia watu zaidi ya 50,000,” amesema.

“Kimekuwa kinaleta shida mara kwa mara na nimekuwa nawasiliana na wizara, sipendi siku moja tuje hapa kuomba rambirambi kwa sababu ya wananchi waliozama katika kivuko kile.”

Taarifa za kuzama kivuko hicho zilizokumbusha tukio la kuzama kwa meli ya MV Bukoba Mei 21, 1996 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 800, zilitolewa kwa nyakati tofauti na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, George Nyamaha.

Inaelezwa kuwa kivuko hicho kilikuwa kimepakia tani nyingi za mizigo na kilibeba idadi kubwa ya watu tofauti na uwezo wake na kwamba kilipinduka na kikageukia kilipokuwa kinatoka na kujifunika hali iliyosababisha kuwafunika watu wengi na wakati huo kivuko hicho kilikuwa kimezama upande mmoja na chini kulikuwa na watu.

Habari kutoka eneo la tukio zinasema ilipofika saa 11:45 jioni waokoaji walitumia mitumbwi wakati wakisubiri meli iliyokuwa ikitokea Mwanza mjini. 

Taarifa za awali zilieleza kuwa kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba abiria 100, tani 25 za mizigo na magari madogo matatu kilizidisha mizigo likiwamo lori kubwa la mahindi.

Kivuko hicho kilifungwa injini mpya Julai mwaka huu baada ya awali kupata hitilafu na kimekuwa kikitoa huduma kutoka Kisiwa cha Bugolora –Ukara wilayani Ukerewe tangu mwaka 2004.

Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo, Denis Kwesiga alisema kivuko hicho kilikuwa kimepakia magari mawili likiwamo la mizigo lililokuwa limesheheni magunia ya mahindi.

Alisema kivuko hicho kimekuwa kikizidisha mizigo na abiria siku za Alhamisi kutokana na gulio hilo la Ukara.
CHANZO- MWANANCHI

Share To:

Anonymous

Post A Comment: